Wafilipi 1

Wafilipi 1

Anwani.

1Sisi Paulo na Timoteo tulio watumwa wake Kristo Yesu tunawaandikia ninyi watakatifu nyote mlio naye Kristo Yesu, mkaao huko Filipi, pamoja nanyi watumishi:[#1 Kor. 1:2; 1 Tim. 3:1-3,8.]

2Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo![#Rom. 1:7.]

Paulo huwaombea.

3*Namshukuru Mungu wangu, kila ninapowakumbuka,

4kwani kila mara nikiwaombea ninyi nyote ninaomba na kufurahi.

5Kwani mwashikamana na Utume mwema tangu siku ile ya kwanza mpaka sasa hivi.

6Kwa hiyo moyo umenitulia, nikijua: Yeye aliyeanza mwenu kazi njema ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.[#Fil. 2:13; 1 Kor. 1:6-8.]

7Ndivyo, inavyonipasa kuwawazia ninyi nyote, kwa sababu ninyi hamtoki moyoni mwangu, ikiwa nafungwa na ikiwa naukania Utume mwema na kuutangaza kwa nguvu; hapo po pote ninyi m wenzangu waliogawiwa kipaji kilekile.

8Kwani Mungu huona, ninavyowatunukia ninyi nyote kwa hivyo, tulivyo moyoni mwake Yesu Kristo.

9Neno, niwaombealo, ni hili: upendo wenu uendelee kukua na kuongezeka, kama mlivyoendelea kutambua na kujua maana yote,

10mpate kuyapambanua yasiyopatana, mtokee siku ya Kristo wenye ung'avu wa mioyo wasiokwaza wengine,[#Rom. 12:2; 1 Tes. 5:23.]

11mkawa wenye mapato yote ya wongofu, anayotupatia Yesu Kristo, Mungu atukuzwe na kusifiwa.*[#Ef. 5:9.]

Kumvumisha Kristo.

12*Basi, ndugu, nataka, mtambue, ya kuwa mambo yangu yaliyonipata yamegeuka kuwa ya kuuendesha Utume mwema.[#2 Tim. 2:9.]

13Maana hapa bomani pote nako kwao wengine minyororo yangu imejulikana, ya kwamba nimefungwa kwa ajili yake Kristo.[#Fil. 4:22.]

14Tena minyororo yangu imeshikiza ndugu wengi walio wake Bwana, wakajipa mioyo nao ya kulisema Neno la Mungu pasipo woga.

15Kweli wako wamtangazao Kristo kwa ajili ya wivu na uchokozi, lakini tena wako wanaomtangaza kwa kupendezwa kweli.

16Hao ndio wanaonipenda, kwani wamejua, ya kuwa nimefungwa, niukanie Utume mwema.

17Lakini wale humtangaza Kristo, kwamba wanichokoze, lakini mioyo haiwang'ai, maana hutaka kuyaongeza maumivu yangu, niliyo nayo humu kifungoni.[#Fil. 1:7.]

18Basi, haidhuru; inafaa, Kristo atangazwe tu kwa njia zozote, ikiwa za uwongo, au ikiwa za kweli; kwa hiyo nafurahi. Hata siku zitakazokuja nitafurahi.[#Fil. 2:17-18.]

19Kwani najua: hili nalo timizo lake ni wokovu wangu, maana ninyi huniombea, nao Roho wake Kristo hunisaidia.[#Iy. 13:16.]

20Hiki nacho ni kingojeo changu, nitumikiacho, kitimie: hakuna neno lo lote, ambalo nitatiwa soni nalo, ila kama vilivyokuwa kale, ndivyo, vitakavyokuwa hata sasa: Kristo atatukuzwa waziwazi po pote mwilini mwangu, ikiwa kwa njia ya kuishi au ya kufa.[#1 Petr. 4:16.]

Kufa ni kupata.

21Kwani kwangu mimi kuishi ni Kristo, hata kufa ni kupata.*[#Gal. 2:20.]

22Lakini kuishi mwilini kunanifaa, niyaone machumo ya kazi yangu; kwa hiyo sikutambui, nitakakokuchagua.[#Rom. 1:13.]

23Kwani nashindana na haya mambo mawili: ninatunukia kuaga nchini, nipate kuwa pamoja na Kristo; nako ni kuzuri kuliko yote.[#1 Fal. 19:4; 2 Kor. 5:8.]

24Lakini kuishi humu mwilini kunafaa zaidi kwa ajili yenu ninyi.

25Kwa hiyo moyo umenitulia, nikijua, ya kuwa nitakaa nchini, nako kwenu nitakaa nanyi nyote, mwendelee kumtegemea Mungu na kufurahiwa ndiko,[#Fil. 2:24.]

26majivuno yenu ya kuwa wake Kristo Yesu yaongezeke kwa ajili yangu, mkiniona, nikifika tena kwenu.

Simameni kwa nguvu ya Kiroho!

27*Tena neno moja: sharti mwongozane, kama iwapasavyo wenye Utume mwema wa Kristo! Maana ikiwa nafika kwenu, sharti niwaone, au ikiwa niko huku mbali, sharti niwasikie kwamba: Mko mmesimama kwa nguvu ya kutenda roho moja, nayo mioyo ni mmoja tu wa kuja vitani pamoja, mkugombee kuutegemea Utume mwema.[#Tume. 4:32; Kol. 1:10; 1 Tes. 2:12.]

28Hivyo halitapatikana neno lo lote, wapigani wenu wanaloweza kuwatisha; napo ndipo, wanapojulika kuwa wenye upotevu, nanyi kuwa wenye wokovu, naye mwenye kuwajulisha kuwa hivyo ni Mungu.

29Kwani ninyi kwa hivyo, mnavyomtumikia Kristo, siko kumtegemea tu mlikopewa, ila mmepewa hata kuteseka kwa ajili yake yeye,[#Tume. 5:41-42.]

30mkapatwa na kondo ileile, mliyoiona kwangu kale, tena mnayoisikia, ya kuwa hata sasa ninayo.[#Tume. 16:22.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania