Mateo 22

Mateo 22

Ndoa ya mwana wa mfalme.

(2-14: Luk. 14:16-24.)

1Yesu akaendelea kusema tena kwa mifano akiwaambia:[#Yoh. 3:29.]

2Ufalme wa mbingu umefanana na mtu mfalme aliyemfanyia mwanawe arusi.

3Akawatuma watumwa wake, wawaite walioalikwa arusini; nao hawakutaka kuja.

4Akatuma watumwa wengine akisema: Waambieni walioalikwa: Tazameni, nimekwisha kuiandaa karamu yangu, ng'ombe na vinono vimechinjwa, vyote viko tayari, njoni arusini![#Mat. 21:36.]

5Lakini wale wakavibeza, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwa uchuuzi wake.

6Nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawapiga, wakawaua.

7Lakini mfalme akachafuka, akawatuma askari wake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.[#Mat. 24:2.]

8Hapo akawaambia watumwa wake: Arusi iko tayari, lakini walioalikwa hawakufaa.

9Basi, nendeni, mfike kwenye njia panda mwalikie arusini wo wote, mtakaowaona![#Mat. 13:47; 21:43.]

10Wale watumwa wakatoka, wakaenda njiani, wakawakusanya wote, waliowaona, wabaya na wema; arusi ikajaa wageni.

11Lakini mfalme alipoingia kuwatazama wageni akaona mle mtu asiyevaa nguo inayopasa arusini.

12Akamwambia: Mwenzangu, uliingiaje humo, nawe hukuvaa nguo inayopasa arusini? Yule akanyamaza kimya.

13Ndipo, mfalme alipowaambia watumishi: Mfungeni miguu na mikono, mmtupe penye giza lililoko nje! ndiko, kitakakokuwa kilio na kukereza meno.[#Mat. 8:12.]

14Kwani waalikwao ni wengi, lakini wachaguliwao ni wachache tu!*[#Mat. 20:16.]

Shilingi ya kodi.

(15-22: Mar. 12:13-17; Luk. 20:20-26.)

15Mafariseo wakaenda zao, wakala njama ya kumtega kwa maneno yake.

16Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na watu wa Herode, wakasema: Mfunzi, tumekujua, ya kuwa wewe ni mtu wa kweli, nayo njia ya Mungu unaifundisha, ilivyo kweli, tena humwuliziulizi mtu ye yote, kwani hutazami nyuso za watu.[#Mar. 3:6; Yoh. 3:2; 5:41.]

17Tuambie, unaonaje wewe? Iko ruhusa ya kumtolea Kaisari kodi au haiko?

18Kwa kuutambua ubaya wao Yesu akasema: Enyi wajanja, mwanijaribiaje? Nionyesheni fedha ya kodi! Walipomletea shilingi,

19akawauliza: Chapa hiki cha nani? Maandiko nayo ya nani?

20Wakasema: Ni yake Kaisari.[#Rom. 13:7.]

21Ndipo, alipowaambia: Basi, yaliyo yake Kaisari mtoleeni Kaisari, naye Mungu yaliyo yake Mungu!

22Walipoyasikia wakastaajabu, wakamwacha, wakaenda zao.*[#Yoh. 8:9.]

Kufufuka.

(23-33: Mar. 12:18-27; Luk. 20:27-40.)

23Siku ileile wakamjia Masadukeo wanaosema: Hakuna ufufuko, wakamwuliza[#Tume. 23:6,8.]

24wakisema: Mfunzi, Mose alisema: Mtu akifa asipokuwa na wana, nduguye amwingilie mkewe, amzalie mkubwa wake mwana![#1 Mose 33:8; 5 Mose 25:5-6.]

25Kwetu kulikuwa na waume saba walio ndugu. Wa kwanza akaoa, akafa; kwa sababu hakuwa na mwana, alimwachia nduguye mkewe.

26Vilevile na wa pili na wa tatu na wale saba wote.

27Mwisho wao wote akafa naye mwanamke.

28Basi, katika ufufuko atakuwa mke wa yupi wa hao saba? Kwani wote waliokuwa naye.

29Yesu akajibu, akawaambia: Mwapotelewa, kwani hamyajui Maandiko wala nguvu ya Mungu.

30Kwani katika ufufuko hawataoa, wala hawataolewa, ila watakuwa, kama malaika walivyo mbinguni.

31Lakini kwa ajili ya ufufuko wa wafu hamkusoma, mliloambiwa na Mungu aliposema:

32Mimi ni Mungu wa Aburahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo? Basi, Mungu siye wa wafu, ila wao walio hai.[#Mat. 8:11; 2 Mose 3:6.]

33Watu walipoyasikia wakastushwa kwa ufundisho wake.[#Mat. 7:28.]

Agizo kubwa.

(34-40: Mar. 12:28-31; Luk. 10:25-28)

34*Mafariseo waliposikia, ya kuwa amewashinda Masafukeo na kuwafumba vinywa, wakakusanyika pamoja.

35Mmoja wao aliyekuwa mjuzi wa Maonyo yake Mungu akamwuliza kwa kumjaribu akisema:

36Mfunzi, agizo lililo kubwa katika Maonyo yake Mungu ni lipi?[#5 Mose 6:5.]

37Naye akamwambia: Umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa mawazo yako yote!

38Hili ndilo agizo lililo kubwa, tena ni la kwanza. Nalo la pili limefanana nalo,

39ndilo hili: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe![#3 Mose 19:18; Rom. 13:9.]

40Katika haya maagizo mawili yamo Maonyo yote ya Mungu pamoja na Wafumbuaji.[#Mat. 7:12; Rom. 13:10; Gal. 5:14.]

Mwana wa Dawidi.

(41-46: Mar. 12:35-37; Luk. 20:41-44.)

41Wao Mafariseo walipokusanyika, Yesu akawauliza[#Rom. 1:3.]

42akisema: Mwamwonaje Kristo kuwa ni mwana wa nani? Wakamwambia: Wa Dawidi.

43Akawauliza: Tena Dawidi alimwitaje Bwana kwa nguvu ya Roho aliposema:

Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu,

44mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako?[#Mat. 26:64; Sh. 110:1.]

45Basi Dawidi akimwita Bwana, anakuwaje mwana wake?

46Hata mmoja hakuweza kumjibu neno, wala toka siku ile hakuwako mtu aliyejipa moyo wa kumwuliza neno tena.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania