1 Samweli 8

1 Samweli 8

Waisraeli waomba kuwa na mfalme

1Na Samweli alipozeeka, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli.[#Kum 16:18; Amu 10:4; 12:14]

2Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza lilikuwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba.

3Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.[#Mhu 2:19; Yer 22:15; Kut 18:21; Kum 16:19; 1 Tim 3:3; 6:10; Zab 15:5]

4Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;

5wakamwambia, Angalia, wewe umezeeka, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tuteulie mfalme atutawale kama mataifa yale mengine yote.[#Kum 17:14; 1 Sam 12:13; Hos 13:10; Mdo 13:21]

6Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA.[#Kut 32:31,32; 1 Sam 15:11; Mit 3:5]

7BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.[#Kut 16:8; Mt 10:24,25; Lk 10:16; Yn 13:16; 1 Sam 10:19]

8Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.

9Basi sasa, isikilize sauti yao; lakini, uwaonye sana, na kuwaonesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.

10Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya BWANA.

11Akasema, Mfalme atakayewatawala ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, katika magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.[#Kum 17:16; 1 Sam 10:25; 14:52; 2 Nya 26:10-15]

12Naye atawaweka kwake kuwa wakuu juu ya maelfu, na makamanda juu ya hamsini hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.

13Na binti zenu atawatwaa kuwa watengenezaji wa marhamu, wapishi na waokaji.

14Atatwaa mashamba yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.[#1 Fal 21:7]

15Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape wakuu wake, na watumishi wake.

16Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe wenu walio wazuri sana, na punda wenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe.

17Atawatoza fungu la kumi la mifugo wenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.

18Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile.[#Ayu 27:9; Zab 18:41; Mit 1:25; Isa 1:15; Mik 3:4; Lk 13:25]

Waisraeli wapewa mfalme

19Lakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;[#Isa 66:4; Yer 44:16]

20ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atuongoze na kupigana vita vyetu

21Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa BWANA.

22BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawateulie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Kila mtu aende nyumbani kwake.[#Hos 13:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya