The chat will start when you send the first message.
1Basi Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na nane wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka kumi na miwili.[#2 Fal 1:17; #3:1 Au, Yehoramu.]
2Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA; ila si kama baba yake na kama mama yake; maana akaiondoa ile nguzo ya Baali aliyoifanya baba yake.[#1 Fal 16:31,32]
3Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha.[#2 Fal 10:28-31; 1 Fal 12:28-32]
4Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli wana-kondoo elfu mia moja na sufu ya kondoo dume elfu mia moja.[#Mwa 13:2; Ayu 1:3; Isa 16:1]
5Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli.[#2 Fal 1:1]
6Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote.
7Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.[#1 Fal 22:4]
8Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu.
9Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata.[#Kut 11:8]
10Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.[#Zab 78:34; Mit 19:3; Isa 8:21]
11Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hakuna nabii yeyote hapa wa BWANA ili tumwulize yeye shauri la BWANA? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya.[#1 Fal 22:7; Amo 3:7; 1 Nya 22:12; Zab 55:22; Mit 3:5,6]
12Yehoshafati akasema, Neno la BWANA analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia.[#2 Fal 2:25]
13Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa BWANA amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.[#Eze 14:3; Amu 10:14; Rut 1:15; 1 Fal 18:19]
14Elisha akasema, Kama BWANA wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe.[#1 Fal 17:1; 2 Fal 5:16; Zab 15:4]
15Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa BWANA ukamjia juu yake.[#1 Sam 10:5; Eze 1:3; 3:14,22; 8:1]
16Akasema, BWANA asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki.[#2 Fal 4:3]
17Kwa kuwa BWANA asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng'ombe zenu, na wanyama wenu.[#Zab 107:35]
18Na jambo hili ni jepesi machoni pa BWANA; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu.[#Yer 32:17,27; Mk 10:27; Lk 1:37; Efe 3:20; 1 Fal 20:28]
19Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe.[#1 Sam 15:3]
20Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji.[#Kut 29:39,40]
21Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani.
22Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likametameta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu.
23Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana wenyewe kwa wenyewe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo!
24Hata walipokuja kambini mwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga Wamoabi hadi kwao.
25Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga.[#Isa 16:7,11]
26Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki.
27Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.[#Amo 2:1; Law 18:21; 20:2; Kum 12:31; 18:10; 2 Fal 17:17; 2 Nya 28:3; Zab 106:37,38; Yer 7:31; 32:35; Eze 16:20; 23:37]