4 Mose 24

4 Mose 24

Bileamu anawabariki Waisiraeli mara ya tatu.

1Bileamu alipoona, ya kuwa imekuwa vema machoni pa Bwana kuwabariki Waisiraeli, hakwenda tena kama mara ya kwanza na mara ya pili kutafuta mambo ya kuagulia, ila akauelekeza uso wake jangwani.

2Bileamu alipoyainua huko macho yake akawaona Waisiraeli, walivyokaa shina kwa shina; ndipo, roho ya Mungu ilipomjia,

3akaanza kusema maneno yake kwamba:

Hivi ndivyo, asemavyo Bileamu, mwana wa Peori,

hivi ndivyo, asemavyo mtu aliyefumbwa macho.

4Hivi ndivyo, asemavyo aliyesikia maneno ya Mungu,

aliyeona maono yake aliye Mwenyezi,

aliyefumbuliwa macho alipomwangukia:

5Mahema yako, Yakobo, ni mema peke yao,

nayo makao yako, wewe Isiraeli.

6Huwa kama mabonde yanayoendelea mbali,

huwa kama mashamba yaliyoko kando ya mto,

huwa kama misagawi, Bwana aliyoipanda,

huwa kama miangati iliyoko kwenye maji!

7Ndoo zake huchuruzisha maji mengi,

nazo mbegu zake hunyweshwa maji mengi.

Mfalme wake ni mkuu kuliko Agagi,

nao ufalme wake utatukuka sana.

8Mungu ndiye aliyemtoa Misri,

naye anazo nguvu kama za nyati,

hula wamizimu wanaomsonga,

nayo mifupa yao huipondaponda,

akiwaangusha chini kwa mishale yake.

9Kama simba mume au simba mke anavyootea,

ndivyo, anavyolala;

yuko nani atakayemwinua?

Mwenye kukubariki amekwisha kubarikiwa naye,

mwenye kukuapiza amekwisha kuapizwa naye.

10Ndipo, makali ya Balaka yalipomwakia Bileamu, akayapiga makofi yake, kisha Balaka akamwambia Bileamu: Nimekuita, uwaapize adui zangu, kumbe umewabariki sasa mara ya tatu!

11Sasa jiendee upesi mahali pako! Nalisema moyoni: Nitakuheshimu sana, lakini tazama, Bwana amekunyima hizo heshima.

12Naye Bileamu akamwambia Balaka: Je? Wajumbe wako, uliowatuma kwangu, sikuwaambia kwamba:

13Ijapo Balaka anipe nyumba yake ijaayo fedha na dhahabu, sitaweza kukipita kinywa cha Bwana, nifanye jambo baya au jema, kama moyo wangu unavyotaka; ila Bwana atakaloniambia, ndilo hilo, nitakalolisema?[#4 Mose 22:18.]

14Sasa tazama, ninakwenda zangu kwa watu wa kwetu; lakini kwanza nitakuonyesha, watu wa ukoo huu watakavyowafanyizia watu wako siku zitakazokuja baadaye.

Nyota ya Yakobo.

15Kisha akaanza kusema maneno yake kwamba:

Hivi ndivyo, asemavyo Bileamu, mwana wa Peori,

hivi ndivyo, asemavyo mtu aliyefumbwa macho.

16Hivi ndivyo, asemavyo aliyesikia maneno ya Mungu,

ajuaye kumtambua Alioko huko juu,

aliyeona maono yake aliye Mwenyezi,

aliyefumbuliwa macho alipomwangukia:

17Ninamtazamia, lakini hayuko sasa,

ninamchungulia, lakini hayuko karibu.

Nyota itatokea kwake Yakobo,

nayo bakora ya kifalme itainuka kwake Isiraeli,

izivunje pande zote mbili zao Wamoabu

na kuwamaliza wana wao wote wapigao vita.

18Nayo nchi ya Edomu itakuwa yake yeye,

nayo ya Seiri itakuwa yake yeye,

nayo ndiyo iliyokuwa yao adui zake!

Kweli Isiraeli atatenda nguvu.

19Mwenye kutawala atatoka mwake Yakobo,

nao waliokimbia na kutoka mijini atawaangamiza.

Kuangamia kwao Waamaleki na Wakeni na wengine.

20Alipowaona Waamaleki akaanza kusema maneno yake kwamba:

Walio wa kwanza wa wamizimu ndio Waamaleki,

lakini mwisho wao utakuwa kuangamia tu.

21Alipowaona Wakeni akaanza kusema maneno yake kwamba:

Kao lako limeshupaa,

tundu lako umelijenga mwambani,

22lakini havikuponyi, Kaini, utateketea,

bado kidogo Waasuri watakuteka.

23Kisha akasema maneno yake mengine kwamba:

Hoi! Yuko nani atakayepona, yatakapowapata?

Nayo yatawapata hapo, Mungu atakapoyatimiza.

24Merikebu zitatoka kwao Wakiti, ziwanyenyekeze Waasuri,

ziwanyenyekeze hata Waeberi, mpaka waangamie nao.

25Kisha Bileamu akaondoka kwenda kurudi kwao, naye Balaka akaenda zake.[#4 Mose 31:8,16.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania