2 Yohana 1

2 Yohana 1

Salamu

1Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuayo ile kweli;[#1 Pet 5:1; 3 Yoh 1:1]

2kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele.

3Neema, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Ukweli na upendo

4Nilifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.

5Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.[#Yn 13:34; 15:12,17; 1 Yoh 2:7]

6Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende kwayo.

7Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.[#1 Yoh 2:18; 4:1-3]

8Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.[#Gal 4:11]

9Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.[#1 Yoh 2:23]

10Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.[#2 The 3:6; 1 Fal 13:17; 3 Yoh 1:8]

11Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu.

Salamu za mwisho

12Kwa kuwa ninayo mambo mengi, sitaki kuyaandika kwa karatasi na wino; lakini natarajia kuja kwenu, na kusema nanyi uso kwa uso, ili furaha yetu iwe imetimizwa.[#3 Yoh 1:13]

13Watoto wa dada yako aliye mteule, wakusalimu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya