The chat will start when you send the first message.
1Antioko, mwana wa mfalme Demetrio, alipeleka barua toka visiwa vya baharini kwa Simoni, kuhani mkuu na mtawala wa Wayahudi, na kwa taifa lote,
2nayo iliandikwa hivi: Mfalme Antioko kwa Simoni, kuhani mkuu na mtawala, na kwa taifa la Wayahudi, salamu.
3Watu kadha wa kadha, waasi, wameushika ufalme wa baba zetu, nami nataka kuudai ufalme ili niufanye kama ulivyokuwa kwanza. Nimeajiri jeshi kubwa la askari wa mshahara, na kuweka tayari merikebu za vita.
4Nia yangu ni kuingia katika nchi ili niwafuatie wale walioiharibu nchi yetu na kuteka miji mingi ya ufalme.
5Basi, sasa nakuthibitishia idhini zote zilizotolewa na wafalme walionitangulia; tena, nakuachilia mambo mengine yoyote waliyokuachilia.
6Nakupa mamlaka ya kuchapa fedha za nchi yako kwa chapa chako mwenyewe.
7Yerusalemu na patakatifu pawe huru. Silaha zile ulizozitengeneza, na ngome ulizozijenga na kushika, ukae nazo.
8Madeni yote unayodaiwa na mfalme, na yote yatakayodaiwa, na yasamehewe kwenu, tangu sasa na sikuzote.
9Zaidi ya hayo, tutakapoushika tena ufalme wetu, tutakukuza sana, na taifa lako na patakatifu, ili ukuu wako ujulikane duniani kote.
10Ikawa, katika mwaka wa mia moja sabini na nne, Antioko aliingia katika nchi ya baba zake, na askari wote walimwendea, hata ni wachache tu waliobaki kwa Trifoni.
11Antioko akamfukuza Trifoni, naye alikimbia kwa njia ya pwani akafika Dori,
12maana alijua ya kuwa anasongwa na mambo mabaya mengi, na askari wake wamemwacha.
13Antioko akajipanga mbele ya Dori, pamoja na askari elfu mia moja na ishirini na wapanda farasi elfu nane.
14Aliuzunguka mji pande zote, na merikebu zilisaidia kwa kuupiga toka baharini. Aliusonga mji kabisa, penye nchi kavu na bahari, asimwache mtu atoke wala kuingia.
15Huko nyuma Numenio na wenzake walirudi kutoka Rumi wenye barua kwa wafalme na kwa nchi zenye maneno haya:[#1 Mak 12:16]
16Lukio, balozi wa Warumi, kwa mfalme Tolemayo, salamu.
17Wajumbe wa Wayahudi waliotumwa na kuhani mkuu Simoni na taifa la Wayahudi wamefika kwetu, kama rafiki na washirika, ili kufanya tena yale mapatano ya urafiki ya zamani,
18nao wameleta ngao ya dhahabu ya uzani wa ratili elfu moja.
19Tumekata shauri, basi, kuandika kwa wafalme na kwa nchi wasiwafanyie dhara lolote, wala kupigana nao na nchi yao na miji yao, wala kufanya mapatano na wale wanaopigana nao.
20Tumeona vema kuipokea ile ngao.
21Kwa hiyo, kama waasi wowote wametoroka nchi yao na kukimbilia kwenu, warudisheni kwa Simoni, kuhani mkuu, awaadhibu kwa sheria yao.
22Maneno yayo hayo yaliandikwa kwa mfalme Demetrio, na Atale, na Arathe na Arsake,
23na kwa nchi zote; na kwa Sampsame na kwa Wasparta, na kwa nchi za Delo, Mindo, Sikyoni, Karia, Samo, Pamfilia, Likia, Halikanaso, Rodo, Faseli, Ko, Side, Arado, Gotina, Nido, Kipro na Kirene.
24Wakapeleka nakili yake kwa Simoni, kuhani mkuu.
25Mfalme Antioko aliihusuru Dori mara ya pili, akiishambulia kwa askari wake tena na tena na kutengeneza mitambo ya vita; akamzuia Trifoni asitoke wala kuingia.
26Simoni akampelekea watu wateule elfu mbili wa kumpigania, pamoja na fedha na dhahabu na silaha tele.
27Lakini hakukubali kuvipokea, wala hakujali mapatano yao ya zamani, bali alijitenga naye.
28Akamtuma Athenobio, mmoja wa rafiki zake, afike kwake na kumwambia, Ninyi mnashika Yafa na Garaza, na ngome iliyoko Yerusalemu, miji ya ufalme wangu.
29Mmeharibu mipaka yake na kufanya hasara nyingi katika ufalme wangu. Mmejitwalia mahali pengi katika ufalme wangu.
30Basi, sasa, rudisheni ile miji mliyoitwaa, na kodi ya mahali mliposhika nje ya mipaka ya Uyahudi,
31au, badala yake, nipeni talanta mia tano za fedha, pamoja na talanta nyingine mia tano kwa ajili ya hasara mliyofanya, na kwa kodi ya miji; ama sivyo, tutawajieni tupigane.
32Athenobio, rafiki wa mfalme alipofika Yerusalemu na kuuona utukufu wa Simoni, na kabati yenye vyombo vya dhahabu na fedha, na fahari yake, alishangaa sana. Akamwarifu maneno ya mfalme.
33Simoni akajibu akamwambia, Sisi hatukutwaa nchi ya watu, wala hatumiliki ardhi ya watu, ila urithi wa baba zetu tu, ambao kwa muda ulishikwa na adui zetu bila haki.
34Basi, kwa kuwa tumepata nafasi ya kufaa, tunaushikilia urithi wa baba zetu.
35Hata hivi, kwa habari za Yafa na Gazara, mnazozidai, tutatoa talanta mia moja kwa ajili yake ingawa zimepatia watu wetu na nchi yetu hasara nyingi.
36Hakujibu neno, lakini alirudi kwa mfalme na hasira nyingi, akamwarifu maneno hayo, akamsimulia habari za fahari ya Simoni, na mambo yote aliyoyaona. Mfalme akakasirika sana.
37Trifoni alipakia katika merikebu akakimbilia Orthosia.
38Mfalme akamweka Kendebayo awe jemadari mkuu wa pwani, akampa askari na wapanda farasi.
39Akamwagiza apige kambi mpakani mwa Uyahudi; tena, ajenge Kedroni na kuiimarisha milango yake na kupigana na watu wake, hali mfalme mwenyewe amfuatie Trifoni.
40Kendebayo alifika Yamnia akaanza kuchokoza watu kwa kuingilia Uyahudi kila mara akikamata watu na kuwaua.
41Akajenga Kedroni, akaweka wapanda farasi huko na vikosi vya askari, ili wazishambulie njia za Uyahudi kama mfalme alivyoagiza.