Mashangilio 37

Mashangilio 37

Mema, wabaya wayapatayo, hayakai; mema ya kweli ndiyo, waongofu wayapatayo.

(Taz. Sh. 49:1-20; 73:1-28; Iyobu.)

1Kwa ajili yao watendao mabaya usijichafushe moyo, wala wafanyao mapotovu usiwaonee wivu![#Fano. 24:19.]

2Kwani hunyauka upesi kama majani, kama machipuko mazuri ya uwandani watakauka.

3Mwegemee Bwana, ufanye mema! Kaa katika nchi, ujilishe mambo yaelekeayo![#Sh. 37:27,29.]

4Furaha zilizoko kwake Bwana na zikutoshe! Naye ndiye atakayekupa, moyo wako uyatakayo.

5Acha, Bwana akuchagulie njia, utakayoishika! Mwegemee tu, yeye atafanya![#1 Petr. 3:7.]

6Atautokeza wongofu wako, uwe kama mwanga; nayo mashauri yako yataangazika kama jua la mchana.[#Sh. 97:11; 112:4; Iy. 11:17.]

7Mnyamazie Bwana na kumngoja! Mwenzio akiona mema njiani, usiwake moto, ijapo awe mtu afanyaye madanganyo![#Sh. 73:3.]

8Tuliza ukali, uache kufoka! Usiwake moto, usije kukukosesha!

9Kwani wafanyao mabaya watang'olewa, lakini wao wamngojeao Bwana wataitwaa nchi.[#Sh. 37:11,22,29,34; Mat. 5:5.]

10Bado kidogo asiyemcha Mungu atakuwa hayupo tena; hapo, utakapopachungulia mahali pake, patakuwa hapapo.[#Sh. 37:35.]

11Lakini wapole ndio watakaoitwaa nchi, kwa kupata matengemano mengi furaha zitawatosha.[#Sh. 37:9; Mat. 5:5.]

12Asiyemcha Mungu huwaza, jinsi atakavyomponza mwongofu, hukereza meno yake kwa ajili yake yeye.

13Lakini Bwana humcheka kwa kupaona, siku yake itakapofika.[#Iy. 18:20.]

14Wasiomcha Mungu huchomoa panga na kuzipinda pindi zao, wapate kuwaangusha walio wanyonge na wakiwa, nao wafuatao njia zinyokazo wawachinje.[#Sh. 11:2.]

15Lakini panga zao zitaichoma mioyo yao wenyewe, nazo pindo zao zitavunjika.

16Mema machache ya mwongofu ni mali, nazo zinapita mafuriko mengi yao wasiomcha Mungu.[#Fano. 15:16.]

17Kwani mikono yao wasiomcha Mungu itavunjwa, lakini wao walio waongofu Bwana huwashikiza.

18Bwana huzijua siku zao wamchao, nayo mafungu yao yatakuwapo kale na kale

19Siku zitakapokuwa mbaya, hawatatwezeka, ila watashiba vema nazo siku za njaa.[#Sh. 33:19.]

20Kwani wasiomcha Mungu wataangamia, nao wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa majani ya uwandani unavyotoweka; watatoweka kweli kama moshi.[#Sh. 68:3.]

21Asiyemcha Mungu hukopa, asiweze kulipa; mwongofu huweza kugawia na kuwapa watu.

22Kwani wabarikiwao naye Bwana huitwaa nchi, lakini waapizwao naye watang'olewa.[#Mat. 25:34,41; Sh. 37:9.]

23Mwendo wa mtu unashupazwa naye Bwana, akiwa anapendezwa na njia, yule anayoishika.

24Kama anajikwaa, hataangushwa chini, kwani Bwana humshika mkono wake.[#Fano. 24:16.]

25Nalikuwa kijana, nikaja kuwa mzee, lakini sijaona bado mwongofu aliyeachwa peke yake, wala watoto wake wakiombaomba chakula.[#Sh. 34:10-11.]

26Kila siku anaweza kugawia wengine, hata kuwakopesha, nao watoto wake hubarikiwa.

27Ondoka pabaya ufanye mema! Ndivyo, utakavyokaa kale na kale.[#Sh. 34:15.]

28Kwani Bwana huyapenda yaongokayo, hatawaacha kabisa wao wamchao, watakuwa wamelindwa kale na kale, lakini watoto wao wasiomcha watang'olewa.[#Sh. 11:7.]

29Walio waongofu wataitwaa nchi, wakae humo kale na kale.[#Yes. 60:21.]

30Kinywa chake mwongofu hueleza yenye werevu wa kweli, ulimi wake husema yaongokayo.

31Maonyo ya Mungu wake yamo moyoni mwake, kwa hiyo hatikisiki atakapokwenda pote.[#Sh. 40:9.]

32Asiyemcha Mungu humwotea mwongofu akitafuta kumwua.[#Sh. 10:8-10.]

33Lakini Bwana hatamwacha mkononi mwake; hata akihukumiwa naye yule, hatamhesabu kuwa mbaya.[#Sh. 34:22.]

34Ishike njia yake Bwana na kumngojea! Ndipo, atakapokukweza, uitwae nchi; nako kung'olewa kwao wasiomcha utakufurahia.[#Sh. 37:9.]

35Nimeona mtu asiyemcha Mungu, akawa mkorofi, akawa mnene sana kama mtamba wenye majani mengi.[#Iy. 5:3-5; 20:6-7; Ez. 31:3-14.]

36Lakini nilipomtazama, siku zilipopita, alikuwa hayupo, nikamtafuta, lakini hakuoneka.[#Sh. 37:10.]

37Jilinde, ukae na kumcha Mungu, uyatazamie yanyokayo! Kwani mtu aliye hivyo mwisho hutengemana.[#1 Mose 39:8-9.]

38Lakini wapotovu huangamizwa wote pamoja, mwisho wao wasiomcha Mungu ni kung'olewa.

39Wokovu wao waongofu hutoka kwake Bwana, yeye ni nguvu yao siku, wanaposongeka.[#Sh. 46:2.]

40Bwana huwasaidia na kuwaopoa, huwaopoa mikononi mwao wasiomcha Mungu; kwa kuwa humkimbilia, huwaokoa.[#Luk. 18:7-8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania