The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, walipomjia Yesu Mafariseo na waandishi waliotoka Yerusalemu, wakasema:[#5 Mose 4:2; Luk. 11:38.]
2Kwa sababu gani wanafunzi wako hawayafuati mazoezo ya wakale? Kwani hawanawi mikono wakila chakula.
3Ndipo, alipowajibu akisema: Nanyi sababu gani hamlifuati agizo lake Mungu kwa ajili ya mazoezo ya wakale wenu?
4Kweli Mungu alisema: Mheshimu baba yako na mama yako! na tena: Atakayemwapiza baba au mama sharti afe kwa kuuawa![#2 Mose 20:12; 21:17.]
5Lakini ninyi husema: Mtu akimwambia baba au mama: Mali, unazozitaka, nikusaidie nazo, amepewa Mungu, basi, ni vema.[#Fano. 28:24.]
6Hivyo hatamheshimu baba na mama tena; ndivyo, mlivyolitangua Neno la Mungu kwa ajili ya mazoezo ya wakale wenu.
7Enyi wajanja, Yesaya aliwafumbua vizuri hayo mambo yenu aliposema:[#Yes. 29:13.]
8Ukoo huu huniheshimu kwa midomo tu,
lakini mioyo yao inanikalia mbali.
9Hivyo hunicha bure,
kwani hufundisha mafundisho yaliyto maagizo ya watu tu.
10Akaliita kundi la watu, akawaambia: Sikilizeni, mjue maana!
11Kinachoingia kinywani sicho kinachomtia mtu uchafu, ila kinachotoka kinywani ndicho kinachomtia mtu uchafu.[#Mat. 12:34; 1 Tim. 4:4; Tit. 1:15.]
12Ndipo, wanafunzi walipomjia, wakamwuliza: Unajua, ya kuwa Mafariseo walikwazwa walipolisikia neno hilo?
13Naye akajibu akisema: Kila mmea, asioupanda Baba yangu wa mbinguni, utang'olewa.
14Waacheni hao! Ni mapofu wenye kuongoza vipofu wenzao. Kipofu akimwongoza kipofu mwenziwe, wote wawili watatumbukia shimoni.[#Mat. 23:24; Luk. 6:39; Rom. 2:19.]
15Petero akajibu, akamwambia: Tuelezee mfano huu!
16Naye akasema: Kumbe nanyi hajaerevuka hata leo!
17Hamjui, kila kitu kinachoingia kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?
18Lakini yanayotoka kinywani mwa mtu yametoka moyoni mwake, nayo ndiyo yanayomtia mtu uchafu.
19Kwani moyoni hutoka mawazo mabaya: uuaji, uzinzi, ugoni, wizi, usingiziaji, matusi.[#1 Mose 8:21.]
20Haya ndiyo yanayomtia mtu uchafu; lakini kula na mikono isiyonawiwa hakumtii mtu uchafu.
21*Yesu alipotika huko akajiepusha kwenda pande za Tiro na Sidoni.
22Mara mwanamke wa Kikanaani aliyekaa mipakani huko akatokea, akapaza sauti akisema: Nihurumie, Bwana, mwana wa Dawidi! Binti yangu anapagawa vibaya na pepo.
23Lakini hakumjibu neno. Wanafunzi wake wakamjia, wakamwomba wakisema: Mwache, aende zake! Kwani anatupigia kelele nyuma yetu.
24Naye akajibu: Sikutumwa pengine, ni kwao tu walio kondoo waliopotea wa mlango wa Isiraeli.[#Mat. 10:6; Rom. 15:8.]
25Naye mwanamke akaja, akamwangukia, akasema: Bwana, nisaidie!
26Naye akajibu akisema: Haifai kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia vijibwa.
27Mwanamke akasema: Ndio Bwana, lakini nao vijibwa hula makombo yanayoanguka mezani pa bwana zao.
28Ndipo, Yesu alipojibu akimwambia: Mama, umenitegemea kabisa. Na uvipate unavyovitaka! Saa ile ile binti yake akapona.*[#Mat. 8:10,13.]
29Kisha Yesu akaondoka huko, akafika kandokando ya bahari ya Galilea, akapanda mlimani, akakaa huko.[#Mar. 7:31.]
30Wakamjia makundi mengi ya watu walio na viwete na wenye vilema na vipofu na mabubu na wengine wengi pamoja nao. Wakawaweka miguuni pa Yesu, naye akawaponya.
31Ikawa, makundi ya watu wakastaajabu waliupoona, mabubu wakisema, nao waliolemaa wakiwa wazima, nao viwete wakitembea, nao vipofu wakiona. Wakamtukuza Mungu wa Isiraeli.[#Mar. 7:37.]
32Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema: Kundi hili la watu nalionea uchungu, kwa kuwa wameshinda kwangu siku tatu, wasione chakula. Nami sitaki kuwaaga, waende zao pasipo kula, maana wasije, wakazimia njiani.[#Mat. 14:14.]
33Wanafunzi wakamwambia: Hapa nyikani tutapata wapi mikate inayotosha kuwashibisha watu walio wengi kama hawa?
34Yesu akawauliza: Mnayo mikate mingapi? Nao waliposema: Tunayo saba na visamaki vichache,
35akawaagiza hao watu wengi, wakae chini.
36Kisha akaitwaa ile mikate saba na samaki, akashukuru, akaimega akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawapa wao wa makundi ya watu.
37Wote wakala, wakashiba; kisha wakayaokota makombo ya mikate yaliyosalia, wakajaza makanda saba.
38Nao waliokula walikuwa waume tu 4000 pasipo wanawake na watoto.
39Kisha akawaaga makundi, waende zao, akaingia chomboni, akaja mipakani kwa Magadala.