2 Mambo ya Nyakati 3

2 Mambo ya Nyakati 3

Sulemani ajenga hekalu

1Ndipo Sulemani akaanza kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, juu ya mlima Moria, pale BWANA alipomtokea Daudi babaye alipotengeza mahali pale alipoagiza Daudi, katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.[#1 Fal 6:1; 1 Nya 29:19; Yn 2:19-21; 1 Kor 6:19; Mwa 22:2; 1 Nya 22:1; #3:1 Au, Ornani.]

2Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.

3Basi hivi ndivyo vipimo vya majengo ya nyumba ya Mungu alivyoviweka Sulemani. Urefu wake ulikuwa dhiraa sitini na upana wake dhiraa ishirini.[#1 Fal 6:2; #3:3 Neno ‘vipimo’ katika lugha ya Kiebrania ni ‘misingi’.; #3:3 Dhiraa tazama Kutoka 25:10.]

4Na ukumbi uliokuwa mbele yake, urefu wake ulikuwa sawa na upana wa nyumba ulikuwa dhiraa ishirini, na kimo chake mia moja na ishirini; akaufunikiza ndani kwa dhahabu safi.[#1 Fal 6:3]

5Nayo nyumba kubwa ilizungushiwa miti ya miberoshi, aliyoifunikiza kwa dhahabu safi, juu yake akaichora mitende na minyororo.[#1 Fal 6:17]

6Akaipamba nyumba kwa vito iwe na uzuri; nayo dhahabu ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.

7Tena, akaifunikiza kwa dhahabu nyumba, na boriti, na vizingiti, na kuta zake, na milango yake; akachora makerubi kutani.

8Akaifanya nyumba ya patakatifu pa patakatifu; urefu wake sawa na upana wa nyumba, ulikuwa dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa ishirini; akaifunikiza kwa dhahabu safi, ya talanta mia sita.

9Na uzani wa misumari ulikuwa shekeli hamsini za dhahabu. Alivifunika vyumba vyake ghorofani kwa dhahabu.

10Na ndani ya nyumba ya patakatifu pa patakatifu akatengeneza makerubi mawili ya kuchonga; wakayafunika kwa dhahabu.[#1 Fal 6:23]

11Na mabawa ya makerubi hayo urefu wake ulikuwa mikono ishirini; bawa moja mikono mitano, likiufikia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la pili.

12Na bawa la kerubi la pili lilikuwa mikono mitano, likiufikia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la kwanza.

13Yakaenea mabawa ya makerubi hayo dhiraa ishirini; yakasimama juu ya miguu yao, na nyuso zao ziliielekea nyumba.

14Akalifanya pazia la samawati na urujuani na nyekundu, na kitani safi, akaitengeneza makerubi.[#Kut 26:31; Mt 27:51; Ebr 9:3]

15Tena akafanya mbele ya nyumba nguzo mbili za mikono thelathini na tano kwenda juu kwake, na mataji yaliyokuwa juu yake moja moja ilikuwa mikono mitano.[#1 Fal 7:15; Yer 52:21]

16Akafanya minyororo ndani ya chumba cha ndani, akaiweka juu ya vichwa vya nguzo; akafanya makomamanga mia moja, akayaweka juu ya hiyo minyororo.

17Akazisimamisha nguzo hizo mbele ya hekalu, moja upande wa kulia, na ya pili upande wa kushoto; akaliita jina la ile ya kulia Yakini, na jina la ile ya kushoto Boazi.[#3:17 maana yake imedhaniwa kuwa ‘atathibitisha.’; #3:17 Boazi maana yake imedhaniwa kuwa Imo nguvu.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya