The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo BWANA amelithibitisha neno lake alilolinena juu yetu ya waamuzi wetu walioamua Israeli, na juu ya wafalme wetu, na juu ya wakuu wetu, na juu ya watu wa Israeli na Yuda,
2kwa kutuletea mapigo makubwa, ambayo chini ya mbingu zote hayakutokea kama yalivyotokea Yerusalemu, sawasawa na mambo yaliyoandikwa katika Torati ya Musa.
3Yaani, tule kila mtu nyama ya mwana wake mwenyewe na kila mtu nyama ya binti yake mwenyewe.
4Zaidi ya hayo, amewatiisha chini ya falme zote zinazotuzunguka, kuwa lawama na ukiwa katikati ya watu wote wa nchi zote BWANA alizowatawanya.
5Hivyo walikuwa chini, wala si juu, kwa sababu tulimkosa Bwana MUNGU wetu kwa kuwa hatukumsikiliza sauti yake.
6Kwa Bwana MUNGU wetu, haki; lakini kwetu na kwa baba zetu haya ya uso, kama hivi leo.
7Mapigo haya yote yametupata aliyoyataja BWANA juu yetu,
8lakini hata hivi hatukuomba radhi kwa BWANA, kwa kuyaacha kila mtu mawazo ya moyo wake mbaya.
9Kwa hiyo Mungu ameyavizia mapigo hayo akatuletea, maana BWANA ni mwenye haki katika kazi zake zote alizotuamuru.
10Lakini sisi hatukuitii sauti yake, kwenda katika amri za BWANA alizoziweka mbele yetu.
11Na sasa, Ee Bwana, MUNGU wa Israeli, uliyewatoa watu wako katika nchi ya Misri kwa mkono hodari, na kwa ishara na maajabu na uweza mwingi, na kwa mkono ulioinuliwa, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo.
12Ee Bwana MUNGU wetu, tumefanya dhambi; tumetenda maovu; tumezivunja sheria zako.
13Hasira yako igeuzwe mbali nasi, maana tumesalia wachache tu katikati ya mataifa ulikotutawanya.
14Yasikilize maombi yetu, Ee BWANA, na dua zetu; utuokoe kwa ajili yako mwenyewe; utupe kibali machoni pao waliotuchukua mateka;
15ili dunia yote ijue ya kuwa Wewe ndiwe Bwana MUNGU wetu, kwa sababu Israeli na uzao wake wanaitwa kwa jina lako.
16Ee BWANA, tazama kutoka makazi yako matakatifu mbinguni, utuangalie;
17fumbua macho yako uone; maana wafu walioko kuzimu, ambao pumzi yao imeondolewa mwilini mwao, hawatampa BWANA utukufu wala haki.
18Bali moyo ulioteseka, na miguu iliyodhoofika na kulegea, na macho yanayozimia, na roho yenye njaa, ndivyo vitakavyokupa utukufu na haki, Ee BWANA.
19Maana hatukutolei maombi yetu, Ee Bwana MUNGU wetu, kwa sababu ya haki ya baba zetu na ya wafalme wetu.
20Wewe umepeleka ghadhabu yako na hasira yako juu yetu kama ulivyonena kwa kinywa cha watumishi wako manabii.
21BWANA asema, Inamisheni mabega yenu kumtumikia mfalme wa Babeli, mkae katika nchi niliyowapa baba zenu.[#Yer 7:34; 27:10-12]
22Lakini kama hamtaisikia sauti ya BWANA kumtumikia mfalme wa Babeli,
23nitakomesha katika njia za Yuda sauti ya kicheko na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi; na nchi yote itakuwa ukiwa asibaki mwenyeji ndani yake.
24Walakini sisi hatukutaka kuisikiliza sauti yako, tumtumikie mfalme wa Babeli. Kwa hiyo umeyathibitisha maneno yako uliyoyanena kwa watumishi wako manabii, ya kuwa mifupa ya wafalme na mifupa ya baba zetu itaondolewa mahali pao.[#Yer 8:1-2]
25Na, tazama, imetawanywa juani mchana, na katika barafu usiku; na walikufa kwa mateso makali, kwa njaa na kwa upanga na kwa tauni.
26Hata nyumba iliyoitwa kwa jina lako umeifanya ukiwa, kama ilivyo leo, kwa sababu ya uovu wa nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
27Hata hivi, Ee Bwana MUNGU wetu, umetutendea kwa kadiri ya fadhili zako zote, na kwa kadiri ya rehema zako nyingi,
28kama ulivyosema kwa mtumishi wako Musa, siku ile uliyomwagiza aiandike sheria yako mbele ya wana wa Israeli, ukisema,[#Kum 28:58-62]
29Msipotaka kuisikiliza sauti yangu, hakika msongano huu mkubwa wa watu wengi utakuwa hesabu ndogo kabisa katikati ya mataifa nitakakowatapanya.
30Maana najua hawatanisikia, kwa kuwa ni watu wenye shingo gumu; lakini katika nchi ya uhamisho wao watatafakari,
31na kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana MUNGU wao. Nami nitawapa moyo, na masikio ya kusikia,
32nao wataisifu katika nchi ya uhamisho wao na kulikumbuka jina langu.
33Watageuka na kuacha ugumu wao na matendo yao mabaya, kwa sababu wataikumbuka njia ya baba zao waliotenda dhambi mbele ya BWANA.
34Nitawarudisha katika nchi niliyowaapia baba zao, Abrahamu na Isaka na Yakobo, nao wataimiliki. Nami nitawaongeza, wala hawatapungua.
35Nami nitafanya agano la milele pamoja nao kwamba nitakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wangu, wala sitawahamisha watu wangu tena kutoka nchi yao niliyowapa.[#Yer 32:38-40]