The chat will start when you send the first message.
1Kisha akanionyesha mtambikaji mkuu Yosua, akisimama mbele ya malaika wa Bwana, naye Satani alikuwa amesimama kuumeni kwake kumsengenya.[#Hag. 1:1; Iy. 1:9; Ufu. 12:10.]
2Bwana akamwambia Satani: Bwana na akukemee wewe, Satani! Yeye Bwana aliyeuchagua Yerusalemu, uwe mji wake, na akukemee wewe! Kumbe huyu si kijinga kilichopona kwa kuokolewa motoni![#Amo. 4:11; Yuda 9.]
3Naye Yosua alikuwa amevaa nguo chafu aliposimama mbele ya malaika.
4Kisha huyu akasema na kuwaambia waliosimama mbele yake kwamba: Mvueni hizi nguo chafu! Akamwambia: Tazama, manza, ulizozikora, nimeziondoa kwako, nikakuvika nguo za sikukuu.[#Yes. 6:7; 61:3.]
5Kisha akasema: Mfungeni kilemba kilichotakata kichwani pake! Wakamfunga kilemba kilichotakata kichwani pake pamoja na kumvika zile nguo, naye malaika wa Bwana alisimama papo hapo.[#2 Mose 28:39.]
6Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yosua kwamba:
7Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kama utakwenda katika njia zangu na kuutumikia utumishi wangu, ndipo, wewe utakapoitunza Nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, kisha nitakupatia njia ya kufika kwangu katikati yao hawa wanaosimama hapa.[#Sh. 91:11.]
8Sasa sikia, wewe mtambikaji mkuu Yosua pamoja na wenzako wanaokaa mbele yako, kwani ndio watu wa kutazamiwa: Mtaniona, nikimleta mtumishi wangu Chipukizi.[#Yes. 8:18; Yer. 23:5; 33:15; Zak. 6:12.]
9Kwani tazameni: Jiwe hili, nililoliweka mbele yake Yosua, macho saba yanalielekea jiwe hili moja; tena tazameni: Mimi ninachora humo machoro yanayolipasa, kisha nitaziondoa manza za nchi hii katika siku moja; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.[#Zak. 4:10; Ufu. 5:6.]
10Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Siku hiyo ndipo, watakapoalikana mtu na mwenziwe kuja kukaa pamoja chini ya mzabibu na chini ya mkuyu.[#1 Fal. 4:25; Mika 4:4.]