The chat will start when you send the first message.
1Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria.[#Amu 6:33; 1 Sam 29:1]
2Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake.[#Mwa 3:6; Kut 20:17; Kum 5:21; Hab 2:9; Lk 12:15; 1 Tim 6:9,10; Yak 1:14,15; 1 Yoh 2:16; 1 Sam 8:14]
3Nabothi akamwambia Ahabu, BWANA apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu.[#Law 25:23; Hes 36:7; Eze 46:18]
4Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.
5Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula?
6Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu.
7Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.[#1 Sam 8:14; Yer 6:7; Mik 2:1; 7:3]
8Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia mhuri wake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi.
9Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamketishe Nabothi juu mbele ya watu,
10mkawaketishe watu wawili, watu walaghai, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.[#Kum 13:13; Amu 19:22; 1 Sam 2:12; 2 Sam 20:1; 23:6; 2 Kor 6:15; Kut 22:28; Law 24:15,16; Mdo 6:11; Law 24:14]
11Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea.
12Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu.[#Ayu 15:34; 34:30; Mit 11:9; 29:12; Isa 9:16,17; 32:6,7; 1 Tim 4:2]
13Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa.[#Hes 15:36; Yos 7:24; 2 Nya 24:21; Mk 15:20; Mdo 7:58,59; Ebr 11:37]
14Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.
15Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hayuko hai, lakini amekufa.
16Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, aliteremkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki.
17Neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema,[#Zab 9:12]
18Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki.[#1 Fal 13:32; 2 Nya 22:9]
19Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.[#Mwa 4:9-11; 2 Sam 12:9; 1 Fal 22:38]
20Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA.[#1 Fal 18:17; Isa 29:21; Amo 5:10; 2 Fal 17:17; Rum 7:14]
21Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli.[#1 Fal 14:10; Kum 32:35; 2 Fal 9:8; Zab 94:1-23; 1 Sam 25:22]
22Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli.[#1 Fal 15:29; 16:3,11]
23Tena BWANA alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.[#2 Fal 9:36; Zab 7:16; 9:15,16]
24Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla.[#1 Fal 14:11; 16:4]
25(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea.[#1 Fal 16:30,31; 11:1,4; Mwa 6:2-5]
26Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)[#Mwa 15:16; 2 Fal 21:11]
27Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.[#Mwa 37:34]
28Neno la BWANA likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,
29Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.[#Zab 51:17; 78:34-37; 2 Fal 9:25]