Ufunuo 5

Kitabu kilichotiwa muhuri saba.

1Nikaona mkononi mwa kuume mwake yule aliyekaa kitini mwa kifalme kitabu kilichoandikwa ndani na mgongoni, nacho kilikuwa kimetiwa muhuri saba.[#Ufu. 4:2; Ez. 2:9-10.]

2Kisha nikaona malaika mwenye nguvu, akatangaza kwa sauti kuu: Yuko nani apaswaye na kukifungua kitabu na kuziondoa muhuri zake?

3Hakuwako hata mmoja wala mbinguni wala nchini wala kuzimuni aliyeweza kukifungua kitabu na kukitazama.

4Ndipo, nilipolia sana, kwa sababu hakuonekana hata mmoja apaswaye na kukifungua kitabu na kukitazama.

5Mmoja wao wale wazee akaniambia: Usilie! Tazama, yule simba wa shina la Yuda aliye mzizi wa Dawidi, yeye ameshinda, apate kukifungua kitabu na kuziondoa muhuri zake saba.[#Ufu. 22:16; 1 Mose 49:9-10; Yes. 11:1,10.]

Kinatwaliwa na Mwana kondoo.

6Kisha nikaona mwana kondoo aliyesimama katikati penye kiti cha kifalme na wale nyama wanne na wale wazee, naye alikuwa, kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba; ndio zile roho saba za Mungu zilizotumwa kwenda kuzifikia nchi zote.[#Ufu. 4:5; Yes. 53:7; Zak. 4:10; Yoh. 1:29,36.]

7Alipokuja akakitwaa kitabu mkononi mwa kuume mwake yeye aliyekaa kitini mwa kifalme.

8Hapo alipokitwaa kitabu, ndipo, wale nyama wanne na wale wazee 24 walipomwangukia Mwana kondoo. Wakawa wameshika kila mmoja zeze na vyano vya dhahabu vilivyojaa uvumba, ndio maombo ya watakatifu.[#Ufu. 8:3-4; 14:12; 15:2.]

9Nao wakaimba wimbo mpya wakisema:

Wewe umepaswa na kukipokea kitabu na kuziondoa

muhuri zake, kwani umechinjwa, umkombolee Mungu kwa

damu yako watu wa mashina yote na wa misemo yote

na wa makabila yote na wa wamizimu wote,

10ukawafanya,

wawe wafalme na watambikaji wa Mungu wetu; ndio

watakaozitawala nchi.

Sifa ya Mwana kondoo.

11Kisha nikaona, nikasikia sauti ya malaika wengi waliokizunguka kiti cha kifalme na wale nyama na wale wazee. Nilipowahesabu, walikuwa maelfu na maelfu na maelfu, wakasema kwa sauti kuu:[#1 Fal. 22:19; Dan. 7:10.]

12Mwana kondoo aliyechinjwa amepaswa na kupokea

uwezo na malimbiko na werevu wa kweli

na nguvu na heshima na utukufu na mapongezo.

13Navyo viumbe vyote vilivyoko mbinguni, navyo vilivyopo nchini, navyo vilivyoko kuzimuni, navyo vilivyomo baharini, navyo vyote vilivyomo ndani yao, nikavisikia, vikisema:

Mpeni yeye aliyekaa kitini mwa kifalme naye Mwana kondoo

mapongezo na heshima na utukufu na nguvu

kale na kale pasipo mwisho!

14Wale nyama wanne waliposema: Amin, ndipo, wale wazee walipoanguka chini, wakamsujudia mwenye kuishi kale na kale.[#Ufu. 4:10; 19:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania