The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa mia moja na sitini Iskanda Epifani, mwana wa Antioko, alipanda akashika Tolemaisi, nao wakamkaribisha, akajitawaza huko.
2Mfalme Demetrio aliposikia hayo, alikusanya jeshi kubwa sana akatoka kupigana naye.
3Demetrio akampelekea Yonathani barua yenye maneno ya amani na ya kumbembeleza,
4maana alisema, Tutangulie sisi kufanya mapatano na Yonathani, kabla hajawahi kupatana na Iskanda juu yetu.
5Maana atayakumbuka mambo mabaya tuliyotenda juu yake, na juu ya ndugu zake na taifa lake.
6Akampa mamlaka ya kuwaajiri askari na kuwapa silaha, na kupigana upande wake kwa urafiki. Akaagiza apewe wale wadhamini waliokuwako ngomeni.
7Yonathani akaenda Yerusalemu akazisoma zile barua masikioni mwa watu wote, hata wale waliokaa ngomeni.
8Nao waliogopa sana waliposikia ya kuwa mfalme amempa mamlaka ya kuwaajiri askari.
9Basi, wale wa ngomeni walimtolea Yonathani wale wadhamini, akawarudisha kwa wazazi wao.
10Ndipo Yonathani akafanya makao yake Yerusalemu akaanza kuujenga mji na kuutengeneza.
11Aliwaamuru watu wa kazi wazijenge kuta na kuuzungushia mlima Sayuni mawe yaliyochongwa ili kuulinda, wakafanya hivyo.
12Nao wageni waliokuwamo katika ngome zilizojengwa na Bakide walikimbia;
13kila mtu akaacha mahali pake akarudi kwao.
14Ila katika Bethsura tu walibaki wengine waliokuwa wameiasi sheria na amri, maana mji huo ulikuwa kimbilio lao.
15Mfalme Iskanda akasikia habari za mambo Demetrio aliyomwahidia Yonathani. Akaelezwa habari za vita vyake, na matendo ya ushujaa waliyoyatenda yeye na ndugu zake, na mambo magumu waliyoyastahimili.
16Akasema, Je, tutapata wapi mtu mwingine kama huyu? Na kumfanye rafiki yetu na mshirika wetu.
17Akaandika barua akampelekea akisema:
18Mfalme Iskanda kwa ndugu yake Yonathani, salamu.
19Tumesikia habari zako, kwamba u mtu shujaa astahiliye kuwa rafiki yetu.
20Basi, tumekuweka tangu leo uwe kuhani mkuu wa taifa lenu, ukaitwe Rafiki wa Mfalme (akampelekea vazi la urujuani na taji la dhahabu). Ujiweke upande wetu na kudumu kuwa rafiki yetu.
21Yonathani akayavaa mavazi matakatifu sikukuu ya vibanda katika mwezi wa saba. Aliwaajiri askari na kuwapatia silaha kwa wingi sana.
22Demetrio aliposikia hayo alifadhaika, akasema,
23Tumefanyaje sisi! Iskanda ametushinda katika kufanya urafiki na Wayahudi ili kujiimarisha.
24Nami pia nitawaandikia maneno ya kuwapa tumaini na kuwabembeleza, na kuwaahidia vipaji, ili wajiweke upande wangu.
25Akawaandikia hivi:
26Mfalme Demetrio kwa taifa la Wayahudi, salamu. Tulifurahi kusikia ya kuwa umeyashika maagano yenu na kudumu katika urafiki wenu kwetu, wala hamkujiunga na adui zetu.
27Basi, dumuni kuwa waaminifu kwetu, nasi tutawatuza vema kwa mambo mema mnayotufanyia.
28Tutawaachilieni mambo mengi na kuwapeni zawadi.
29Na kwa sasa nawaachilia ninyi na Wayahudi wote kodi ya kichwa na kodi ya chumvi na yale malipo yatolewayo kwa mfalme.
30Hata ile theluthi ya mbegu na nusu ya matunda iliyo haki yangu, naiacha kabisa tangu leo, nisiidai kwa nchi ya Yuda wala kwa ile mitaa mitatu iliyounganishwa nayo kutoka Samaria na Galilaya.[#1 Mak 11:34]
31Yerusalemu iwe takatifu na huru, pamoja na mipaka yake, zaka zake, na ada zake.
32Aidha, naiacha mamlaka yangu juu ya ngome ya Yerusalemu na kuikabidhi kwa kuhani mkuu ili aweke watu aliowachagua mwenyewe kuilinda.
33Aidha, kila Myahudi aliyechukuliwa mateka kutoka nchi ya Uyahudi kwenye sehemu yoyote ya milki yangu namweka huru bila fidia; wala watu wasitozwe kodi ya ng'ombe.
34Sikukuu zote, na siku za Sabato na za mwezi mpya, na siku za mikutano mikuu (siku tatu kabla ya sikukuu na siku tatu baada yake) ziwe siku za uhuru na kuachiliwa kwa Wayahudi wote wa milki yangu.
35Hakuna ruhusa kwa mtu yeyote kuwatoza kitu au kuwasumbua kwa jambo lolote.
36Wayahudi wapatao elfu thelathini waandikwe katika kazi za mfalme, na wapewe riziki zao na mshahara kama inavyowapasa askari wa mfalme.
37Wengine wao wawekwe katika ngome kubwa na mfalme, na wengine juu ya mambo ya mfalme yatakayo uaminifu. Viongozi wao na wenye amri juu yao wachaguliwe miongoni mwao wenyewe. Nao wazifuate amri zao wenyewe, kama mfalme alivyoamuru katika nchi ya Yuda.
38Na kwa habari za ile mitaa mitatu iliyounganishwa na Uyahudi kutoka nchi ya Samaria, ihesabiwe kuwa pamoja na Uyahudi, yote iwe chini ya mamlaka ya mtu mmoja, wasitii amri ya mtu yeyote ila ya kuhani mkuu tu.
39Tolemaisi na mipaka yake nimetoa zawadi kwa patakatifu huko Yerusalemu kwa gharama za patakatifu.
40Nami nitatoa shekeli elfu kumi na tano za fedha kila mwaka, katika hesabu ya fedha za mfalme, kutoka mahali pa kufaa.
41Na fedha inayobaki katika ile hesabu iliyolipwa na watumishi wangu katika miaka iliyopita, tangu sasa wataitoa kwa huduma ya patakatifu.
42Zaidi ya hayo, zile shekeli elfu tano za fedha walizozoea kuzitoza katika ada za patakatifu kila mwaka zimeachiliwa pia, kwa sababu fedha hiyo yawahusu makuhani wanaofanya huduma.
43Yeyote atakayepakimbilia patakatifu katika Yerusalemu, au nyua zake, kwa sababu anadaiwa fedha na mfalme au kwa sababu ya neno lingine lolote, ataachiliwa pamoja na mali yoyote aliyo nayo katika milki yangu.
44Gharama za kujenga na kutengeneza kazi za patakatifu zitatoka katika hazina ya mfalme.
45Gharama za kuzijenga kuta za Yerusalemu pia na kuzitia nguvu, na za kujenga kuta katika Uyahudi, zitatoka katika hazina ya mfalme.
46Yonathani na watu wake walipoyasikia maneno hayo hawakuyasadiki wala kuyakubali, kwa kuwa waliyakumbuka mabaya makubwa aliyoyafanya katika Israeli na mateso makali aliyowatesa.
47Kwa hiyo walimpendelea Iskanda, maana yeye alikuwa wa kwanza kuwapa maneno ya amani, wakadumu kuwa rafiki zake sikuzote.
48Mfalme Iskanda akaunda jeshi kubwa akajipanga juu ya Demetrio,
49nao wale wafalme wawili walipigana, hata jeshi la Iskanda lilikimbia.
50Demetrio akamfuatia akamshinda, akahimiza mapigano mpaka jua limekuchwa. Naye Demetrio alikufa siku ile.
51Iskanda akapeleka wajumbe kwa Tolemayo, mfalme wa Misri, kusema hivi:
52Sasa nimeurudia ufalme wangu! Nimeketi katika kiti cha enzi cha baba zangu na kumiliki, maana nimemshinda Demetrio na kujitwalia nchi yake.
53Naam, nilipigana naye nikamshinda yeye na jeshi lake, nikakaa katika kiti cha enzi cha ufalme wake.
54Basi, sasa tufanye urafiki; unipe binti yako awe mke wangu, ili niwe mkwe wako, nami nitakupa wewe na yeye pia mahari iliyo stahili yenu.
55Mfalme Tolemayo akajibu: Heri siku uliyoirudia nchi ya baba zako na kuketi katika kiti cha enzi cha ufalme wao.
56Nitakufanyia ulivyoandika, lakini tukutane Tolemaisi ili tuonane, nami nitakuwa mkwe wako kama ulivyotaka.
57Basi, Tolemayo na binti yake Kleopatra walitoka Misri wakafika Tolemaisi katika mwaka wa mia moja sitini na mbili,
58akamwoza binti yake Kleopatra, akaishangilia arusi yake Tolemaisi kwa sherehe kuu, kama ilivyo desturi ya wafalme.
59Kisha mfalme Iskanda alimwandikia Yonathani kutaka aje wakutane.
60Akaenda Tolemaisi kwa fahari, akaonana na wale wafalme wawili akawapa fedha na dhahabu na zawadi nyingi, wao na rafiki zao pia, akapata kibali machoni pao.
61Waisraeli wengine wenye matata, watu walioiasi sheria, walikusanyika pale ili kumshtaki, lakini mfalme hakuwaangalia.
62Bali alitoa amri wamvue Yonathani nguo zake na kumvika mavazi ya urujuani, wakafanya hivyo.
63Mfalme akamketisha mkononi pake, akawaambia wakuu wake, mpelekeni hata katikati ya mji. Katangazeni ya kuwa hakuna ruhusa mtu yeyote amshtaki kwa habari yoyote, wala asimwudhi kwa sababu yoyote.
64Basi, wale waliokuja kumshtaki walipoona jinsi alivyotukuzwa kwa maneno ya mpiga mbiu, na kuvikwa urujuani, walikimbia wote.
65Mfalme akamfanyia heshima, akamwandika katika rafiki zake walio bora, akamfanya jemadari na Mkuu wa Mkoa.
66Yonathani akarejea Yerusalemu kwa amani na furaha.
67Katika mwaka wa mia moja sitini na tano, Demetrio, mwana wa Demetrio, alifika nchi ya baba zake kutoka Krete.
68Mfalme Iskanda aliposikia habari hiyo alifadhaika sana akarudia Antiokia.
69Demetrio akamwagiza Apolonio, ambaye wakati ule alikuwa juu ya Koele-Shamu, akaunda jeshi kubwa. Alipiga kambi yake karibu na Yamnia, akapeleka habari kwa Yonathani kuhani mkuu.
70Kusema, Wewe peke yako umejipanga juu yetu, na kwa sababu yako nimekuwa dhihaka na lawama. Kwa nini unatusimanga milimani?
71Kama unawatumainia askari zako, basi shukeni kwetu uwandani. Tupimane nguvu huko, maana nguvu ya miji iko kwangu.
72Uliza, ujue mimi ni nani, na wale wanaotusaidia ni nani, nao watakuambia, Mguu wako hauwezi kusimama mbele yetu, maana baba zako wameshindwa mara mbili katika nchi yao wenyewe.
73Hutaweza kushindana na wapanda farasi na jeshi la namna hii katika nchi tambarare isiyo na jiwe wala kokoto, wala mahali pa kukimbilia.
74Yonathani alipoyasikia maneno hayo ya Apolonio aliingiwa na hasira. Akachagua watu elfu kumi akaondoka Yerusalemu, naye Simoni nduguye alikwenda naye kumsaidia.
75Akapiga kambi kuelekea Yafa, watu wa mjini wakamfungia milango, maana Apolonio alikuwa ameweka askari walinzi humo.
76Wakapigana hata watu wa mjini walishikwa na hofu wakaifungua milango; Yonathani akautwaa Yafa.
77Apolonio aliposikia, aliunda kikosi cha wapanda farasi elfu tatu, na jeshi kubwa la askari, akaenda Ashdodi kana kwamba anasafiri tu; lakini katika kwenda mbele aliuelekea uwanda wa chini, maana aliutumainia wingi wa wapanda farasi wake.
78Akamfuatia Yonathani hata Ashdodi majeshi yakapambana vitani.
79Apolonio alikuwa ameacha wapanda farasi elfu moja huko nyuma kwa siri,
80lakini Yonathani alitambua ya kuwa pana maoteo nyuma yake. Wakalizunguka jeshi lake na kuwatupia mishale tangu asubuhi mpaka jioni,
81lakini watu walisimama imara, kama Yonathani alivyoamuru, hata farasi walichoka.
82Ndipo Simoni akajitokeza na jeshi lake, akawashambulia askari wa miguu, maana wapanda farasi walikuwa hawana nguvu tena; akawashinda, wakakimbia.
83Nao wapanda farasi walitawanyika uwandani, wakakimbilia Ashdodi, wakaingia katika Beth-dagoni, nyumba ya mungu wao, ili kujiokoa.
84Yonathani akatia moto Ashdodi na viunga vyake, akateka nyara; akaliteketeza hekalu la Dagoni na wote waliolikimbilia.
85Waliouawa kwa upanga pamoja na wao waliochomwa moto walikuwa kama watu elfu nane.
86Yonathani akaondoka hapo akaenda Ashkeloni, watu wa mjini wakatoka kumlaki kwa sherehe kubwa.
87Baada ya hayo, Yonathani akarudi Yerusalemu na watu wake na mateka mengi.
88Mfalme Iskanda alipopata habari hizo alimfanyia Yonathani heshima nyingi zaidi,
89akimpelekea bizimu ya dhahabu, ambayo kwa kawaida hupewa jamaa za mfalme tu. Akampa Ekroni na mipaka yake yote iwe milki yake.