2 Wathesalonike 1

2 Wathesalonike 1

Salamu

1Paulo, Silwano na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo.[#Mdo 17:1; 1 The 1:1]

2Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo.[#Rum 1:7]

Shukrani

3Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi.[#1 The 1:2,3; 2 The 2:13]

4Hata na sisi wenyewe tunaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya subira yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili.[#2 Kor 7:4; Ufu 1:9; 1 The 2:19; 3:2,7]

Hukumu wakati wa kuja kwa Yesu

5Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa.[#1 The 2:12; Flp 1:28; Lk 21:36]

6Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi;[#Ufu 18:6,7; Rum 12:19]

7na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake,[#Mt 25:31; 1 The 3:13; 4:16]

8katika muali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;[#Rum 2:8; Isa 66:15; Yer 10:25; Zab 79:6; 1 Pet 4:17]

9watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;[#Isa 2:10,19,21]

10yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu).[#1 The 3:13; Kol 3:4; Zab 89:7; 69:36; Isa 49:3; 2:11,17]

11Kwa hiyo tunawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu;[#1 The 1:2,3]

12jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.[#Isa 24:15; 66:5; Mal 1:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya