Ufunuo 2

Barua kwa wateule wa Efeso.

1Malaika wa wateule walioko Efeso mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye anayezishika zile nyota saba mkononi mwake mwa kuume, anayekwenda katikati ya zile taa saba za dhahabu:[#Ufu. 1:13,16,20.]

2Nayajua matendo yako na usumbufu na uvumilivu wako; nakujua: huwezi kuwavumilia waovu, ukawajaribu wale wanaojisema kuwa mitume, lakini sio mitume; nawe uliwaona kuwa waongo.[#Ufu. 2:9,13,19; 3:1; 8:13; 1 Yoh. 4:1.]

3Ukavumilia ulipoumizwa kwa ajili ya Jina langu, hukuchoka.

4Lakini ninakuonya, ya kuwa umeuacha upendo wako wa kwanza.

5Kumbuka, uliyoyapoteza ulipoanguka! Kisha juta, uyafanye yale matendo ya kwanza! Usipoyafanya, nitakujia, niiondoe taa yako mahali pake, ukiwa hukujuta.[#Ufu. 2:16,22; 3:3,19.]

6Lakini neno hili unalo, ya kuwa unayachukia matendo yao Wanikolai, ninayoyachukia hata mimi.[#Ufu. 2:15; Sh. 139:21.]

7Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Mwenye kushinda nitampa kula matunda ya mti wa uzima ulioko katika paradiso ya Mungu.[#Ufu. 2:11,17,26; 3:5,12,21; 22:2; 1 Mose 2:9; 3:22,24.]

Barua kwa wateule wa Simirna.

8*Malaika wa wateule walioko Simirna mwandikie: Ndivyo, anavyosema yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, akapata kuishi tena:[#Ufu. 1:11,17,18.]

9Nayajua matendo na maumivu yako na umaskini wako, lakini u mwenye mali nyingi. Nakujua, unavyotukanwa nao wajisemao kuwa Wayuda, lakini sio, ila ni wanafuzi wake Satani.[#Ufu. 3:9; 2 Kor. 11:14-15; Yak. 2:5.]

10Usiyaogope, utakayoteswa! Tazama, Msengenyaji atawatia wengine wenu kifungoni, mpate kujaribiwa. Nanyi mtaumizwa siku kumi. Uwe mwelekevu mpaka kufa! Ndipo, nitakapokupa kilemba cha uzima.[#Ufu. 3:11; Mat. 10:28; 2 Tim. 4:8.]

11Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule! Mwenye kushinda hatapotolewa na kufa kwa pili.*[#Ufu. 20:14.]

Barua kwa wateule wa Pergamo.

12Malaika wa wateule walioko Pergamo mwandikie: Ndivyo, anavyosema mwenye ule upanga mkali wenye makali pande mbili:[#Ufu. 1:16; Yes. 49:2; Ebr. 4:12.]

13Napajua, unapokaa. Ni hapo, kiti cha kifalme cha Satani kilipo. Lakini unalishika sana Jina langu, hukukana, ya kuwa unanitegemea mimi, hata siku zile, shahidi wangu mwelekevu Antipa alipouawa huko kwenu, Satani anakokaa.[#Ufu. 3:8; 13:2.]

14Lakini ninayokuonya, ni machache, ya kuwa unao kwako wanaoushika ufundisho wa Bileamu aliyemfundisha Balaka kukwaza wana wa Isiraeli, akiwafundisha kula nyama za tambiko na kufanya ugoni.[#4 Mose 31:16; Yuda 11.]

15Vivyo hivyo hata wewe unao wanaoyashika mafundisho ya Wanikolai yaliyo hivyo.[#Ufu. 2:6.]

16Sasa juta! Usipojuta, nitakujia upesi, nipigane nao kwa upanga uliomo kinywani mwangu.[#Ufu. 1:16.]

17Mwenye masikio na asikie, Roho anavyowaambia wateule! Mwenye kushinda nitamgawia ile Mana iliyofichwa, kisha nitampa kijiwe cheupe, namo katika kijiwe hiki limeandikwa jina jipya lisilojulika kwa mtu, asipokuwa mwenye kulipata.[#Ufu. 3:12; Sh. 78:24; Yes. 62:2.]

Barua kwa wateule wa Tiatira.

18Malaika wa wateule walioko Tiatira mwandikie: Ndivyo, anavyosema Mwana wa Mungu aliye mwenye macho yaliyo kama moto unaowaka, ambaye miguu yake imefanana na shaba nyekundu:[#Ufu. 1:14-15.]

19Nayajua matendo yako ya kupenda na ya kumtegemea Mungu na ya kutumikia na ya kuvumilia kwako. Tena najua: kazi zako za mwisho ni nyingi kuliko za kwanza.

20Lakini ninakuonya, ya kuwa humkatai mwanamke Izebeli anayejisema kuwa mfumbuaji, akiwafundisha na kuwapoteza watumwa wangu, wafanye ugoni, tena wale nyama za tambiko.[#Ufu. 2:4; 1 Fal. 16:31; 2 Fal. 9:22.]

21Nimempa siku za kujuta, lakini hataki kujuta na kuuacha ugoni wake.

22Tazama, nitambwaga kitandani, nao waliofanya naye ugoni vilevile, waumizwe sana, wasipojuta na kuyaacha matendo yake.

23Hata watoto wake nitawaua, wafe. Ndipo, wateule wote watakaponitambua, ya kuwa mimi ni mwenye kuyapeleleza mafigo, hata mioyo. Nami nitawapa ninyi kila mmoja, kama matendo yenu yalivyo.[#Sh. 7:10; Yer. 17:10.]

24Wengine wenu ninyi, mlioko Tiatira, msioyafuata hayo mafundisho, msiovitambua vilindi vya Satani, nawaambia ninyi kwa mfano: Siwatwiki mzigo wa wengine,

25ila hicho, mlicho nacho, kishikeni, mpaka nitakapokuja![#Ufu. 3:11.]

26Mwenye kushinda na kuzishika kazi zangu mpaka mwisho nitampa kuwa mkuu wa wamizimu;

27naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, awapondeponde kama vyungu vya udongo.[#Ufu. 12:5.]

28Kama nami nilivyopewa na Baba yangu, nitampa naye nyota ya mapema.[#Sh. 2:8-9.]

29Mwenye masikio na asikie, Roho anayowaambia wateule![#Ufu. 3:6,13,22.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania