The chat will start when you send the first message.
1Jibu lenye upole hutuliza makali,
lakini neno liumizalo hukasirisha sana.
2Ndimi zao walio werevu wa kweli husema ujuzi mwema,
lakini vinywa vya wapumbavu hububujika ujinga.
3Macho ya Bwana huwa po pote,
huwatazama wabaya na wema.
4Upole wa ulimi ni mti wa uzima,
lakini udanganyifu uliomo huvunja moyo.
5Mjinga hukataa kuonywa na baba yake,
lakini aangaliaye akikanywa huerevuka.
6Nyumbani mwa mwongofu mna limbiko kubwa,
lakini mapato yake asiyemcha Mungu utawanyika.
7Midomo yao walio werevu wa kweli humwaga ujuzi,
lakini mioyo ya wapumbavu haifanyi hivyo.
8Vipaji vya tambiko vyao wasiomcha humtapisha Bwana,
lakini maombo yao wanyokao humpendeza.
9Njia yake asiyemcha humtapisha Bwana,
lakini humpenda aukimbiliaye wongofu.
10Ayaachaye mapito yampasayo hupata mapigo mabaya,
achukiaye kukanywa hufa.
11Kuzimu nako, wafu wanakopotelea, kuko mbele ya Bwana;
tena je? Mioyo ya wana wa Adamu haitakuwa wazi zaidi?
12Mfyozaji hapendi, mtu akimkanya,
wala haendi kwao werevu wa kweli.
13Moyo wenye furaha huuchangamsha uso,
lakini moyo ukisikitika, roho hupondeka.
14Moyo wa mtambuzi hutafuta ujuzi,
lakini vinywa vya wapumbavu hujilisha ujinga.
15Siku zote za mtu atesekaye ni mbaya,
lakini moyo mwema hufanana na karamu ya siku zote.
16Machache yake amwogopaye Bwana ni mema
kuliko malimbiko mengi yamhangaishayo mwenyewe.
17Kula maboga na mtu wa kupendana naye ni kwema
kuliko ng'ombe ya manono, ukila na mtu wa kuchikzwa naye.
18Mtu mkali huzusha magomvi,
lakini mvumilivu hutuliza mateto.
19Njia ya mvivu hufanana na boma lenye miiba mikali,
lakini mapito yao wanyokao ni njia zilizotengenezwa.
20Mwana mwerevu wa kweli humfurahisha baba yake,
lakini mtu mpumbavu humbeza mama yake.
21Ujinga humfurahisha aliyepotelewa na akili,
lakini mwenye utambuzi huunyosha mwenendo wake.
22Nayo mawazo mema hayafanikiwi pasipo kupiga mashauri,
lakini wenye kuongoza wanapokuwa wengi, huendelea.
23Mtu hufurahia jibu jema la kinywa chake,
nalo neno lisemwalo panapopasa ni zuri zaidi.
24Njia yake aerevukaye ya kwenda uzimani huelekea juu,
kusudi ajiepushe kuzimuni huko chini.
25Nyumba zao wenye majivuno Bwana huzibomoa,
lakini mipaka ya wajane huishupaza.
26Mawazo ya wabaya humtapisha Bwana,
lakini maneno yampendezayo ndiyo yatakatayo.
27Atakaye mapato ya upotovu huwavuruga waliomo nyumbani mwake,
lakini achukiaye mapenyezo hujipatia uzima.
28Moyo wa mwongofu huyawaza, atakayoyajibu,
lakini vinywa vyao wasiomcha Mungu hububujika mabaya.
29Bwana huwakalia mbali wasiomcha,
lakini malalamiko ya waongofu huyasikia.
30Macho yakiangaza, moyo hufurahi,
habari njema huishupaza mifupa.
31Sikio linalosikia maonyo yanayompatia mtu uzima
hupenda kukaa kwao werevu wa kweli.
32Akataaye kuonywa huitupa roho yake,
lakini asikiaye akikanywa hujipatia akili zaidi.
33Amchaye Bwana huonyeka, ajipatie werevu wa kweli,
nayo macheo hutanguliwa na unyenyekevu.