Amosi 5

Amosi 5

Maombolezo kwa ajili ya dhambi ya Israeli

1Lisikieni neno hili nilitamkalo liwe maombolezo juu yenu, enyi nyumba ya Israeli.[#Yer 7:29]

2Bikira wa Israeli ameanguka;

hatainuka tena;

Ameangushwa katika nchi yake;

hakuna mtu wa kumwinua.

3Kwa kuwa Bwana MUNGU asema hivi; Mji uliotoka nje wenye watu elfu moja, utabakiziwa watu mia moja, na mji uliotoka wenye watu mia moja, utabakiziwa watu kumi, kwa nyumba ya Israeli.

4Maana BWANA awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi;[#2 Nya 15:2; Isa 55:3]

5bali msitafute Betheli, wala msiingie Gilgali, wala msipite kwenda Beer-sheba; kwani Gilgali hakika yake itakwenda utumwani, na Betheli itakuwa ubatili.[#Amo 4:4; 8:14]

6Mtafuteni BWANA, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli.

7Ninyi mnaogeuza hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini,

8mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA, ndilo jina lake;[#Ayu 9:9; 38:31,34; Amo 4:13]

9yeye aletaye uharibifu wa ghafla juu ya wenye nguvu, hata kuiharibu ngome.

10Wao humchukia yeye akemeaye langoni, nao humzira anenaye maneno ya adili.[#Isa 29:21; 1 Fal 22:8]

11Basi, kwa kuwa mnamkanyaga maskini, na kumtoza ngano; ninyi mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, lakini hamtakaa ndani yake; ninyi mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake.[#Mik 6:15; Sef 1:13]

12Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao.[#Isa 29:21]

13Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya.

14Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo BWANA, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo.[#Zab 34:12-16; Mit 11:27; Isa 1:16,17; Mik 6:8; Mt 7:7; Rum 2:7-9; Mik 3:11]

15Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.[#Rum 12:9; Kut 32:30]

16Kwa ajili ya hayo, asema BWANA, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza.[#Yer 9:17]

17Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema BWANA.[#Kut 12:12]

Siku ya BWANA; siku ya giza

18Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwa nini kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru.[#Isa 5:19; Eze 12:22; Mal 3:1; 2 Pet 3:4]

19Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

20Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.

21Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini.[#Isa 1:11]

22Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona.

23Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.

24Lakini hukumu na iteremke kama maji, na haki kama maji makuu.

25Je! Mliniletea dhabihu na sadaka jangwani muda wa miaka arubaini, enyi nyumba ya Israeli?[#Mdo 7:42]

26Naam, mtamchukua Sikuthi, mfalme wenu, na Kiuni, sanamu zenu, nyota ya mungu wenu, mliojifanyia wenyewe.

27Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni, mwende mbali kupita Dameski, asema BWANA, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya