Nahumu 2

Nahumu 2

Wokovu wa Yuda.

1Tazameni! Milimani juu iko miguu ya mpiga mbiu

atangazaye utengemano:

Uzile sikukuu zako, Yuda! Vilipe viapo vyako!

Kwani yule mwovu asiyefaa hatapita tena kwako,

amekwisha kung'olewa wote pia.

2Amepanda mwenye kutawanya, akujie;

kwa hiyo lilinde boma na kuiangalia njia!

Jifunge sana viuno vyako! Nazo nguvu, ulizo nazo, zikaze

kabisa!

3Kwani Bwana anaurudisha utukufu wake Yakobo

nao utukufu wake Isiraeli,

kwani wapokonyi waliyapokonya yaliyokuwako,

nayo matawi ya mizabibu yao waliyaharibu.

Jinsi Niniwe utakavyobomolewa.

4Ngao za mafundi wake wa vita ni nyekundu,

watu wake wenye nguvu wanavaa nguo nyekundu za kifalme,

siku, yanapopangwa, vyuma vya magari yake humetuka kama moto,

nayo mikuki yake hutikiswatikiswa.

5Barabarani magari yanapiga vishindo vya nguvu,

namo uwanjani yanashindana mbio;

mkiyatazama huwa kama mienge ya moto,

tena hurukaruka upesi kama umeme.

6Basi, anawakumbuka wakuu wake,

lakini wanakuja na kujikwaakwaa;

walipokwenda mbiombio kuufikia ukuta wa boma la nje,

kikingio cha kuubomolea kilikuwa kimekwisha kuwekwa.

7Malango ya upande wa mtoni yalipofunguliwa,

waliomo jumbani mwa mfalme wakayeyuka.

8Mke wa mfalme hana budi kuvuliwa nguo na kupelekwa mbali,

vijakazi wake wakilia kama sauti za hua na kujipigapiga vifua.

9Niniwe ulikuwa kama ziwa la maji tangu kale,

lakini sasa hao wengi wanajikimbilia tu;

wanaambiwa: Simameni! Simameni! Lakini hakuna anayegeuka.

10Tekeni fedha! Tekeni dhahabu! Kwani malimbiko hayana

mwisho;

viko vyombo vya kila namna vipendezavyo.

11Lakini kwa kuwa mioyo imeyeyuka, uko uchi na utupu na

ukiwa,

nayo magoti yanagotanagotana,

viuno vyote vinatetemeka, nazo nyuso zao wote zimewapoa.

12Makao ya simba yako wapi?

Malisho ya wana wa simba yako wapi nayo?

Ndipo wapi, walipotembea simba mume na mke na watoto

pasipo kuona awastushaye?

13Ndipo wapi, simba waliporarua nyama, mpaka watoto wao

washibe?

Ndipo wapi, walipoona nyama wa kuwapatia nao wake zao?

Ndipo wapi, walipojaza mapango yao nyama, waliowararua?

Yako wapi mashimo yao nyama wao hao, waliowararua?

14Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi:

Utaniona, nikikujia, niyachome magari yako, yawe moshi,

nao wana wako wa simba upanga utawala;

nitakukomesha, usirarue tena nyama katika nchi,

wala sauti za wajumbe wako zisisikilike tena.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania