The chat will start when you send the first message.
1*Wewe Beti-Lehemu wa Efurata,
ijapo uwe mdogo katika miji yenye maelfu ya Yuda,
mwako ndimo, atakamonitokea yeye
atakayekuwa mtawala Waisiraeli;
matokeo yake ni ya siku nyingi za mbele,
kweli ni ya siku za kale na kale.
2Kwa hiyo atawatoa, siku zitimie,
yule atakayezaa atakapokuwa amezaa;
ndipo, wazao wa ndugu zao watakaporudi kwao kwa wana wa
Isiraeli.
3Ndipo, atakapotokea na kusimama, awachunge kwa nguvu za
Bwana,
kwa ukuu wa Jina la Bwana Mungu wake,
nao watakaa, kwani hapo ndipo, atakapokua,
awe mkuu mpaka mapeoni kwa nchi.
4Naye yeye atakuwa utengemano wetu.*
Kama Waasuri wataingia katika nchi yetu,
wakanyage namo majumbani mwetu,
tutaweka wachungaji wetu saba, wawazuie,
pamoja na watu wanane wa kifalme.
5Hao watailisha nchi ya Asuri kwa panga
nayo nchi ya Nimurodi malangoni kwake.
Ndivyo, atakavyotuponya mikononi mwa Waasuri,
kama wanaingia katika nchi yetu na kukanyaga mipakani
kwetu.
6Nao masao ya Isiraeli watakuwa kati ya makabila mengi
kama umande utokao kwa Bwana,
au kama manyunyu yanyeayo majani
yasiyomngojea mtu, yasiyokalii wana wa watu.
7Kweli masao ya Yakobo watakuwa kwa wamizimu kati ya
makabila mengi,
kama simba alivyo katika nyama wa porini,
au kama mwana wa simba alivyo katika makundi ya kondoo,
akiwapita huwakanyaga pamoja na kuwararua, asipatikane
mponya.
8Hivyo mkono wako utakuwa mkuu kwao wakusongao,
nao adui zako watatoweshwa wote.
9Ndivyo, asemavyo Bwana:
Siku hiyo itakuwa, nitakapotowesha kwako farasi wako,
nayo magari yako ya vita nitayapoteza.
10Nayo miji ya nchi yako nitaitowesha,
nayo maboma yako yote nitayabomoa.
11Nazo hirizi nitazitowesha mikononi pako,
nao waaguaji hawatakuwako kwako.
12Tena ndipo, nitakapovitowesha kwako
vinyago vyako na nguzo zako za mawe za kutambikia,
usiangukie tena yaliyo kazi za mikono yako.
13Hata mifano yenu ya mwezi nitaing'oa kwako,
nayo miji yako nitaiangamiza.
14Kwa makali yenye moto nitawalipisha wamizimu wasiosikia.