2 Wathesalonike 3

2 Wathesalonike 3

Hitaji la maombi

1Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa kote kama ilivyo kwenu;[#Kol 4:3; 1 The 5:25]

2na tukaokolewe kutoka kwa watu wasio haki, na waovu, maana si wote walio na imani.

3Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda kutoka kwa yule mwovu.[#1 The 5:24]

4Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza na kwamba mtaendelea kuyafanya.[#1 The 4:10; Gal 5:10; 2 Kor 7:16]

5Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na subira ya Kristo.

Onyo juu ya kutofanya kazi

6Ndugu, tunawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu kutoka kwa kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu.[#Mt 18:17; Rum 16:17; 1 The 5:14; 4:1]

7Mnajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu;[#1 The 2:1; 1:6]

8wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulifanya kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.[#1 Kor 4:12; Flp 3:17; 1 The 2:9]

9Si kwamba hatuna haki hiyo, ila kwa makusudi ya kuwapa mfano wa kuiga, mtufuate.[#Mt 10:10; 1 Kor 4:16; 1 The 1:6,7]

10Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.[#Mwa 3:19; 1 The 3:4; 4:11]

11Maana tunasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.[#1 The 5:14]

12Basi tunawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, wafanye kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.[#1 The 4:11]

13Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.[#Gal 6:9]

14Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la barua hii, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari;[#1 Kor 5:9,11]

15lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.[#1 The 5:13,14]

Salamu za mwisho na baraka

16Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote.[#1 The 5:23]

17Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila barua yangu, ndio mwandiko wangu.[#1 Kor 16:21]

18Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya