The chat will start when you send the first message.
1Ukikaa chakulani kwa mtawalaji
sharti umtambue yeye aliopo usoni pako.
2Jibandikie kisu kooni pako
wewe ukiwa mwenye tamaa ya kula sana!
3Usivitamani vilaji vya urembo vya mwingine!
Kwani ni vyakula vya udanganyifu.
4Usijisumbue kupata mali nyingi,
ukaacha kuutumia utambuzi wako kwa ajili ya hizo mali!
5Au sivyo? Ukizitupia macho yako, basi, haziko tena,
nazo hujitengenezea mabawa kama ya tai ya kurukia kwenda mbinguni.
6Usile chakula chake mwenye jicho baya,
wala usivitamani vyakula vyake vya urembo!
7Kwani yeye ni kama mtu ahesabuye yote rohoni mwake;
hukuambia: Haya! Ule, unywe! lakini moyo wake hauko kwako.
8Kwa hiyo utakitapika kitonge, ulichokila,
nayo maneno yako yapendezayo yatakuwa umeyasema bure tu.
9Usiseme masikioni pa mpumbavu!
Kwani atayabeza maneno yako, uliyoyasema kwa akili.
10Usisogeze mawe ya mipaka ya kale,
wala usiingie mashambani kwao waliofiwa na wazazi wao!
11Kwani mkombozi wao ni mwenye nguvu,
yeye huwagombea, wakigombezwa na wewe.
12Ushurutishe moyo wako, uonyeke,
nayo maskio yako, yasikie maneno ya ujuzi!
13Usimnyime mtoto mapigo!
ukimpiga kwa fimbo, hatakufa.
14Wewe ukimpiga kwa fimbo
utaiokoa roho yake kuzimuni.
15Mwanangu, moyo wako ukierevuka kweli,
moyo wangu mimi utafurahi nao.
16Maini yangu yatashangilia,
midomo yako ikisema yanyokayo.
17Moyo wako usione wivu kwa ajili ya wakosaji,
ila kaa tu na kumcha Bwana siku zote!
18Kwani yote yako na mwisho wao,
lakini kingojeo chako hakitaangamia.
19Wewe mwanangu, sikiliza, uereuke kweli,
kauongoze moyo wako katika njia hii!
20Usiwe mwenzao wanywaji wa mvinyo,
wala wao walao nyama kwa ulafi!
21Kwani mnywaji na mlafi watachukuliwa mali zao,
kwani usingizi mwingi huvika watu vitambaa vichakavu.
22Msikie baba yako aliyekuzaa!
Usimbeze mama yako, akiwa mzee!
23Inunue kweli! Lakini usiiuze tena!
Hata werevu wa kweli na usikivu na utambuzi!
24Babake mwana mwongofu hupiga shangwe nyingi,
aliyezaa mwana mwerevu wa kweli humfurahia.
25Naye baba yako na mama yako na wakufurahie hivyo,
yeye aliyekuzaa na apige shangwe!
26Mwanangu, nipe moyo wako,
njia zangu ziyapendeze macho yako!
27Kwani mwanamke mgoni ni shimo refu sana,
naye aliye mwanamke wa mwingine ni kisima chembamba.
28Naye huotea kama mpokonyi,
awaongoze kuwa wengi, wao wavunjao maagano kwa watu.
29Ni nani aliaye? Ni nani apigaye kite?
Ni nani apatwaye na magomvi? Ni nani aombolezaye?
Ni nani ajiumizaye bure? Ni nani aliye na macho mekundu?
30Ndio wao wanaokunywa mvinyo usiku kucha,
ndio wao watembeao kutafuta vileo vikali.
31Usiitazame mvinyo, jinsi wekundu wake unavyopendeza,
jinsi inavyometuka katika bilauri, inavyozidi utamu, ukiinywa!
32Mwisho huuma kama nyoka,
huchoma kama pili;
33ndipo, macho yako yatakapoona mambo mageni,
nao moyo wako utakaposema mapotovu;
34nawe utakuwa kama mtu alalaye chini baharini,
au kama mtu alalaye pembeni juu ya mlingoti;
35utasema: Walinipiga, lakini sikuumia,
walinichapa, lakini sikusikia.
Nitaamka lini? Ndipo, nitakapokwenda kuitafuta tena.