The chat will start when you send the first message.
1Katika mwezi wa nane katika mwaka wa pili wa Dario neno la Bwana lilimjia mfumbuaji Zakaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kwamba:[#Ezr. 5:1.]
2Bwana alikuwa amewakasirikia sana baba zenu.
3Kwa hiyo uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Rudini kwangu! ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi; ndipo, nami nitakaporudi kwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#Mal. 3:7; Yak. 4:8.]
4Msiwe kama baba zenu walioambiwa na wafumbuaji wa kwanza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Rudini na kuziacha njia zenu mbaya na kazi zenu mbaya! Lakini hawakusikia, wala hawakunitegea masikio; ndivyo, asemavyo Bwana.
5Basi, baba zenu wako wapi? Nao wafumbuaji watakuwapo kale na kale?
6Ila maneno yangu na maagizo yangu, niliyowaagiza watumishi wangu wafumbuaji kuyatangaza, hayakutimia kwa baba zenu? Ndipo, walipojirudia na kusema: Kama Bwana Mwenye vikosi alivyowaza moyoni kutufanyizia kwa ajili ya njia zetu na kwa ajili ya matendo yetu, ndivyo, alivyotufanyizia kweli.
7Siku ya ishirini na nne ya Mwezi wa kumi na moja, ndio mwezi wa Sebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana likamjia mfumbuaji Zakaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kwamba:
8Usiku huu nimeona mambo: nimeona mtu aliyepanda farasi mwekundu; naye alikuwa amesimama katikati ya miti ya vihagilo iliyoko huko chini bondeni, nyuma yake walikuwa farasi wekundu na wa kijivujivu na weupe.[#Zak. 6:1-8.]
9Nikauliza: Wa nini hawa, Bwana wangu? Akaniambia yule malaika aliyesema na mimi: Mimi nitakuonyesha, kama hawa ni wa nini.
10Akajibu yule mtu aliyesimama katikati ya vihagilo, akasema: Hawa ndio, Bwana aliowatuma kutembea katika nchi po pote.
11Wakamjibu malaika wa Bwana aliyesimama katikati ya vihagilo, wakasema: Tumetembea po pote katika nchi, tukaiona nchi yote nzima, ya kuwa inatulia kimya.
12Ndipo, malaika wa Bwana alipojibu akisema: Bwana Mwenye vikosi, utaacha mpaka lini kuuhurumia Yerusalemu nayo miji ya Yuda, uliyoikasirikia hii miaka 70?[#Sh. 102:14; Dan. 9:2.]
13Bwana akamjibu malaika aliyesema na mimi, akamwambia maneno mema ya kuutuliza moyo.
14Kisha malaika aliyesema na mimi akaniambia: Tangaza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Nimeingiwa na wivu mwingi kwa ajili ya Yerusalemu na kwa ajili ya Sioni.
15Tena mimi ninawakasirikia sanasana wao wa hayo mataifa yanayokaa na kutulia; kwani nilipokasirika, ilikuwa kidogo tu, lakini wao wamejihimiza kuwafanyia mabaya.[#Yes. 47:6.]
16Kwa hiyo Bwana anasema hivi: Nimeugeukia Yerusalemu tena kwa huruma nyingi, Nyumba yangu ijengwe tena mwake; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi, hata kamba za kupimia viwanja zitavutwa tena mle Yerusalemu.[#Zak. 8:3.]
17Kisha tangaza kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Miji yangu itafurikiwa tena na mema yote, naye Bwana ataituliza tena mioyo ya Wasioni, maana atauchagua tena Yerusalemu, uwe wake.[#Yes. 14:1; 40:1-2.]
18Nilipoyainua macho yangu, nichungulie, mara nikaona pembe nne.
19Nikamwuliza malaika aliyesema na mimi: Za nini hizi? Akaniambia: Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Wayuda na Waisiraeli na Wayerusalemu.
20Kisha Bwana akanionyesha wafua vyuma wanne.
21Nikauliza: Hawa wanakuja kufanya nini? Akajibu kwamba: Hizo ndizo pembe zilizowatawanya Wayuda, asipatikane hata mtu mmoja aliyeweza kukiinua kichwa chake. Lakini hawa wamekuja kuzitisha na kuzibwaga zile pembe za wamizimu walioziinua pembe zao na kuzielekezea nchi ya Yuda, wapate kuwatawanya waliokuwako.