The chat will start when you send the first message.
1Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema,[#Kum 16:18]
2Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha;[#2 Fal 5:6]
3basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu.
4Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama?[#2 Fal 9:24,27; Lk 14:31]
5Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako.[#Yos 9:11,24,25; 1 Fal 20:4]
6Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea.[#Ayu 21:19; Kut 20:5; Yos 7:24]
7Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli.[#1 Fal 21:21]
8Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni marundo mawili penye maingilio ya lango hata asubuhi.
9Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalimfitinia bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote?[#2 Fal 9:14,24; Hos 1:4]
10Jueni basi ya kwamba halianguki chini lolote la neno la BWANA, alilolinena BWANA juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana BWANA ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya.[#1 Sam 3:19; Zab 33:11; 119:89; Isa 14:27; 40:8; Mt 24:35; 1 Pet 1:25; 1 Fal 21:19,21,29]
11Hivyo Yehu akawaua wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja.[#1 Fal 18:19]
12Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji.
13Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia.[#2 Fal 8:29; 2 Nya 22:8]
14Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arubaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.
15Alipotoka huko akamkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu akija kumlaki; akamsalimu akamwambia, Je! Moyo wako umenyoka, kama moyo wangu ulivyo pamoja na moyo wako? Akajibu Yehonadabu, Ndio. Yehu akamwambia, Kama ndio, nipe mkono wako. Akampa mkono, akamkalisha pamoja naye garini.[#Yer 35:6; 1 Nya 2:55; Ezr 10:19]
16Akasema, Fuatana nami, ukaone wivu wangu kwa BWANA. Wakampandisha garini mwake.[#1 Fal 19:10; Mit 27:2; Mt 6:2; Rum 10:2]
17Naye alipofika Samaria, aliwaua wote wa Ahabu waliokuwa wamebakia katika Samaria, hata akamwangamiza, sawasawa na neno la BWANA alilomwambia Eliya.[#2 Fal 9:8; 2 Nya 22:8; Ayu 18:5-21; 21:17-30; Zab 34:16; 145:20; Mit 2:22; Mal 4:1; 1 Fal 21:21]
18Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.[#1 Fal 16:31,32]
19Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; yeyote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.[#1 Fal 22:6]
20Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu yeyote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.[#1 Fal 16:32]
22Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye BWANA, ila wamwabuduo Baali peke yao.
24Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.[#1 Fal 20:39]
25Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maofisa, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maofisa wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.
26Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.[#1 Fal 14:23]
27Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.[#Ezr 6:11; Dan 2:5; 3:29]
28Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli.
29Walakini katika makosa yake Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, Yehu hakutoka katika kuyafuata, yaani, ndama za dhahabu zilizokuwako katika Betheli na Dani.[#Kut 32:4; 1 Fal 12:28,29; Hos 8:5,6]
30BWANA akamwambia Yehu, Kwa kuwa umetenda vema kwa kufanya vilivyo haki machoni pangu, kuitendea nyumba ya Ahabu sawasawa na yote yaliyomo moyoni mwangu, wana wako wa kizazi cha nne watakaa kitini mwa Israeli.[#2 Fal 13:1; 15:8,12]
31Lakini Yehu hakuangalia, aende katika sheria ya BWANA, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote; hakutoka katika makosa ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.[#Mit 4:23; Law 26:14,17; Kum 28:15; 1 Fal 12:30; 13:34; 14:16; 15:29,30,34; 16:2,3,26]
32Siku zile BWANA akaanza kupunguza Israeli. Hazaeli akawapiga kote mipakani mwa Israeli;[#2 Fal 8:12; 13:22]
33kutoka Yordani upande wa mashariki, nchi yote ya Gileadi, na ya Wagadi, na Wareubeni, na Wamanase, kutoka Aroeri iliopo karibu na bonde la Arnoni, yaani, Gileadi, na Bashani.[#Amo 1:3]
34Basi mambo yote ya Yehu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?
35Yehu akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoahazi mwanawe akatawala mahali pake.
36Na muda Yehu aliotawala juu ya Israeli katika Samaria ulikuwa miaka ishirini na minane.