The chat will start when you send the first message.
1Ndipo tukageuka, tukashika maisha ya jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia BWANA; tukaizunguka milima ya Seiri siku nyingi.[#Hes 21:4]
2BWANA akasema, akaniambia,
3Mmeuzunguka mlima huu vya kutosha; geukeni upande wa kaskazini.
4Nawe waagize watu, uwaambie, Mtapita katika mpaka wa ndugu zenu wana wa watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa Esau waishio Seiri; nao watawaogopa; basi jihadharini sana;[#Mwa 36:8]
5msipigane nao; kwa kuwa sitawapa sehemu ya nchi yao kamwe, hata kiasi cha kukanyaga wayo wa mguu; kwa kuwa nimempa Esau milima ya Seiri kuwa milki yake.[#Mwa 36:8; Kum 32:8; Yos 24:4; 2 Nya 20:10-12; Zab 115:3; 135:5,6; Dan 4:32,35; Mdo 17:26]
6Nunueni vyakula kwao kwa fedha, mpate kula; na maji nayo nunueni kwao kwa fedha, mpate kunywa.
7Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, amekubariki katika kazi yote ya mkono wako; amejua ulivyotembea katika jangwa kubwa hili; miaka arubaini hii alikuwa nawe BWANA, Mungu wako; hukukosa kitu.
8Basi tukapita kando yao ndugu zetu wana wa Esau, waishio Seiri kutoka njia ya Araba, kutoka Elathi na kutoka Esion-geberi.[#1 Fal 9:26; 2 Fal 14:22; 16:6]
Tukageuka tukapita njia ya bara ya Moabu.
9BWANA akaniambia, Usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki.[#Mwa 19:37; Hes 21:28; Zab 83:8]
10(Walioishi humo hapo kale ni Waemi, nao ni watu wakubwa, wengi, warefu, mfano wa Waanaki;[#Mwa 14:5; Hes 13:22; Kum 9:2]
11na hawa nao wadhaniwa kuwa Warefai kama Waanaki; lakini Wamoabi huwaita Waemi.[#2:11 Katika Kiebrania ni majitu.]
12Na Wahori nao walikuwa wakikaa Seiri hapo kale, lakini wazawa wa Esau waliwafuata; wakawaangamiza mbele yao, wakakaa badala yao; kama alivyofanya Israeli nchi ya milki yake aliyopewa na BWANA.)[#Mwa 14:6; 36:20; 1 Nya 1:38-42]
13Sasa basi ondokeni, mkakivuke kijito cha Zeredi. Nasi tukakivuka kile kijito cha Zeredi.
14Na siku tulizokuwa tukienda kutoka Kadesh-barnea hata tulipovuka kijito cha Zeredi, ilikuwa ni miaka thelathini na minane; maana, hata walipokwisha kuangamizwa watu wa vita kutoka kati ya kambi, kizazi chao chote, kama walivyoapiwa na BWANA.[#Hes 14:28-35; 26:64; 32:11; Zab 78:33; 90:3-9; Kum 1:34,35; Eze 20:15]
15Tena mkono wa BWANA ulikuwa juu yao ili kuwaangamiza, kuwatoa katika kambi hadi walipouwawa.[#1 Sam 5:6-11; 7:13; Zab 95:10,11; 106:26; Ebr 3:11-19; 4:1-5]
16Basi ikawa, walipoangamizwa kwa kufa watu wote wa vita waliokuwemo,
17BWANA aliniambia, akasema,
18Hivi leo ivuke Ari, mpaka wa Moabu;
19na utakaposongea kuwaelekea wana wa Amoni, usiwasumbue wana wa Amoni, wala usishindane nao; kwa kuwa sitakupa katika nchi ya hao wana wa Amoni kuwa milki yako; kwa sababu nimewapa wana wa Lutu iwe milki yao.[#Mwa 19:38; 14:5]
20(Nchi hiyo nayo yadhaniwa kuwa ni nchi ya Warefai, hapo kale Warefai walikaa humo; lakini Waamoni huwaita Wazamzumi;
21nao ni watu wengi, wakubwa, warefu, kama Waanaki; lakini BWANA aliwaangamiza mbele yao; wakawafuata wakakaa badala yao;
22kama vile alivyowafanyia wana wa Esau, waliokaa Seiri, alipowaangamiza Wahori mbele yao; wakawafuata, wakakaa badala yao hadi hivi leo;[#Mwa 36:8; Ayu 12:23]
23na Waavi waliokuwa wakikaa katika vijiji mpaka Gaza waliangamizwa na Wakaftori waliotoka Kaftori, na hawa wakakaa badala yao.)[#Yos 13:3; Yer 25:20; Sef 2:4; Zek 9:5; Mwa 10:14; Amo 9:7]
24Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano.[#Hes 21:13,14; Amu 11:18]
25Hivi leo nitaanza mimi kutia utisho wako na kuhofiwa kwako juu ya watu walio chini ya mbingu kila mahali, watakaosikia uvumi wako, na kutetemeka, na kuingiwa na uchungu kwa sababu yako.[#Kut 15:14; Kum 11:25; Yos 2:9]
26Nikatuma wajumbe kutoka bara ya Kedemothi kwenda kwa Sihoni mfalme wa Heshboni na maneno ya amani, kusema.[#Kum 20:10; Est 9:30]
27Nipishe katikati ya nchi yako; nitakwenda kwa njia ya barabara, sitageuka kwenda mkono wa kulia wala wa kushoto.[#Hes 21:21; Amu 11:19]
28Nawe uniuzie chakula kwa fedha nile; unipe na maji kwa fedha, ninywe; ila unipishe katikati kwa miguu yangu, hayo tu;[#Hes 20:19]
29kama walivyonifanyia hao wana wa Esau waishio Seiri, na hao Wamoabi waishio Ari; hata nivuke Yordani niingie nchi tupewayo na BWANA, Mungu wetu.[#Kum 23:3; Amu 11:17]
30Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni hakutuacha kupitia kwake; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, alifanya roho yake kuwa ngumu, akamtia ukaidi moyoni mwake, apate kumtia mkononi mwako kama alivyo hivi leo.[#Hes 21:23; Yos 11:19,20; Kut 4:21; Hos 4:17; Yak 1:13-15]
31Kisha BWANA akaniambia, Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako; anza kuimiliki, upate kuirithi nchi yake.
32Ndipo Sihoni alipojitokeza juu yetu, yeye na watu wake wote ili kupigana nasi huko Yahasa.
33BWANA, Mungu wetu, akamtoa mbele yetu, tukampiga yeye na wanawe, na watu wake wote.[#Kut 23:31; Kum 7:2; 20:16; Zab 135:10-12; 136:18-20; Kum 29:7]
34Tukatwaa miji yake yote wakati huo, tukaharibu kabisa kila mji uliokuwa na wanaume, wanawake na watoto; tusimbakize hata mmoja;[#Law 27:28; Hes 21:2,3; Kum 7:2,26; Yos 7:11; 8:25,26; 9:24; 11:14; 1 Sam 15:3-9]
35ila ng'ombe zao tuliwatwaa kuwa mawindo yetu, pamoja na nyara za miji tuliyoitwaa.
36Kutoka Aroeri iliyo katika ukingo wa bonde la Arnoni, na huo mji ulio ndani ya bonde, mpaka kufika Gileadi, hapakuwa na mji uliokuwa na ngome ndefu ya kutushinda; BWANA, Mungu wetu, aliiweka wazi yote mbele yetu; ila nchi ya wana wa Amoni hukuisongelea;[#Kum 3:12; 4:48; Yos 13:9; Zab 44:3]
37upande wote wa mto wa Yaboki, na miji ya nchi ile ya milimani, na kila mahali alipotukataza BWANA, Mungu wetu.[#Mwa 32:22; Hes 21:24; Kum 3:16]