2 Wafalme 11

2 Wafalme 11

Malkia Athalia atawala Yuda

1Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme.[#2 Nya 22:10; 2 Fal 8:26]

2Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa.[#11:2 Au, Yoramu.]

3Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa BWANA, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi.[#2 Nya 22:12; Zab 12:8]

Yehoyada ampaka mafuta mtoto Yoashi

4Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya BWANA; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa BWANA, akawaonesha huyo mwana wa mfalme.[#2 Nya 23:1]

5Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoshika zamu siku ya sabato, mtalinda kasri ya mfalme;[#1 Nya 9:25]

6na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo ndivyo mtalinda kasri, kuzuia watu wasiingie.

7Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya BWANA kumzunguka mfalme.

8Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia.

9Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani.[#2 Nya 23:8]

10Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa BWANA.[#1 Sam 21:9; 2 Sam 8:7; 1 Nya 26:26,27; 2 Nya 23:9,10]

11Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kulia ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote.

12Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, Mfalme na aishi.[#Kut 25:16; Kum 17:14; Zab 19:7; 78:5; Isa 8:16; 1 Sam 10:24]

Kifo cha Athalia

13Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa BWANA;[#2 Nya 23:12]

14akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Uhaini! Uhaini![#2 Fal 23:3; 2 Nya 6:13; 34:31; 1 Fal 1:39; Mit 29:2; Mt 21:9; Lk 19:37; Ufu 19:1-7; 1 Fal 18:17,18; 2 Fal 9:23]

15Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye yeyote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa BWANA.

16Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko.[#Mwa 9:6; Kut 21:12,14; Law 24:17; Hes 35:30,31; Amu 1:7; 1 Sam 15:33; Mit 11:31; Isa 3:11; Mt 26:52; Yak 2:13; Ufu 13:10]

17Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya BWANA na mfalme na watu, ili wawe watu wa BWANA; tena kati ya mfalme na watu.[#Kum 5:2,3; 29:1; 2 Fal 23:3; Yer 11:3,6; 1 Sam 10:25; 2 Sam 5:3]

18Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunjavunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka walinzi wa nyumba ya BWANA.[#2 Fal 10:26; 2 Nya 23:17,18; Kut 32:20; Kum 7:5; 12:3; Amu 6:25,28; 1 Fal 15:12,13; 2 Nya 23:17]

19Akawatwaa wakuu wa mamia, na Wakari, na walinzi, na watu wote wa nchi; wakamleta mfalme kushuka nyumbani mwa BWANA, wakaja kwa njia ya mlango wa walinzi mpaka nyumba ya mfalme. Naye akakaa katika kiti cha enzi cha wafalme.

20Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia.[#Mit 11:10]

Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme.

21Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.[#11:21 Au, Yehoashi.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya