The chat will start when you send the first message.
1Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo.
2Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.[#Yud 1:2]
3Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.[#1 Pet 2:9]
4Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa kutoka kwa uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.
5Naam, na kwa sababu iyo hiyo jitahidini sana ili katika imani yenu mtie na wema, na katika wema wenu maarifa,[#Gal 5:6,22; Yud 1:3]
6na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu subira, na katika subira yenu utauwa,
7na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.[#Gal 6:10]
8Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.[#1 Yoh 2:9,11]
10Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.
11Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.[#Yn 3:5; 10:7]
12Kwa hiyo nitakuwa tayari kuwakumbusha hayo siku zote, ijapokuwa mnayajua na kuthibitishwa katika kweli mliyo nayo.[#Yud 1:5]
13Nami naona ni haki, maadamu nipo mimi katika maskani hii, kuwaamsha kwa kuwakumbusha.[#2 Kor 5:1; #1:13 katika Kigiriki ni ‘hema’.]
14Nikijua kwamba kule kuwekea mbali maskani yangu kwaja upesi, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyonionesha.[#Yn 21:18,19]
15Lakini nitajitahidi, ili kila wakati baada ya kufariki kwangu mpate kuyakumbuka mambo hayo.
16Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake.
17Maana alipata heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.[#Mt 17:1-5; Mk 9:2-7; Lk 9:28-35]
18Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.
19Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa iangazayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.
20Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika Maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu.
21Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.[#2 Tim 3:16,17]