The chat will start when you send the first message.
1Ifungue milango yako, Libanoni, moto uile miangati yako!
Ombolezeni, ninyi mivinje, kwa kuwa miangati imeanguka!
Miti hiyo iliyokuwa yenye utukufu, imeangamizwa!
2Ombolezeni, ninyi mivule ya Basani!
Kwani msitu uliokuwa hauingiliki umeanguka.
3Sikilizeni, wachungaji wanavyolia,
kwa kuwa hayo malisho yao mazuri mno yameangamizwa!
Sikilizeni, wana wa simba wanavyonguruma,
kwani machaka ya Yordani, waliyojivunia, yameangamizwa!
4Hivi ndivyo, Bwana Mungu wangu anavyosema: Wachunge kondoo walio wa kuuawa tu!
5Waliowanunua huwaua pasipo kukora manza; nao waliowauza husema: Atukuzwe Bwana, kwa kuwa nimepata mali! Nao wachungaji wao hawawahurumii.[#Yer. 23; Ez. 34.]
6Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Sitawahurumia tena wakaao katika nchi hii, utaniona, mimi nikiwatoa watu hawa na kuwatia kila mtu mkononi mwa mchungaji wake namo mkononi mwa mfalme wake, ndio watakaoiponda nchi hii, nami sitawaponya mikononi mwao.
7Basi, nikawachunga hao kondoo walio wa kuuawa tu, nao walikuwa kondoo wanyonge kweli; nikajichukulia fimbo mbili, moja nikaiita Mapendeleo, ya pili nikaiita Mapatanisho, nikawachunga hao kondoo.[#Zak. 11:11.]
8Nikatowesha wachungaji watatu katika mwezi mmoja, kisha Roho yangu ikashindwa kuwavumilia, roho zao nazo zikanichukia.
9Nikasema: Sitawachunga ninyi, watakaokufa na wafe! Nao watakaotoweka na watoweke! Nao watakaosalia na walane kila mtu nyama za mwili wa mwenziwe![#Yer. 15:2.]
10Kisha nikaichukua fimbo yangu iitwayo Mapendeleo, nikaivunja, ni kwamba: Nilitangue agano langu, nililolifanya na makabila yote.
11Siku ile, lilipotanguliwa, ndipo, wale kondoo wanyonge walioniangalia walipotambua, ya kuwa hiyo ilifanyika kwa neno la Bwana.[#Zak. 11:7.]
12Nikawaambia: Mkiona kuwa vema, nipeni mshahara wangu! Kama sivyo, acheni! Wakanipimia fedha 30, ziwe mshahara wangu.[#Mat. 26:15.]
13Kisha Bwana akaniambia: Mtupie mfinyanzi kima hiki kizuri, walichoniwazia kuwa malipo yangu mimi! Nikazichukua hizo fedha 30, nikazipeleka Nyumbani mwa Bwana, nikamtupia mfinyanzi.[#Mat. 27:9-10.]
14Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Mapatanisho, ni kwamba: Niutangue udugu wao Wayuda nao wa Waisiraeli.[#Ez. 37:22.]
15Bwana akaniambia: Jichukulie tena vyombo vya mchungaji asiyefaa kitu!
16Kwani utaniona, mimi nikiinua katika nchi hii mchungaji asiyewakagua waliotoweka, asiyewatafuta waliopotea, asiyewaponya waliovunjika, asiyewatunza walio wakiwa, lakini nyama za vinono atazila, nazo kwato zao ataziondoa kwa nguvu.
17Yatampata huyo mchungaji wangu asiyefaa, anayewaacha kondoo! Upanga utaupiga mkono wake na jicho lake la kuume, mkono wake ukauke kabisa, nalo jicho lake la kuume lipofuke kabisa.