Mashangilio 10

Mashangilio 10

Kuomba msaada wa Mungu kwa ajili ya wakorofi.

1Bwana, ukisimama mbali, ni kwa sababu gani? Ukaja kujificha siku za kusongeka?[#Sh. 44:25.]

2Kwa majivuno yao wasiokucha mnyonge hutishika, na watekwe kwa mapotovu, waliyoyawaza!

3Asiyemcha Mungu hujivunia tamaa za roho yake, naye mwenye choyo humtukana Bwana na kumbeza.

4Asiyemcha Mungu huvimba kichwa kwamba: Halipishi; mawazo yake yote ni kwamba: Hakuna Mungu.

5Njia zake huendelea kwa nguvu siku zote, kwani mapatilizo yako humkalia mbali, wote wamsongao huwafokea.[#Amo. 6:3.]

6Husema moyoni mwake: Sitatikisika, vizazi na vizazi vitapita, nisipatwe na kibaya.[#Sh. 73:4-8.]

7Kinywa chake hujaa viapizo na mapunjo ya kudanganya watu, nayo makorofi na maovu yamo chini ya ulimi wake.[#Rom. 3:14.]

8Hukaa nyuani na kuotea, amwue asiyekosa, watu wasipovijua, macho yake hutunduia walio wanyonge.

9Hunyata na kujifichaficha kama simba kichakani, humnyatia mnyonge, amkamate, humkamata mnyonge kweli na kumnasa tanzini.[#Sh. 17:12.]

10Maana huwatambalia na kunyemelea, mpaka wao wakiwa waanguke makuchani mwake.

11Husema moyoni mwake: Mungu amewasahau, ameuficha uso wake, asiwatazame kale na kale.[#Sh. 94:7.]

12Inuka, Bwana! Nao mkono wako uunyoshe, Mungu! Usiwasahau hao walio wanyonge!

13Sababu gani wakubeze, Mungu, wao wasiokucha wakisema mioyoni mwao: Hutalipisha?

14Kwa kuyatazama makorofi na maumivu umeyaona hayo, namo mkononi mwako ndimo, yalimo sasa; akorofikaye hukuachilia wewe mambo yake yote, naye aliyefiwa na wazazi, wewe humwia msaidiaji.[#Sh. 68:6; 2 Mose 22:23.]

15Ivunje mikono yake asiyekucha kwa kuwa mbaya! Yalipize mabezo yake, yasionekane tena![#Sh. 37:10,36.]

16Bwana ni mfalme siku zote zitakazokuwa kale na kale, wamizimu sharti waangamie nchini kwake.[#Sh. 99:1.]

17Wanyonge umewasikia, Bwana, walipokupigia kite, ukaishikiza mioyo yao na kuwasikiliza kwa masikio yako.

18Huwaamulia waliofiwa na wazazi, nao wakorofikao, mtu asifulize tena kujivuna huku nchini.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania