The chat will start when you send the first message.
2Utukufu wake Mungu ni kufunika jambo,
utukufu wao wafalme ni kufunua jambo.
3Kama mbingu zilivyoko juu, kama nchi ilivyoko nako kuzimuni,
ndivyo, mioyo ya wafalme inavyotushinda, isichunguzike.
4Mtu akiondoa mitapo katika fedha
hutengeneza chombo kinachomfaa mwenye kuyeyusha.
5Mtu akimwondoa asiyemcha Mungu machoni pake mfalme,
kiti chake cha kifalme hupata nguvu kwa wongofu.
6Usijitukuze mbele ya mfalme,
wala usisimame mahali, wakuu walipo!
7Kwani kuambiwa: Sogea hapa mbele! ni kwema
kuliko kunyenyekezwa penye macho ya mkuu yaliyokutazama.
8Usitokee upesi kugombana na mtu!
Kwani mwisho utafanya nini, mwenzio akikutia soni?
9Kama yako ya kupigania na mwenzio, yapiganie!
Lakini usifunue shauri la njama ya mwingine,
10mtu aisikiaye asikuapize,
uchongezi wako ukakurudia.
11Kama machunguwa yaliyomo katika vyano vya fedha yalivyo,
ndivyo, lilivyo neno linalosemwa papasapo.
12Kama pete ya dhahabu na mkufu wa dhahabu tupu wa shingoni
ni maonyo ya mwerevu wa kweli yakiingia katika sikio lisikialo.
13Kama baridi ya theluji inavyofurahisha siku ya mavuno,
ndivyo, mjumbe mwelekevu anavyowafurahisha waliomtuma
kwani huzituliza roho za mabwana zake.
14Mawingu na upepo pasipo mvua
ni mtu ajivuniaye vipaji vya uwongo, asivyovitoa.
15Kwa uvumilivu hushindwa naye mwamuzi
nao ulimi mwororo huvunja mifupa.
16Kama umeona asali, ule na kuipima,
usije kuitapika, kama ulijishibisha sana!
17Kawilia kuingia nyumbani mwa mwenzio,
usije kumchokesha, akakuchukia.
18Nyundo ipondayo na upanga na mshale mkali
ni mtu amshuhudiaye mwenziwe ushahidi wa uwongo.
19Jino livunjikalo na mguu utegukao
ni kumwegemea mtu avunjaye maagano siku ya masongano.
20Avuaye nguo siku ya baridi, au siki itiwayo katika magadi
ni mtu amwimbiaye mwenziwe nyimbo, moyo wake ukiwa mzito.
21Mchukivu wako akiwa ana njaa, mpe chakula!
Akiwa ana kiu, mpe cha kunywa!
22Kwani hivyo utampalia makaa ya moto kichwani pake,
naye Bwana atakulipa hayo.
23Upepo wa kaskazini huleta mvua,
nao ulimi usingiziao hukasirisha nyuso.
24Kukaa darini pembeni ni kwema
kuliko kukaa na mwanamke mgomvi katika nyumba moja.
25Kama maji ya baridi, roho iyatweteayo,
ni habari njema itokayo katika nchi ya mbali.
26Kama chemchemi ivurugikavyo au kama kisima kiharibikacho
ni mwongofu atukutikaye machoni pake asiyemcha Mungu.
27Kula asali nyingi hakufai,
lakini kuyachunguza mambo mazito huleta macheo.
28Kama mji uliobomolewa kwa kukosa ukuta wa boma ulivyo,
ndivyo, alivyo mtu asiyejua kuiangalia roho yake.