The chat will start when you send the first message.
1Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba.[#1 Fal 5:5]
2Sulemani akahesabu watu elfu sabini wawe wapagazi, na watu elfu themanini wawe wachonga mawe milimani, na watu elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.[#1 Fal 5:15]
3Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi.[#1 Nya 14:1; #2:3 Au, Huramu.]
4Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli.[#Kut 30:7; 25:30; Law 24:8; Mt 12:4; Kut 29:38-42; Hes 28:3]
5Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote.[#Kut 15:11; 1 Nya 16:25; Zab 86:8,9; 135:5; Yer 10:6]
6Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya pahali pa kufukizia mafusho mbele zake?[#1 Fal 8:27; 2 Nya 6:18; Isa 66:1]
7Unitumie mtu stadi wa kuchonga dhahabu, fedha, shaba na chuma, na wa nguo za urujuani, nyekundu na samawati, ajuaye kutia nakshi, awe mmoja wa mastadi walioko pamoja nami Yuda na Yerusalemu ambao aliwaweka baba yangu Daudi.[#1 Nya 22:15]
8Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako,[#1 Fal 5:6; 19:11]
9ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.
10Na tazama, nitawapa watumishi wako, wachongaji wakatao miti, kori elfu ishirini za ngano iliyopondwa, na kori elfu ishirini za shayiri, na bathi elfu ishirini za mvinyo na bathi elfu ishirini za mafuta.[#1 Fal 5:11; #2:10 Kori ni kipimo cha Kiebrania, kama lita 220 ni sawa na pipa moja.; #2:10 Ni kipimo cha Kiebrania kama lita 22 (au galoni 5) ni sawa na efa moja.]
11Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akajibu kwa waraka, aliomtumia Sulemani, Ni kwa sababu BWANA awapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme juu yao.[#Kum 33:3; 1 Fal 10:9]
12Hiramu akasema tena, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, aliyezifanya mbingu na nchi, ambaye amempa mfalme Daudi mwana wa hekima, mwenye busara na akili, ili amjengee BWANA nyumba, na kasri kwa ufalme wake.[#1 Fal 5:7; Mwa 1:1; Zab 33:6; 102:25; Mdo 4:24; Ufu 10:6]
13Na sasa nimemtuma mtu stadi, mwenye akili, yaani, Hiramu baba yangu,[#2:13 Au, Huramu.]
14mwana wa mwanamke wa kabila la Dani, na babaye alikuwa mkazi wa Tiro, yeye ni bingwa wa kutumia dhahabu, fedha, shaba, chuma, mawe na mti; na wa nguo za urujuani, samawati, nyekundu na kitani safi; tena ni stadi kwa kutia nakshi na kuchora michoro yoyote, mbunifu na kuchora chochote kufuatana na kielekezo ambacho angepewa yeye na watu wako mastadi wa bwana wangu Daudi baba yako.[#1 Fal 7:13]
15Basi sasa hiyo ngano na shayiri, mafuta na mvinyo, aliyonena bwana wangu, na wapelekewe watumishi wake;
16nasi tutakata miti katika Lebanoni, kadiri utakavyohitaji; na kukuletea tukiieleza baharini mpaka Yafa; nawe utaipeleka Yerusalemu.[#1 Fal 5:8; Yos 19:46; Mdo 9:36]
17Ndipo Sulemani akawahesabu wageni wote waliokuwamo katika nchi ya Israeli, kulingana na hesabu aliyoifanya Daudi baba yake; wakatokea elfu mia moja hamsini na tatu, na mia sita.[#1 Fal 5:13; 1 Nya 22:2; 2 Nya 8:7,8]
18Katika hao akawaweka elfu sabini wawe wapagazi na elfu themanini wawe wachonga mawe milimani, na elfu tatu na mia sita wewe wasimamizi ili wawahimize watu kazini.