1 Wamakabayo 3

1 Wamakabayo 3

YUDA MAKABAYO KIONGOZI WA WAYAHUDI (166-160 K.K.)

Yuda Makabayo asifiwa

1Na mwanawe Yuda, aliyeitwa Makabayo,

aliondokea mahali pake.

2Ndugu zake wote wakimsaidia,

Nao walioshikamana na baba yake

Wakavipiga vita vya Israeli kwa furaha.

3Akaongeza utukufu wa watu wake,

Akajivika dirii kifuani kama shujaa,

Na kujifunga silaha za vita.

Alilipanga jeshi lake kwa vita

Na kulilinda kwa upanga wake.

4Alikuwa kama simba kwa matendo yake,

Kama mwana simba akinguruma akitaka mawindo.

5Aliwafuatia waasi akiwatafuta,

Akawateketeza wale waliowaudhi watu wake.

6Walioasi walikufa moyo kwa hofu yake,

Watenda maovu wote walifadhaika,

Wokovu ulisitawi mikononi mwake.

7Alitia hasira wafalme wengi,

Akamfurahisha Yakobo kwa matendo yake;

Ukumbusho wake utabarikiwa milele.

8Alizungukazunguka katika miji ya Yuda

Akiwafutia mbali waovu,

Akageuza hasira mbali na Israeli.

Sifa zake zikaenea hata miisho ya dunia,

9Akakusanya pamoja wale wanaopotea.

Ushindi wa kwanza wa Yuda

10Apolonio akakusanya mataifa, pamoja na watu wengi kutoka Samaria, ili apigane na Israeli.

11Yuda akapata habari, akaenda kukutana naye, akampiga, akamwua. Watu wengi wakaanguka wametiwa jeraha za mauti, na wengine wakakimbia.

12Wakateka nyara; naye Yuda aliutwaa upanga wa Apolonio, akautumia sikuzote.

13Seroni, jemadari wa jeshi la Shamu, alisikia ya kuwa Yuda amekutanisha mkutano, jeshi la watu waaminifu na walio hodari wa vita,

14akasema, Nitalitukuza jina langu na kujipatia heshima katika ufalme kwa kupigana na Yuda na wale walioko kwake wanaoidharau amri ya mfalme.

15Na pamoja naye walikwenda jeshi kubwa la watu waovu ili wamsaidie kuwalipiza kisasi wana wa Israeli.

16Akaja karibu na mipando ya Beth-horoni, Yuda akamwendea na kikosi kidogo.

17Nao walipoliona lile jeshi kubwa likija juu yao walimwambia Yuda, Je! Sisi kundi dogo tutaweza kupigana na umati huu mkubwa wa nguvu? Nasi tumedhoofika kwa sababu hatujaonja kitu leo.

18Yuda akasema, Ni jambo rahisi watu wengi wazingirwe kwa mikono ya wachache. Kwa mbingu ni mamoja tu, kuokolewa kwa wengi au kwa wachache,

19maana kushinda vitani hakupatikani kwa wingi wa watu, ila kwa nguvu itokayo mbinguni.

20Wao wanatujia kwa wingi wa jeuri na udhalimu ili kutuharibu sisi na wake zetu na watoto wetu na kututeka.

21Lakini sisi tunayapigania maisha yetu na amri zetu.

22Yeye Mwenyewe atawafadhaisha usoni petu, basi msiwaogope.

23Akiisha kusema hayo, aliwashambulia kwa ghafla, Seroni na jeshi lake wakapondwa mbele yake.

24Wakawafuatia katika miteremko ya Beth-horoni hata uwandani chini. Wakaanguka watu kama mia nane, na waliosalia waliikimbilia nchi ya Wafilisti.

25Basi, hofu na woga uliwaangukia mataifa ya jirani kwa sababu ya Yuda na ndugu zake;

26jina lake likajulikana hata kwa mfalme, na mataifa yote walisimulia habari za vita vyake.

ANTIOKO AJIANDAA VITA NA WAAJEMI

Sera ya Antioko

27Mfalme Antioko aliposikia maneno hayo alikasirika sana. Akavikusanya vikosi vyote vya askari vya nchi yake, jeshi kubwa mno.

28Akafungua hazina yake akawapa askari wake ijara ya mwaka mzima, akawaagiza wawe tayari kwa haja yoyote.

29Akaona fedha ya hazina yake inapungua, tena kodi haipatikani sana kwa sababu ya uasi na matata aliyoingiza mwenyewe katika nchi tangu zamani.

30Akashuku kama fedha haitamtosha kama zamani kwa gharama na kwa vipawa alivyozoea kutoa kwa ukarimu – naye alikuwa mpaji kuliko wafalme waliomtangulia.

31Kwa hiyo alifadhaika sana, akakata shauri kwenda Uajemi kutoza kodi za nchi zile na kukusanya fedha nyingi.

32Akamwacha Lisia, mtu mstahiki wa ukoo wa mfalme, awe juu ya mambo ya mfalme toka mto Frati hadi mipaka ya Misri,

33na kumlea mwanawe Antioko hadi atakaporudi.

34Akamkabidhi nusu ya majeshi yake na tembo. Akamwagiza mambo yote aliyotaka yafanyike, na kwamba apeleke jeshi juu ya watu wakaao Uyahudi na katika Yerusalemu,

35ili kuwang'oa na kuivunja nguvu ya Israeli na ya mabaki ya Yerusalemu. Auondoe ukumbusho wao katika mahali pale

36na kukalisha wageni katika mipaka yao yote, akiwagawia nchi kwa kura.

37Ndipo mfalme aliitwaa ile nusu nyingine ya jeshi akaondoka Antiokia, mji wake wa kifalme, mwaka mia arubaini na saba akavuka mto Frati akazipitia nchi za juu.

GORGIA NA NIKANO WANAONGOZA JESHI LA SHAMU KUPIGANA NA WAYAHUDI

Maandalio ya Vita

38Lisia akamchagua Tolemayo mwana wa Dorimene na Nikano na Gorgia, watu hodari katika rafiki za mfalme.

39Akapeleka pamoja nao askari elfu arubaini na wapanda farasi elfu saba, ili waiendee nchi ya Uyahudi kuiharibu, kama mfalme alivyoamuru.

40Wakaondoka na jeshi lao lote, wakaja wakapiga kambi karibu na Emao katika uwanda wa chini.

41Wachuuzi wa nchi wakapata habari, wakachukua fedha na dhahabu nyingi, na pingu, wakaja kambini kusudi wawanunue Waisraeli kuwa watumwa. Majeshi ya Shamu na ya nchi ya Wafilisti wakajiunga nao.

42Yuda na ndugu zake waliona ya kuwa mabaya yameongezeka, hata majeshi wamepiga kambi katika mipaka yao. Wakaikumbuka ile amri aliyoitoa mfalme ya kuwaangamiza watu kabisa.

Mkusanyo wa Wayahudi huko Mizpa

43Wakasemezana kila mtu na mwenzake. Na tuiinue hali nyonge ya watu wetu; tuwapiganie watu wetu na mahali patakatifu.

44Watu wakakutanika pamoja ili wawe tayari kwa vita, tena wapate kusali na kuomba rehema na huruma.

45Yerusalemu ilikuwa ukiwa kama jangwa,

Hakuna watoto wake walioingia wala kutoka;

Mahali patakatifu palikanyagwa chini,

Wana wa wageni walikuwamo mjini,

Ukawa maskani ya mataifa.

Furaha iliondolewa katika Yakobo,

Sauti ya filimbi na kinubi ilikoma.

46Wakakusanyana, wakaja Mizpa, kuelekea Yerusalemu, kwa sababu Waisraeli walikuwa na mahali pa kusali huko Mizpa.

47Siku hiyo walifunga, wakajivika magunia na kujitia majivu kichwani na kurarua nguo zao.

48Wakakunjua gombo la chuo cha sheria, ambalo juu yake watu wa mataifa walikuwa wamechora taswira za sanamu zao;

49wakatoa mavazi ya makuhani, na malimbuko, na zaka, na kuwanyoa Wanadhiri waliokuwa wamezitimiza siku zao.

50Wakazililia mbingu kwa sauti kuu, wakisema, Tufanyeje na watu hawa? Tuwapeleke wapi?

51-52-53Maana mahali pako patakatifu pamekanyagwa na kutiwa unajisi, na makuhani wako wamo katika huzuni na unyonge.

54Wakazipiga tarumbeta na kulia kwa sauti kuu.

55Baada ya hayo, Yuda aliweka wakuu wa watu, viongozi wa maelfu, na viongozi wa mamia, na viongozi wa hamsini hamsini, na viongozi wa kumi kumi.

56Na watu waliokuwa wakijenga nyumba, au kataka kuoa, au wamepanda mashamba ya mizabibu, au wanaona hofu, aliwaagiza warudi kila mtu nyumbani kwake, kama ilivyoamriwa na sheria.[#Kum 20:5-8; Amu 7:3]

57Kisha jeshi lake likaondoka likapiga kambi kusini ya Emao.

58Yuda akasema, Jifungeni, mwe hodari.

59Kesho mwe tayari kupigana na mataifa waliotukusanyikia ili kutuharibu sisi na patakatifu.

60Na yatakayokuwa mapenzi ya mbinguni, ndivyo Yeye atakavyofanya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya