Mateo 27

Mateo 27

(1-2: Mar. 15:1; Luk. 22:66; Yoh. 18:28-32.)

1Ilipokuwa asubuhi, watambikaji wakuu wote na wazee wa kwao wakamlia Yesu njama, kwamba wamwue.[#Luk. 23:1; Yoh. 18:31-32.]

2Wakamfunga, wakaenda naye, wakamtia mikononi mwa Pilato aliyekuwa mtawala nchi.

Kufa kwa Yuda.

3Hapo Yuda aliyemchongea akamwona, ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, akajuta, akazirudisha zile fedha 30 kwa watambikaji wakuu na kwa wazee[#Mat. 26:15.]

4akisema: Nimekosa nilipotoa mtu asiyepaswa na kumwagwa damu yake. Wale wakasema: Jambo hilo hatumo, litazame mwenyewe!

5Ndipo, alipozitupa zile fedha Jumbani mwa Mungu, akaondoka, akaenda zake, akajinyonga.[#2 Sam. 17:23; Tume. 1:18.]

6Kisha watambikaji wakuu wakaziokota zile fedha, wakasema: Ni mwiko kuzitia katiaka sanduku ya vipaji, kwa kuwa ni fedha za damu.[#Mar. 12:41.]

7Wakazipigia shauri, wakazinunua shamba la mfinyanzi, liwe la kuzikia wageni.

8Kwa hiyo shamba lile linaitwa hata leo Shamba la Damu.[#Tume. 1:19.]

9Ndipo, yalipotimia, mfumbuaji Yeremia aliyoyasema: Wamezichukua fedha 30, ni upato wa mtu aliyeuzwa, waliomnunua kwa wana wa Isiraeli;[#Yer. 18:2; 32:6-9; Zak. 11:12,13.]

10wakazitoa kununua shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniambia.

Yesu mbele ya Pilato.

(11-14: Mar. 15:2-5; Luka. 23:2-3; Yoh. 18:29-38.)

11Yesu alipopelekwa mbele ya mtawala nchi, mtawala nchi akamwuliza akisema: Wewe ndiwe mfalme wa Wayuda? Yesu akamwambia: Wewe unavyosema, ndivyo.

12Tena aliposutwa nao watambikaji wakuu na wazee hakujibu neno.[#Mat. 26:63; Yes. 53:7.]

13Pilato alipomwambia: Husikii yote, wanayokusimangia?

14hakumjibu hata neno moja. Ikawa, mtawala nchi akastaajabu sana.[#Yoh. 19:9.]

(15-26: Mar. 15:6-15; Luk. 23:13-25; Yoh. 18:39-19:1.)

15*Kwa desturi ya sikukuu mtawala nchi alikuwa amezoea kuwafungulia mfungwa mmoja, watu wengi waliyemtaka.

16Siku zile palikuwa na mfungwa aliyejulikana kwa ubaya, jina lake Baraba.

17Walipokusanyika, Pilato akawauliza: Mwamtaka yupi, niwafungulie? Baraba au Yesu anayeitwa Kristo?

18Kwani aliwajua, ya kuwa wamemtoa kwa wivu.[#Mat. 21:38; Yoh. 11:47-48; 12:19.]

19Naye alipoketi katika kiti cha uamuzi, mkewe akatuma kwake kumwambia: Usijitie katika jambo la yule mwongofu! Kwani nimeteseka mengi kwa ajili yake katika ndoto za usiku wa leo.

20Lakini watambikaji wakuu na wazee wakawashurutisha makundi ya watu, wamtake Baraba, wamwangamize Yesu.

21Mtawala nchi akajibu akiwaambia: Katika hawawawili mwamtaka yupi, niwafungulie? Wakasema: Baraba!

22Pilato akamwambia: Basi, Yesu anayeitwa Kristo nimfanyie nini? Wakasema wote: Na awambwe msalabani!

23Aliposema: Ni kiovu gani, alichokifanya? wakakaza kupiga makelele wakisema: Na awambwe msalabani!

24Pilato alipoona, ya kama hakuna linalofaa, ila matata yatakuwako mengi, akatwaa maji, akanawa mikono yake machoni pa watu, akasema: Mimi simo katika damu ya mtu huyu mwongofu, tazameni, ni shauri lenu![#5 Mose 21:6.]

25Ndipo, watu wote walipojibu wakisema: Damu yake itujie sisi na watoto wetu![#Mat. 23:35; Tume. 5:28.]

26Kisha akawafungulia Baraba, lakini Yesu akamtoa, apigwe viboko, kisha awambwe msalabani.

Kilemba cha miiba.

(27-31: Mar. 15:16-20; Yoh. 19:2-3.)

27Ndipo, askari wa mtawala nchi walipompeleka Yesu bomani, wakakita kikosi chote cha askari, waje hapo, alipokuwa.

28Wakamvua nguo zake, wakamvika kanzu nyekundu ya kifalme.

29Wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani, wakampa mwanzi mkononi mwake mwa kuume, wakampigia magoti, wakamfyoza na kusema: Pongezi, mfalme wa Wayuda!

30Kisha wakamtemea mate, wakaushika ule mwanzi, wakampiga kichwani.[#Yes. 50:6.]

31Walipokwisha kumfyoza wakamvua kanzu ya kifalme, wakamvika tena nguo zake, wakampeleka, wamwambe msalabani.*

Kuwambwa msalabani.

(32-56: Mar. 15:21-41; Luk. 23:26; 33-49; Yoh. 19:16-30.)

32Walipotoka wakaona mtu wa Kirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha, amchukulie msalaba wake.

33Walipofika mahali panapoitwa Golgota, maana yake: Fuvu la Kichwa,

34wakampa mvinyo iliyochanganyika na maji ya nyongo, anywe. Naye alipoyaonja hakutaka kunywa.[#Sh. 69:22.]

35Walipokwisha kumwamba msalabani wakazigawanya nguo zake na kuzipigia kura, kusudi yatimie yaliyosemwa na mfumbuaji kwamba:

Wakajigawanyia nguo zangu, nalo vazi langu wakalipigia

kura.

36Wakakaa wakimlinda palepale.

37Juu ya kichwa chake wakabandika andiko la mashtaka yake ya kwamba: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYUDA.

38Pamoja naye wakawambwa misalabani wanyang, anyi wawili, mmoja kuumeni, mmoja kushotoni.[#Yes. 53:12.]

39Waliopita wakamtukana, wakavitingisha vichwa vyao[#Sh. 22:8; 109:25.]

40wakisema: Wewe unayelivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe! Ukiwa Mwana wa Mungu shuka msalabani![#Mat. 26:61; Yoh. 2:19.]

41Vilevile nao watambikaji wakuu pamoja na waandishi na wazee wakamfyoza wakisema:

42Wengine aliwaokoa, lakini mwenyewe hawezi kujiokoa. Kama ndiye mfalme wa Waisiraeli, ashuke sasa hivi msalabani! Ndivyo, tutakavyomtegemea nasi.

43Alimtegemea Mungu, na amwokoe sasa, kama anamtaka! kwani alisema: Mimi ni Mwana wa Mungu.[#Sh. 22:9.]

44Vivyo hivyo wakamtukana hata wale wanyang'anyi waliowambwa misalabani pamoja naye.

Kufa.

45Tangu saa sita pakawa na giza katika nchi yote mpaka saa tisa.

46Ilipokuwa kama saa tisa, Yesu akapaza sauti sana akisema: Eli, Eli, lama sabaktani? Ni kwamba: Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?[#Sh. 22:2.]

47Wengine wao waliosimama hapo walipoyasikia wakasema: Huyu anamwita Elia.

48Papo hapo mmoja wao akapiga mbio, akachukua mwani, akauchovya sikini na kuutia katika utete, akamnywesha.[#Sh. 69:22.]

49Wengine wakasema: Acha, tuone, kama Elia anakuja kumwokoa!

50Kisha Yesu akapaza tena sauti sana, akakata roho.

51Papo hapo ndipo, pazia la Jumbani mwa Mungu lilipopasuka toka juu mpaka chini, likawa vipande viwili. Nchi ikatetemeka, miamba ikapasuka,[#2 Mose 26:31; Ebr. 10:19-20.]

52makaburi yakafunuka, ikafufuka miili mingi ya watu watakatifu waliolala,

53wakatoka makaburini mwao, yeye alipokwisha kufufuka, wakauingia mji mtakatifu, wakatokea wengi, wawaone.[#Dan. 12:2; Tume. 26:23.]

54Lakini bwana askari nao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoliona lile tetemeko na yale mambo yaliyokuwapo, wakaogopa sana, wakasema: Kweli, huyu alikuwa Mwana wa Mungu!

55Pale palikuwa na wanawake wengi, walisimama mbali wakitazama; ndio waliomfuata Yesu toka Galilea wakimtumikia.[#Luk. 8:1-3.]

56Kati yao walikuwapo Maria Magadalene na Maria, mama yao Yakobo na Yosefu, tena mama yao wana wa Zebedeo.[#Mat. 20:20.]

Kuzikwa.

(57-61: Mar. 15:42-47; Luk. 23:50-55; Yoh. 19:38-42.)

57Ilipokuwa jioni, akaja mtu mwenye mali nyingi wa Arimatia, jina lake Yosefu; naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu.[#2 Mose 34:25.]

58Huyo akaenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu; ndipo, Pilato alipoagiza, apewe.

59Yosefu akauchukua ule mwili, akaufunga kwa sanda nyeupe,

60akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani. Akafingirisha jiwe kubwa mlangoni pa kaburi, akaenda zake.[#Yes. 53:9.]

61Nao akina Maria Magadalene na Maria yule mwingine, walikuwa wamekaa hapa wakilielekea kaburi.

62Kulipokucha, ni siku inayofuata maandalio ya kondoo ya Pasaka, watambikaji wakuu na Mafariseo wakamkusanyikia Pilato,

63wakamwambia: Bwana, tumekumbuka, ya kuwa yule mdanganyifu alisema alipokuwa anaishi bado: Baada ya siku tatu nitafufuka.[#Mat. 12:40; 20:19; 27:40; 2 Kor. 6:8.]

64Kwa hiyo agiza, kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu, wanafunzi wake wasije, wamwibe, wakawaambia watu: Amefufuka katika wafu! madanganyo hayo ya mwisho yakawa mabaya kuliko yale ya kwanza.

65Pilato akawaambia: Chukueni askari wa kulinda! Nendeni, mkalilinde kaburi, kama mnavyojua!

66Nao wakaenda, wakaitia muhuri yao juu ya lile jiwe, wakawaweka askari hapo, walilinde kaburi.[#Dan. 6:17.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania