The chat will start when you send the first message.
1Mkiwa aishikaye njia yake pasipo kukosa na mwema
kuliko mpotovu wa midomo aliye mpumbavu.
2Roho ikosayo ujuzi siyo njema,
naye mwenye haraka ya kupiga mbio kwa miguu hukosa.
3Ujinga wa mtu huipotoa njia yake mwenyewe,
lakini moyo wake humkasirikia Bwana.
4Kuwa na mali huongeza rafiki, wawe wengi,
lakini mnyonge huachwa na rafiki zake.
5Shahidi ya uwongo hana budi kupatilizwa,
asemaye na kuongopa haponi.
6Watu wengi hulalamika usoni pa wakuu,
watu wote huwa rafiki zake awapaye matunzo.
7Maskini huchukiwa na ndugu zake wote,
wanaozidi ni rafiki zake, hutengana naye humwacha mbali;
akiwafuata, aseme nao, sio rafiki zake tena.
8Apataye akili hujipenda mwenyewe
utambuzi huona mema.
9Shahidi ya uwongo hana budi kupatilizwa,
asemaye na kuongopa huangamia.
10Mpumbavu hapaswi na kutumia yenye urembo,
sembuse mtumishi, hapaswi na kuwatawala wafalme.
11Akili za mtu humvumilisha,
utukufu wake umo katika kuwaondolea wengine mapotovu yao.
12Ukali wa mfalme ni kama ngurumo ya simba,
lakini upole wake ni kama umande unyweshao majani.
13Mwana mpumbavu humpatia baba yake mabaya,
lakini magomvi ya mwanamke huwa mchirizi usiokoma kuchuruzika.
14Nyumba na mali watu huachiwa na baba zao,
lakini mwanamke mwenye akili hutoka kwa Bwana.
15Uvivu humpatia mtu usingizi mwingi,
nayo roho ya mtu afanyaye kazi na kulegeza mikono huona njaa.
16Aliangaliaye agizo la Mungu hujiangalia mwenyewe,
lakini azibezaye njia zake hufa.
17Ahurumiaye mnyonge humkopesha Bwana,
ndiye atakayemlipa tendo lake.
18Mpige mwanao unapoweza kumngojea, aonyeke,
lakini usiwaze moyoni mwako kumwua!
19Mwenye makali mengi hutozwa malipo,
kwani ukimwacha tu, unayazidisha makali yake.
20Yasikie mashauri, unayopewa, uonyeke,
kusudi uerevuke kweli katika siku zako zijazo.
21Moyoni mwa mtu yamo mawazo mengi,
lakini shauri la Bwana ndilo litakalokuwa.
22Ugawiaji wa mtu hutokea katika mapenzi yake,
naye maskini ni mwema kuliko mwenye uwongo.
23Kumcha Bwana hupeleka uzimani,
hivyo mtu hulala na kushiba pasipo kupatwa na mabaya.
24Mvivu akiutia mkono wake katika bakuli
haurudishi kinywani mwake.
25Ukimpiga mfyozaji, ndipo, mjinga atakapoerevuka,
ukimwonya mtambuzi, ndipo, atakapotambua ujuzi.
26Amtesaye baba yake na kumfukuza mama yake
ni mwana atiaye soni kwa kutweza.
27Mwanangu, acha kuyasikiliza mafunzo,
ukitaka kuyakosea tena maneno ya ujuzi!
28Shahidi asiyefaa kitu hufyoza mashauri yaliyo sawa,
navyo vinywa vyao wasiomcha Mungu hujilisha mapotovu.
29Mashauri ya wafyozaji yamekwisha kutengenezwa,
nayo mapigo ya migongoni kwa wapumbavu yako tayari.