The chat will start when you send the first message.
1Mwana mwerevu wa kweli hutaka kuonywa na baba,
lakini mfyozaji hasikii akikemewa.
2Kila mtu hula mema, kinywa chake kilichoyazaa,
lakini roho zao wavunja maagano hula makorofi.
3Akilindaye kinywa chake huilinda roho yake,
lakini aifunuaye midomo yake hujiangamiza.
4Roho yake mvivu hutamani vingi pasipo kupata kitu,
lakini roho zao wajihimizao kufanya kazi hushibishwa sana.
5Mwongofu huchukia neno la uwongo,
lakini asiyemcha Mungu hufanya yachukizayo nayo yatwezayo.
6Mwongofu humlinda ashikaye njia isiyokosesha,
lakini kuacha kumcha Mungu humwangusha mkosaji.
7Wako wanaojitendekeza kuwa wenye mali, lakini hawana kitu,
tena wako wanaojitendekeza kuwa maskini, lakini wana mali nyingi.
8Makombozi ya roho ya mtu ni mali zake nyingi,
lakini maskini hasikii makemeo yo yote.
9Mwanga wa waongofu huangaza kwa furaha,
lakini taa zao wasiomcha Mungu huzimika.
10Hakuna mengine, majivuno yanayoyaleta, ila ugomvi tu,
lakini kwao wanaotaka mashauri mema uko werevu wa kweli.
11Mali zilizopatikana bure tu hupunguka upesi,
lakini azikusanyaye kwa kazi za mkono wake huziongeza.
12Uliyoyangojea yakikawia sana huuguza moyo,
lakini kuyapata, uliyoyatamani, ni mtu wa uzima.
13Alibezaye Neno hupatiwa mwangamizo nalo,
lakini aogopaye kulikosea agizo hupata malipo.
14Maonyo ya mwerevu wa kweli ni kisima cha uzima,
maana ni kuepuka penye matanzi ya kifo.
15Ujuzi mwema huleta mapendeleo,
lakini njia zao walioacha kumcha Mungu hushupaza.
16Mwerevu hufanya yote kwa ujuzi,
lakini mpumbavu hujikuza kwa mapumbavu yake.
17Mjumbe asiyemcha Mungu huanguka kwa ubaya,
lakini mtume mwelekevu huponya.
18Ukiwa na matusi humpata akataaye kuonyeka,
lakini aangaliaye akikanywa hupata heshima.
19Kuyapata, mtu aliyoyatamani, huipendeza roho yake,
lakini yanayowatapisha wapumbavu ni kuacha mabaya.
20Atembeaye na werevu wa kweli huerevuka kweli,
lakini rafiki ya wapumbavu hupata mabaya.
21Mabaya huwakimbiza wakosaji,
lakini waongofu Mungu huwalipa mema.
22Mwema huwaachia wanawe na wana wao mali zake,
lakini mapato ya mkosaji hulimbikiwa mwongofu.
23Shamba, waliloanza kulilima, huwapatia wakiwa vilaji vingi,
lakini wengine hupokonywa kwa kufanya yasiyo sawa.
24Amnyimaye mwanawe fimbo humchukia,
lakini ampendaye hakawii kabisa kumchapa.
25Mwongofu hupata kula, hata aishibishe roho yake,
lakini matumbo yao wasiomcha Mungu huona njaa.