Mifano 9

Mifano 9

Werevu na ujinga wanawaalika watu.

1*Werevu wa kweli ulijenga nyumba yake,

ukazichonga nguzo zake saba.

2Ukachinja nyama wake, ukaziandalia mvinyo zake,

ukatandika nayo meza yake.

3Kisha ukatuma vijakazi wake kualika wageni

mjini po pote palipoinukia kwamba:

4Aliye mjinga aje kuingia humu!

Nao wasiojua kitu ukawaambia:

5Njoni, mle vilaji vyangu!

Nyweni nazo mvinyo, nilizoziandalia!

6Ninyi wajinga, uacheni ujinga, mpate uzima,

mwendelee katika njia ya utambuzi!

7Amkanyaye mfyozaji hujipatia matusi,

naye aonyaye mtu asiyemcha Mungu hutiwa soni naye.

8Usimwonye mfyozaji, asikuchukie!

Mwonye mwerevu wa kweli naye atakupenda.

9Aliye mwerevu wa kweli mwerevushe,

ndipo, atakapoendelea kuerevuka zaidi.

Aliye mwongofu mfunze!

Ndipo, atakapoendelea kujipatia ujuzi.

10Kumcha Bwana ndio mwanzo wa werevu wa kweli,

tena kumjua Mtakatifu ndio ujuzi.*

11Kwani kwa msaada wangu siku zako zitakuwa nyingi,

nayo miaka yako ya kukaa mwenye uzima itaongozeka.

12Ukiwa umeerevuka kweli, umejipatia mapato ya werevu wa kweli;

ukiwa u mfyozaji, basi, utatwikwa peke yako huo mzigo wako.

13Mwanamke aitwaye ujinga hupiga kelele;

yeye aliye mjinga asiyejua maana ya kitu cho chote

14hukaa mlangoni pa nyumba yake katika kiti

mahali pa mjini panapoinukia,

15awaalike wote wapitao njiani

nao wanaokwenda katika njia zao zinyokazo,

16akisema: Aliye mjinga aje kuingia humu!

Nao wasiojua kitu huwaambia:

17Maji yaliyoibiwa ni matamu,

navyo vilaji vinavyoliwa na kufichaficha hupendeza!

18Naye mjinga hajui, ya kuwa ndiko, mizimu iliko,

ya kuwa wao walioalikwa naye hufika katika makorongo ya kuzimuni.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania