Mashangilio 145

Mashangilio 145

Kuutukuza ukuu na wema wake Mungu.

1Na nikutukuze, Mungu wangu, uliye mfalme! Na nilisifu Jina lako kale na kale!

2Na nikusifu siku zote, nisikome kulishangilia Jina lako kale na kale!

3Bwana ni mkuu, hushangiliwa sana, ukuu wake hauchunguziki.

4Kizazi kinasifia kizazi kingine kazi zako na kuyatangaza matendo yako yaliyo makuu.

5Urembo na utukufu ndio mapambo yako, mambo yako ya kustaajabisha na niyawaze moyoni!

6Watu na wayaongee ya nguvu zako yaogopeshayo, na niyasimulie matendo yako yaliyo makuu!

7Na waukumbuke wema wako mwingi, wautangaze, nao wongofu wako waupigie vigelegele!

8Bwana ni mwenye utu na mwenye huruma, tena ni mwenye uvumilivu na mwenye upole mkubwa.[#Sh. 103:8; 2 Mose 34:6.]

9Bwana huwaendea wote kwa kuwa mwema, yote aliyoyafanya huyaonea uchungu.[#Rom. 11:32.]

10Bwana, kazi zako zote na zikushukuru, nao wakuchao na wakutukuze!

11Utukufu wa ufalme wako na wauongee! Na wasimuliane matendo yako yaliyo makuu!

12Hayo matendo yako makuu na wayajulishe wana wa watu, hata utukufu na urembo wa ufalme wako![#Sh. 145:5.]

13Ufalme wako ni ufalme wa siku zote za kale na kale, nao ubwana wako ni wa vizazi vyote kwa vizazi na vizazi.

14Bwana huwashikiza wote waangukao, huwainua wote walioinamishwa.[#Sh. 146:8; Luk. 1:52.]

15*Macho yao wote hukutazamia, nawe huwapa vilaji vyao, wanapoona njaa.[#Sh. 104:27-28; 136:25.]

16Unapokifumbua kiganja chako, huwashibisha wote waliopo, wapendezwe.[#Sh. 147:9.]

17Katika njia zake zote Bwana ni mwongofu, katika kazi zake zote ni mwenye upole.[#5 Mose 32:4.]

18Bwana yuko karibu kwao wote wamwitao, kwao wote watakaomwita kwa ukweli.

19Huyafanya yawapendezayo wamwogopao, huyasikia malalamiko yao, wakimlilia, huwaokoa.[#Fano. 10:24.]

20Bwana huwalinda wote wampendao, lakini wote wasiomcha atawaishiliza.

21Kinywa changu sharti kiseme sifa za Bwana! Wote wenye miili ya kimtu sharti walitukuze Jina lake takatifu pasipo kukoma kale na kale!*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania