The chat will start when you send the first message.
1Sikilizeni! Werevu wa kweli unawaita,
utambuzi nao unapaza sauti yake.
2Kileleni juu ya vilima, njia zinapofika,
penye njia panda ndipo, unaposimama.
3Napo penye malango ya kutokea mjini,
hata penye milango ya kuingia unatangaza kwamba:
4Ninyi waume ninawaita,
ninawapalizia sauti, ninyi wana wa Adamu.
5Msipojua kitu, utambueni ubingwa!
Nanyi wapumbavu itambueni mioyo!
6Sikilizeni! Kwani nitasema mambo makuu,
nikifumbua midomo yangu, yatatoka maneno yanyokayo.
7Kwani kinywa changu kitayatamka yaliyo ya kweli,
maneno yasiyomcha Mungu huitapisha midomo yangu.
8Maneno yote ya kinywa changu yanaongoka,
hakuna hata moja lililopotoka la kudanganya watu.
9Yote pia humwelea mwenye utambuzi,
nao wenye ujuzi huona, ya kuwa yamenyoka.
10Yapokeeni mafunzo yangu, mwache fedha!
Maana ujuzi una kima kuliko dhahabu zilizochaguliwa.
11Kwani werevu wa kweli ni mwema kuliko lulu,
nayo yote pia yapendezayo watu hayalingani nao.
12Mimi werevu wa kweli ninakaa pamoja na ubingwa,
nikapata kujua nayo mawazo ya moyo.
13Kumcha Bwana ni kuyachukia mabaya;
kujikuza kujivuna na kushika ufalme wao,
na kusema mapotovu ndiko, ninakochukia.
14Ninayo mashauri mema na ujuzi wa kweli,
tena ninao utambuzi na uwezo.
15Kwa msaada wangu wafalme hushika ufalme wao,
nao wakuu hutoa maongozi yaongokayo.
16Kwa msaada wangu watawalaji hutawala,
nao mabwana wakubwa na waamuzi wote wa nchi.
17Wanipendao ninawapenda,
nao wanitafutao kwa bidii toka asubuhi huniona.
18Mali na macheo ninayo,
hata malimbiko yenye utukufu na mtendo yaongokayo.
19Mazao yangu ni mema kuliko dhahabu,
ijapo ziwe zimetakata sana;
mtu anayoyapata kwangu ni mema
kuliko fedha zilizochaguliwa.
20Ninashika njia iongokayo,
nikapitia katikati palipo sawa,
21niwapate mali wao wanipendao
na kuzijaza vyanja vyao.
22Bwana aliniumba, niwe mwanzo wa njia yake,
hapo kale kabisa, alipokuwa hajatengeneza vingine;
23nikawekwa kuwapo tangu kale, tangu mwanzo,
ulimwengu ulipokuwa haujawa bado.
24Vilindi vilipokuwa havijawa bado, nilikuwa nimezaliwa,
nazo chemchemi zibubujikazo maji zilikuwa hazijawa bado.
25Milima ilipokuwa haijawekewa misingi,
navyo vilima vilipokuwa havijawa bado, nilikuwa nimezaliwa.
26Alipokuwa hajaiumba nchi na mbuga,
nao mwanzo wa mavumbi ulipokuwa haujawa bado,
27alipozishikiza mbingu, ndipo, nilipokuwa naye,
ilikuwa hapo, alipoupima mviringo wake juu ya vilindi vya maji.
28Alipoyashupaza mawingu huko juu,
visima vilivyoko vilindini viliposongana kwa nguvu,
29alipoikatia bahari mipaka yake,
maji yake yasipite hapo, aliposema,
alipoishupaza nayo misingi ya nchi:
30ndipo, nilipokuwa kwake kuzitazama kazi hizo,
nikawa mwenye furaha siku kwa siku
nikicheza mbele yake siku hizo zote.
31Nikacheza katika nchi yake, ilipokaa watu,
nikawafurahia hao watu.
32Sasa wanangu, nisikilizeni!
Wenye shangwe ndio wazishikao njia zangu.
33Yasikieni mafunzo, mpate kuerevuka kweli!
Msiyaache kabisa!
34Mwenye shangwe ni mtu anisikiaye,
alalaye macho siku kwa siku penye malango yangu.
35Kwani aliyenipata mimi amekwisha kupata uzima,
tena huona upendeleo kwake Bwana.
36Lakini asiyenipata mimi huikorofisha roho yake mwenyewe,
kwani wote wanichukiao hupenda kufa.