Ruti 2

Ruti 2

Ruti alipookoteza kwake Boazi anahurumiwa.

1Kulikuwa na mtu aliyekuwa fundi wa vita mwenye nguvu, naye alijuana sana na mumewe Naomi, alikuwa wa mlango wa Elimeleki, jina lake Boazi.

2Ruti wa Moabu akamwambia Naomi: Na niende shambani kuokoteza masuke nikimfuata mtu, nitakayempendeza machoni pake. Akamwambia: Nenda, mwanangu!

3Akaenda, akaja kuokoteza shambani akiwafuata wavunaji. Ikatukia kwa bahati, lile fugu la shamba kuwa lake Boazi aliyekuwa wa mlango wa Elimeleki.

4Ndipo, Boazi alipokuja toka Beti-Lehemu, akawaambia wavunaji: Bwana awe nanyi! Wakamwitikia: Bwana akubariki!

5Boazi akamwuliza kijana aliyewasimamia wavunaji: Huyu kijana wa kike ni wa nani?

6Yule kijana aliyewasimamia wavunaji akamjibu akimwambia: Huyu ni kijana wa Kimoabu aliyerudi na Naomi, alipotoka kwenye mbuga za Moabu.

7Alituambia: Na niokoteze na kukusanyakusanya penye miganda nikiwafuata wavunaji. Basi, akaja, akashinda hapa tangu asubuhi mpaka sasa; sasa anapumzika kidogo pale penye dungu.

8Ndipo, Boazi alipomwambia Ruti: Sikia, mwanangu! Usiende kuokoteza shambani pengine, wala usiondoke hapa, fuatana tu na vijana wa kwangu!

9Elekeza macho tu shambani, wanapovuna, uwafuate! Nimewaagiza hawa vijana, wasikusumbue. Ukiona kiu, nenda tu kwenye vyombo vyao, kanywe vijana hawa waliyoyachota!

10Ruti akamwangukia usoni pake na kumwimamia hapo chini, akamwambia: Mbona nimekupendeza machoni pako, unionee mema? Nami ni mgeni.

11Boazi akamjibu, akamwambia: Nimesimuliwa yote pia, uliyomfanyizia mkweo, mumeo alipokwisha kufa, ya kuwa umemwacha baba yako na mama yako na nchi, uliyozaliwa, ukaja kwa ukoo wa watu, usiowajua zamani zote.[#Ruti 1:16-17.]

12Bwana na akurudishie hayo matendo yako, upate mshahara wako wote mzima kwake Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa kuwa umekuja kumkimbilia mabawani pake.

13Akamjibu: Kumbe nimekupendeza machoni pako, bwana wangu, ukanituliza moyo, ukaniambia maneno yaliyoingia moyoni mwa kijakazi wako, nami si kama mmoja wao hawa vijakazi wako!

14Saa wanapolia chakula, Boazi akamwambia: Karibu hapa, ule huku chakulani, nacho kitonge chako ukichovye hapa sikini! Akakaa kando ya wavunaji, naye akamgawia bisi, akala, hata akishiba, nyingine akazisaza.

15Alipoondoka kwenda kuokoteza, Boazi akawaagiza vijana wake kwamba: Hata katikati ya miganda na aokoteze, msimkaripie.

16Namo migandani mtoe mengine, myaache, aje kuyaokoteza, msimkaripie.[#3 Mose 19:9.]

17Akaokoteza shambani mpaka jioni, akayapura maokotezo yake, yakawa kama frasila ya mawele.

18Akayachukua, akaja mjini. Mkwewe alipoyaona hayo maokotezo yake, akayatoa nayo, aliyoyasaza hapo, alipokula na kushiba, akampa.

19Mkwewe akamwuliza: Umeokoteza wapi leo? Umekwenda wapi kufanya kazi? Aliyekuonea mema na abarikiwe! Akamsimulia mkwewe, kama ni nani, ambaye amezifanya kazi zake kwake, akasema: Jina la huyo mtu, ambaye nimezifanya leo kazi zangu kwake, ndiye Boazi.

20Ndipo, Naomi alipomjibu mkwewe: Na abarikiwe na Bwana! Kwa kuwa hakuacha kuwatolea mema, wala wazima, wala wafu. Naomi akamwambia tena: Mtu huyo ni ndugu yetu, naye ni mmoja wa waingiliaji wetu.

21Ruti wa Moabu akamwambia: Tena ameniambia: Fuatana na hawa vijana wa kwangu, mpaka watakapoyamaliza mavuno yangu!

22Naomi akamjibu mkwewe Ruti: Inafaa, mwanangu, ukitoka pamoja na vijakazi wake, wasikukaripie halafu shambani.

23Basi, akafuatana na vijakazi wa Boazi kwenda kuokoteza, mpaka walipoyamaliza mavuno ya mawele na mavuno ya ngano; kisha akakaa kwa mkwewe.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania