The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa mia moja sabini na mbili mfalme Demetrio alikusanya majeshi yake akaenda Umedi kujipatia msaada ili apigane na Trifoni.
2Arsake, mfalme wa Uajemi na Umedi, aliposikia kwamba Demetrio ameingia mipakani mwake, alituma kamanda mmoja amkamate mzima.
3Akaenda akalipiga jeshi la Demetrio, akamkamata, akamleta kwa Arsake, naye akamtia kifungoni.
4Nchi ya Yuda ikakaa kwa amani siku zote za Simoni. Alilitafutia taifa mema, hata utawala wake na sifa yake iliwafurahisha siku zake zote.
5Jambo moja lililompatia sifa kubwa lilikuwa kuitwaa Yafa iwe bandari, na kuifanya kuwa mahali pa kuviingilia visiwa vya baharini.
6Aliipanua mipaka ya taifa lake
Na kuitawala nchi;
7Alikusanya mateka mengi,
Akamiliki Gazara, Bethsura na Ngomeni,
Akaitakasa ngome katika unajisi wake,
Wala hakuna mtu wa kumpinga.
8Walilima ardhi kwa amani,
Nchi ikatoa mazao yake,
Na miti ya bondeni matunda yake.
9Wazee waliketi njiani
Wakizungumza mambo mema ya kale,
Na vijana walijivika mavazi matukufu ya vita.
10Aliipatia miji chakula,
Na kutoa kwa wingi silaha za vita.
Sifa zake zilivuma hata miisho ya ulimwengu.
11Alifanya amani katika nchi,
Israeli ikafurahi sana;
12Kila mtu alikaa chini ya mzabibu wake na mtini wake,
Wala hakuna wa kuwaogofya;
13Hakuna aliyebaki katika nchi kupigana nao;
Siku zile wafalme waliharibiwa.
14Alitia nguvu walioonewa katika watu wake.
Aliichungua sheria,
Akawaondoa waasi na waovu.
15Alipatukuza patakatifu,
Akaviongeza vyombo vya hekalu.
16Habari za kufa kwake Yonathani zilipofika Rumi, na hata Sparta, walisikitika sana.
17Na mara waliposikia ya kuwa nduguye Simoni amekuwa kuhani mkuu mahali pake, akiitawala ile nchi na miji yake,
18walimwandikia juu ya vibao vya shaba kuyafanya tena yale mapatano ya urafiki ambayo walikuwa wamewathibitishia Yuda na Yonathani, ndugu zake;[#1 Mak 8:22]
19yakasomwa mbele ya mkutano Yerusalemu.
20Hii ndiyo nakala ya barua waliyoileta Wasparta: Watawala wa Wasparta, na mji, kwa kuhani mkuu Simoni, na kwa wazee na makuhani na Wayahudi wengine, ndugu zetu, salamu.
21Wajumbe mliowatuma kwa watu wetu walituarifu habari za sifa yenu na utukufu wenu, nasi tulikufurahia kuja kwao.
22Tumeyaandika maneno yao katika taarifa za mji kama hivi: Numenio mwana wa Antioko na Antipateri mwana wa Yasoni, wajumbe wa Wayahudi, wamekuja kwetu ili kufanya tena mapatano ya urafiki nasi.
23Iliwapendeza watu kuwakaribisha watu hawa kwa heshima, na kutia nakala ya maneno yao katika taarifa za mji ili Wasparta wawe na kumbukumbu; wakaandika nakala ya maneno hayo kwa Simoni, kuhani mkuu.
24Baada ya hayo, Simoni alimpeleka Numenio aende Rumi na ngao kubwa ya dhahabu ya uzani wa ratili elfu moja, ili kuuthibitisha ushirika wao.
25Watu walipoyasikia hayo, walisema, Twawezaje kumshukuru Simoni na wanawe?
26Yeye na ndugu zake na nyumba ya baba yake wametenda kwa ushujaa. Walifukuzia mbali adui wa Israeli, wakaipatia Israeli uhuru. Wakaandika juu ya vibao vya shaba, wakaviweka katika nguzo juu ya mlima Sayuni.
27Hii ndiyo nakala ya maandishi: Siku ya kumi na nane ya Eluli, mwaka wa mia moja sabini na mbili, ndio mwaka wa tatu wa Simoni, kuhani mkuu, jemadari wa Israeli,
28katika mkutano mkuu wa makuhani wa watu, na wakuu wa taifa, na wazee wa nchi, shauri hili lilikatwa:
29Mara nyingi, wakati wa vita katika nchi, Simoni, mwana wa Matathia, wa ukoo wa Yoaribu, na nduguze, walijihatarisha nafsi zao wakiwapinga adui za taifa lao, ili patakatifu na sheria isidhuriwe; wakalikuza taifa lao kwa utukufu mwingi.
30Yonathani aliliunganisha taifa kwa umoja, akawa kuhani mkuu wao, akaga dunia.
31Adui zao walipokusudia kuiingilia nchi yao ili kuiharibu kabisa, wakainyosha mikono yao juu ya patakatifu,
32Simoni aliondoka akalipigania taifa lake. Alitumia mali yake nyingi katika kuwapatia silaha watu hodari wa taifa lake, na kuwapa ijara yao.
33Akaiimarisha miji ya Uyahudi, na Bethsura mipakani mwa Uyahudi, silaha za adui zilipowekwa akiba zamani, akaweka kikosi cha Wayahudi kuilinda.
34Akaiimarisha Yafa, iliyopo pwani, na Gazara katika mipaka ya Ashdodi, walipokaa adui zamani, akaweka Wayahudi huko, pamoja na vifaa vyote walivyovihitaji.
35Watu walipouona uaminifu wa Simoni, na utukufu waliolitafutia taifa lake, walimfanya kiongozi wao na kuhani mkuu, kwa sababu ya hayo yote aliyoyafanya, na ya haki na uaminifu aliokuwa nao daima kwa taifa lake, na kwa sababu alijitahidi kwa kila njia kuwakuza watu wake.
36Katika siku zake mambo yalifanikiwa mikononi mwake na mataifa waliondolewa katika nchi yao. Nao pia waliondolewa waliokuwamo katika mji wa Daudi, Yerusalemu, ambao walikuwa wamejifanyia ngome na kutoka humo kila mara kutia unajisi mipaka ya patakatifu na kuuharibu usafi wake.
37Akawakalisha Wayahudi ndani yake, akaiimarisha kwa ajili ya usalama wa nchi na mji, akaongeza urefu wa kuta za Yerusalemu.
38Kwa sababu ya mambo hayo mfalme Demetrio alimthibitisha katika cheo chake cha kuhani mkuu,
39akamfanya mmoja wa rafiki zake, akamfanyia heshima nyingi,
40kwa sababu alisikia kwamba Wayahudi wametajwa na Warumi kuwa rafiki na washarika na ndugu, hata wajumbe wa Simoni walipokewa kwa heshima kuu.
41Kwa hiyo, Wayahudi na makuhani waliona vema Simoni awe kiongozi wao na kuhani mkuu daima, mpaka nabii wa kweli atokee.
42Tena, awe jemadari wa kuwaagiza kazi zao, awe juu ya nchi na juu ya silaha na juu ya ngome.
43Iwe kazi yake kupatunza patakatifu, na wote wamtii, na taarifa zote za nchi ziandikwe kwa jina lake. Naye avikwe urujuani na kuvaa dhahabu.
44Wala isiwe halali mtu yeyote miongoni mwa watu au miongoni mwa makuhani adharau jambo lolote katika hayo, wala kukaidi amri yake yoyote, wala kufanya mkutano pasipo idhini yake, wala kuvaa urujuani au kujifungia bizimu ya dhahabu.
45Na yeyote atakayokaidi mambo hayo au kuyadharau atakuwa na hatia.
46Watu wote waliona vema Simoni aamriwe mambo hayo.
47Simoni akaitikia, akakubali kuishika huduma ya kuhani mkuu, kuwa jemadari na mtawala wa Wayahudi na wa makuhani, na kuyasimamia yote.
48Wakaamuru hayo yaandikwe juu ya vibao vya shaba, na viwekwe katika ua wa patakatifu, mahali pa kuonekana na wote,
49tena, nakala zake zitiwe katika chumba cha hazina, ili Simoni na wanawe wawe nazo.