The chat will start when you send the first message.
1Yamenipata! Kwani yamenijia mambo
yapatikanayo penye mwisho wa machumo ya matunda,
siku za kiangazi zikitimia, au watu wakiokotezaokoteza zabibu:
hakuna kichala cha zabibu za kula
wala kuyu tu, roho yangu inazozitunukia sana.
2Wamchao Mungu wametoweka katika nchi hii,
kwa watu wa huku hakuna mwenye moyo unyokao.
Wote huvizia, wamwage damu za watu,
kila mmoja humtegea mwenziwe tanzi.
3Kama ni kufanya mabaya,
mikono yote miwili iko tayari, yamalizike vema.
Mkuu ayatakayo, mwenye kukata mashauri huyafanya
akipenyezewa mali;
mwenye nguvu akiyasema, roho yake inayoyatamani,
basi, yayo hayo wanayafunganyafunganya.
4Aliye mwema kwao hufanana na mbigili,
anyokaye moyo kwao ni mbaya kuliko boma la migunga.
Siku, wapelelezi wako waliyoisema, ile siku,
utakapopatilizwa, inakuja!
Ndipo, watakapochafukwa na mioyo.
5Usimtegemee mwenzio!
Wala usimjetee rafiki yako umpendaye!
Ilinde midomo ya kinywa chako,
mwanamke alalaye kifuani pako asiyajue yaliyomo!
6Kwani mwana wa kiume anambeza baba yake,
naye mwana wa kike anamwinukia mama yake,
vilevile mkwe na mkwewe,
nao watakaomchukiza mtu ndio waliomo mwake.
7Lakini mimi nitamchungulia Bwana,
nimngojee Mungu wangu atakayeniokoa.
Mungu wangu atanisikia.
8Usinifurahie, uliye adui yangu! Kama ningeanguka, nitainuka tena.
Kama ninakaa gizani, Bwana ni mwanga wangu.
9Makali yake Bwana nitayavumilia, kwani nimemkosea:
mwisho atanigombea magomvi yangu, anikatie shauri lililo sawa,
atanitoa na kuniweka mwangani, nipate kuuona wongofu wake.
10Naye adui yangu ataviona; ndipo, soni itakapomfunika,
yeye aniulizaye sasa: Bwana Mungu wako yuko wapi?
Macho yangu yatamfurahia,
atakapokanyagwa kama taka ya barabarani.
11Siku itakuja, kuta zako zitakapojengwa,
siku hiyo mipaka yako itakuwa mbali.
12Siku hiyo watakuja kwako watokao Asuri na miji ya Misri,
tena kutoka Misri mpaka mto huo mkubwa,
tena kutoka bahari hii mpaka bahari ya pili,
tena kutoka mlima huu mpaka mlima ule.
13Lakini kwanza nchi hii sharti iwe mapori tu
kwa ajili yao waikaao; hayo ndiyo mapato ya matendo yao.
14Walio ukoo wako wachunge kwa fimbo yako,
ndilo kundi lililo fungu lako.
ni wao wakaao peke yao katika mwitu huko Karmeli,
walishe hata Basani na Gileadi kama siku za kale.
15Kama siku zile, mlipotoka katika nchi ya Misri,
nitawaonyesha mambo yatakayowastaajabisha.
16Wamizimu watakapoyaona, watapatwa na soni,
nguvu zao zote zikiwa za bure,
wataweka mikono vinywani,
nayo masikio watayaziba, yasisikie.
17Watalamba mavumbi kama nyoka,
kama wadudu watambaao chini watatoka mafichoni mwao na
kutetemeka,
wamjie Bwana Mungu wetu kwa kutishika,
nawe wewe watakuogopa.
18Je? Yuko Mungu afananaye na wewe,
aondoaye maovu, ayapitaye mapotovu yao
walio masao yao waliokuwa fungu lake?
Hazishiki kale na kale nguvu za makali yake,
kwani hupendezwa na kuwaendea watu kwa upole.
19Nasi atatuhurumia tena, maovu yetu yote
atayapondaponda, yatutoke,
makosa yetu yote atayatupa vilindini mwa bahari.
20Yakobo utamwendea kwa welekevu, naye Aburahamu kwa upole,
kama ulivyowaapia baba zetu tangu siku zile za kale.