Mifano 4

Mifano 4

Vijana sharti wafuate mafundisho yenye ujuzi.

1Wanangu, sikieni, baba akiwakanya!

Yategeni masikio, myajue yenye utambuzi!

2Kwani ninawapa ninyi mafundisho mema:

maonyo yangu msiyaache!

3Kwani nami nilipokuwa mwana wa baba yangu,

mtoto mnyonge aliyependwa sana na mama kwa kuwa wa pekee,

4baba alinifundisha, akaniambia:

Moyo wako sharti uyashike sana maneno yangu,

uyaangalie maagizo yangu! Ndipo, utakapopata uzima.

5Jipatie werevu wa kweli! Jipatie nao utambuzi!

Usiusahau! wala usiyageukie mgongo maneno ya kinywa changu!

6Usiuache! Ndipo, nao utakapokuangalia;

uupende! Ndipo, nao utakapokulinda.

7Mwanzo wa werevu wa kweli ndio huu: jipatie werevu wa kweli!

Jipatie utambuzi kwa kuyatoa mapato yako yote!

8Uutukuze! Ndipo, nao utakapokutukuza,

utakupatia macheo, ukiukumbatia.

9Kichwa chako utakivika kilemba kipendezachao,

utakugawia taji yenye utukufu.

10Sikia, mwanangu, uyapokee maneno yangu!

Ndipo, miaka yako ya kukaa uzimani itakapokuwa mingi.

11Nimekuongoza katika njia ya werevu wa kweli,

nikakuendesha katika mapito yanyokayo;

12ukiyashika, nyayo zako hazitasongeka,

hata utakapopiga mbio hutajikwaa.

13Yashike kwa nguvu mafundisho yakuonyayo, usiyaache kabisa!

Yalinde, kwani ndiyo yaliyo uzima wako.

14Mapito yao wasiomcha Mungu usiyakanyage!

Wala usitembee katika njia ya wabaya!

15Ondoka hapo, ilipo, usiifuate!

Epuka hapo, ilipo, upapite!

16Kwani hawawezi kulala wasipokwisha kufanya mabaya;

usingizi huwapotelea, wasipokwisha kukwaza mtu.

17Kwani vilaji, wanavyovila, ni vya kumbeza Mungu,

nayo mvinyo, wanayoinywa, ni yenye makorofi.

18Lakini mapito ya waongofu huwa kama mwanga wa kucha,

huendelea ukiangaza, hata mchana wenyewe utimie.

19Njia yao wasiomcha Mungu huwa kama giza lenyewe,

wasijue, kama ni kitu gani kiwakwazacho.

20Mwanangu, yasikilize maneno yangu

Yategee sikio, ninayokuambia!

21Usiyaache, yatoweke machoni pako!

Yaangalie moyoni mwako ndani!

22Kwani hayo ndio uzima wao wayapatao,

tena ni dawa ya miili yao wote.

23Kuliko yote, unayoyaanglia, ulinde moyo wako!

Kwani humo ndimo, uzima unamotoka.

24Ondoa kwako upotovu wa kinywa,

ukiiepusha midomo yako kwenye mambo yasiyonyoka!

25Yaelekeze macho yao kuyatazama yaliyoko mbele,

kope zako nazo ziyaelekee sawasawa yaliyoko mbele yako!

26Miguu yako ishikishe mapito yaliyo malinganifu,

njia zako zote ziwe zimeshupaa!

27Usigeukie kuumeni wala kushotoni,

upate kuiondoa miguu yako penye mabaya!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania