The chat will start when you send the first message.
1Mtaona, siku ya Bwana ikija; ndipo, mateka yako yatakapogawanywa mjini mwako.[#Yes. 39:6; Zak. 12:3.]
2Kwani nitawakusanya wamizimu wote, waje kuupelekea Yerusalemu vita; ndipo, huo mji utakapochukuliwa, nazo nyumba zitatekwa, hata wanawake watatiwa soni. Kisha nusu ya watu wa mji watatoka humo kwenda utumwani, lakini walio masao ya watu wa humo mjini hawataangamizwa.
3Kisha Bwana atatoka kupigana nao hao wamizimu, kama alivyopigana nao hata siku nyingine za vita.[#Ufu. 19:19.]
4Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa michekele ulioko ng'ambo ya Yerusalemu upande wa maawioni kwa jua; ndipo, huo mlima wa michekele utakapopasuka, pawe korongo kubwa sana katikati lielekealo nusu maawioni kwa jua, nusu baharini, kipande kimoja cha mlima huo kikiondoka upande wa kaskazini, kipande chake kingine upande wa kusini.
5Nanyi mtapata kukimbilia mle bondeni kwenye milima yangu, kwani hilo bonde la milima yangu litakwenda kufika mpaka Aseli; nanyi mtakimbia, kama mlivyoukimbia ule mtetemeko wa nchi siku za Uzia, mfalme wa Yuda. Kisha Bwana Mungu wangu atakuja, nao watakatifu wote watakuwa pamoja na wewe.[#Amo. 1:1.]
6Siku hiyo haitakuwa na mwanga, nazo nyota zimetukazo zitaguiwa na giza.
7Siku hiyo moja inayojulikana kwake Bwana haitakuwa mchana wala usiku, lakini wakati wa jioni patakuwa na mwanga tena.[#Mar. 13:32.]
8Siku hiyo ndipo, maji yenye uzima yatakapotoka Yerusalemu, nusu yatakwenda katika bahari iliyoko maawioni kwa jua, nusu yatakwenda katika bahari nyingine; yatakuwa vivyo hivyo siku za kiangazi na siku za kipupwe.[#Ez. 47:1-8.]
9Naye Bwana atakuwa mfalme wa nchi yote nzima tena siku hiyo Bwana atakuwa yeye mmoja, nalo Jina lake litakuwa hilo moja.[#Sh. 97:1; Ufu. 11:15.]
10Nchi yote nzima itageuka kuwa nchi ya tambarare toka Geba hata Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu. Lakini huu wenyewe utatukuka kwa kukaa mahali pake kuanzia penye lango la Benyamini kufikia mahali pa lango la kwanza napo penye lango la pembeni hata mnara wa Hananeli mpaka penye makamulio ya mfalme.[#Yer. 31:38.]
11Humo ndimo, watu watakamokaa pasipo kupatwa tena na kiapizo cho chote; ndivyo, Yerusalemu utakavyokaa salama.[#Yer. 33:16; Ufu. 22:3.]
12Hili ndilo pigo, Bwana atakaloyapiga makabila yote yaliyopeleka vikosi vyao kupigana na Yerusalemu: ataziozesha nyama za miili yao, wakiwa wamesimama kwa miguu yao, nayo macho yao yataoza ndani ya matundu yao, nazo ndimi zao zitaoza vinywani mwao.
13Tena siku hiyo ndipo, patakapokuwa kwao kitisho kikubwa kitokacho kwa Bwana, kila mtu akamate mkono wa mwenziwe, nao mkono wake yule utauinukia mkono wa mwenziwe.
14Wayuda nao watakuja kupigana mle Yerusalemu, mali za wamizimu wote pia wanaokaa na kuuzunguka zitakapokusanywa mle: dhahabu na fedha na nguo za sikukuu nyingi mno.
15Lile pigo litapiga vilevile nao farasi na nyumbu na ngamia na punda na nyama wote pia watakaokuwamo makambini mwao hao, liwe sawa na pigo lile la watu.
16Kisha masao ya wamizimu wote waliokuja kupigana na Yerusalemu watatoka kwao kuja kupanda papo hapo mwaka kwa mwaka, wamwangukie mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi, na kuila sikukuu ya Vibanda.[#Zak. 14:9.]
17Lakini kama mlango mmoja wa milango ya nchi hautapanda Yerusalemu kumwangukia mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi, basi, kwao mvua haitanyesha.
18Ingawa mlango wa Wamisri usipande kufika huko, basi, hata kwao mvua haitanyesha. Hilo ndilo pigo, Bwana atakalowapiga wamizimu watakaokataa kupanda huko, waile sikukuu ya Vibanda.
19Hilo litakuwa kosa lao Wamisri na kosa lao wamizimu wote watakaokataa kupanda huko, waile sikukuu ya Vibanda.
20Siku hiyo ndipo, njuga za farasi zitakapokuwa zimeandikwa: Watakatifu wa Bwana. Nazo sufuria zilizomo Nyumbani mwa Bwana zitawaziwa kuwa sawa na vyano vilivyoko penye meza ya kutambikia.[#2 Mose 28:36.]
21Ndipo, kila sufuria iliyomo Yerusalemu au iliyoko katika nchi ya Yuda itakapokuwa takatifu ya Bwana Mwenye vikosi; kwa hiyo wote watakaokuja kutambika watajichukulia moja yao, wajipikie mle nyama ya tambiko. Siku hiyo hatakuwako tena Mkanaani hata mmoja atakayeingia Nyumbani mwa Bwana Mwenye vikosi.[#Ufu. 21:27.]