The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, yaangalie maneno yangu,
uyashike sana maagizo yangu moyoni mwako!
2Yaangalie maagizo yangu! Ndipo, utakapopata uzima;
yaangalie maonyo yangu, kama unavyoangalia mboni ya jicho lako!
3Yafunge vidoleni pako,
tena yaandike katika kibao cha moyo wako!
4Uuambie werevu wa kweli: Wewe ndiwe umbu langu,
utambuzi nao uuite: Mpendwa wa kujuana naye!
5Ukuanglie, usitazame mwanamke mgeni,
wala usiyasikilize maneno yatelezayo ya mke wa mwingine!
6Kwani dirishani nyumbani mwangu
siku moja nilipochungulia penye vyuma vyake,
7niliwatazama wajinga, nikaona kijana mmoja aliyepotelewa na akili,
nikamtambua katikati yao wasioyajua bado mambo hayo.
8Alitembea barabarani hapo pembeni, yule alipokaa,
akaishika njia ya kutembea penye nyumba yake;
9ikawa jioni, jua lilipokwisha kuchwa,
hata ikawa usiku wa manane penye giza.
10Mara mwanamke anakuja kukutana naye,
alivaa nguo kama mgoni, nao moyo wake ulikuwa mdanganyifu.
11Anapiga kelele pasipo kujizuia,
miguu yake haipendi kukaa nyumbani mwake;
12mara moja yuko barabarani, mara nyingine yuko uwanjani,
huvizia po pote penye njia panda.
13Basi, huyu akamshika, akamnonea,
akaushupaza uso wake akamwambia:
14Sina budi kutoa kipaji cha tambiko cha shukrani,
leo hivi ninavilipa viapo vyangu.
15Kwa hiyo nimetoka nyumbani, nikutane na wewe,
nikauchungulia uso wako, mpaka nikakuona.
16Kitanda changu nimekitandika mazulia
na mablanketi mororo yenye rangi ya Kimisri.
17Pangu pa kulalia nimepamwagia manukato,
manemane na liwa na dalasini.
18Haya! Njoo, tulileweshe na kukumbatiana hata asubuhi
tukifurahishana kwa mapendano!
19Kwani mume hayumo nyumbani mwake,
amekwenda safari, yuko mbali;
20akachukua mfuko wa fedha mkononi mwake,
siku ya mwezi mpevu atarudi nyumbani mwake.
21Hivyo ndivyo, alivyomshinda kwa maneno yake mengi yatelezayo,
akamwangusha kwa huo utelezi wa midomo yake.
22Mara akamfuata kama ng'ombe aendaye kuchinjwa,
kama mwenye wazimu aendaye kufungwa kwa kongwa,
23mpaka mshale uyachome maini yake;
ni kama ndege akimbiliaye tanzi
pasipo kujua, ya kuwa anakwenda kuuawa.
24Sasa wanangu, nisikieni,
yategeeni maneno yangu masikio yenu!
25Uangalie moyo wako, usizielekee njia zake,
nawe usije kupotea penye mapito yake!
26Kwani wengi aliwaangusha alipokwisha kuwatia vidonda,
wote waliouawa naye ni wengi sana.
27Kuingia mwake ni kushika njia za kwenda kuzimuni
zitelemkazo kukufikisha penye vyumba vya kifo.