2 Wafalme 13

2 Wafalme 13

Yehoahazi atawala Israeli

1Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba.

2Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha.

3Hasira ya BWANA ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote.[#Law 26:17; Kum 4:23,24; 6:13; Amu 2:14; Zab 7:11; Isa 10:5,6; 42:8; Nah 1:3,6; 2 Fal 8:12]

4Naye Yehoahazi akamsihi BWANA, BWANA akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa.[#Hes 21:7; Amu 6:6-8; Zab 78:34; 106:23; Yer 2:27; Kut 3:7; 2 Fal 14:26; Mit 15:3; Yer 32:19]

5(BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza.[#2 Fal 14:25,27; Lk 2:11]

6Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa katika Samaria).[#1 Fal 16:33]

7Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa.[#Amo 1:3]

8Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?

9Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake.[#13:9 Au, Yoashi.]

Yehoashi atawala Israeli

10Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita.

11Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo.

12Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli?[#2 Fal 14:9,15; 2 Nya 25:17]

13Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.

Kifo cha Elisha

14Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akateremka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake![#2 Fal 2:12; Ayu 22:30]

15Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale.

16Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.[#Mwa 49:24; 2 Fal 4:34]

17Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.[#1 Fal 20:26]

18Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha.[#Kut 17:11]

19Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.

20Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka.[#2 Fal 5:2; 6:33]

21Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu.[#2 Fal 4:35; Mt 27:52; Yn 5:25-29]

Israeli wateka miji ya Aramu

22Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi.[#2 Fal 8:12]

23Lakini BWANA akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado.[#Kut 33:19; Amu 10:16; Neh 9:31; 2 Fal 14:27; Isa 30:18,19; Yer 12:15; Omb 3:32; Eze 20:9; Kut 2:24,25; 32:13; Mik 7:20; Lk 1:54,55,72,73]

24Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake.

25Naye Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, akaitwaa tena mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli miji ile aliyoitwaa yeye mkononi mwa Yehoahazi baba yake vitani. Mara tatu Yehoashi akamshinda, akairudisha miji ya Israeli.[#2 Fal 18:19]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya