Esta 1

Esta 1

Mfalme Ahasuero amfukuza malkia Vashti

1Katika nyakati za Ahasuero; Ahasuero aliyetawala mikoa mia moja ishirini na saba, kutoka India mpaka Kushi;[#Est 8:9; Dan 6:1; #1:1 au Ethiopia.]

2siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Susa, mji mkuu ngomeni;[#2 Sam 7:1; Dan 4:4; Neh 1:1; Dan 8:2]

3mwaka wa tatu wa kutawala kwake, ikawa aliwafanyia karamu wakuu na mawaziri wake; wakuu wa majeshi ya Uajemi na Umedi; watu maarufu na wakuu wa mikoa, wakihudhuria mbele zake.[#Mwa 40:20; Est 2:18; Dan 5:1; Mk 6:21]

4Akawaonesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, yaani siku mia moja na themanini.

5Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani mji mkuu, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika ukumbi wa bustani ya ngome ya mfalme.

6Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawati, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu yenye nakshi ya vito vyekundu, marumaru, lulu za manjano na nyeusi na mawe ya thamani.[#Est 7:8; Amo 2:8]

7Wakawanywesha kileo katika vyombo mbalimbali vya dhahabu, na divai tele ya kifalme, kufuatana na ukarimu wa ufalme;

8Walikunywa kama ilivyoamriwa, bila kushurutishwa; maana mfalme aliwaagiza watumishi wahudumie kila mtu kadiri ya mahitaji yake.

9Naye Vashti, malkia, akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero.

10Katika siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale Matowashi saba, wasimamizi wa nyumba saba waliohudumu mbele zake,

11wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, akiwa amevaa taji la kifalme; ili kuwaonesha watu na wakuu uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.[#Mit 16:9]

12Bali Vashti, malkia, hakutii amri ya mfalme, alikataa kuja kama alivyoamriwa na mfalme kupitia kwa matowashi; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.

13Basi mfalme akawaambia wenye hekima, waliojua sheria; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu;[#Yer 10:7; Dan 2:12; 1 Nya 12:32; Isa 7:14; Dan 9:24; Mal 3:1; Mt 16:3; #1:13 au walio na elimu ya nyakati.]

14na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale wakuu saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza,[#Ezr 7:14]

15Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi wa nyumba?

16Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na wakuu, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na wakuu wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero.

17Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja.

18Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliozisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maofisa wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.

19Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye.

20Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo.[#Efe 5:22,23; Kol 3:18; 1 Pet 3:1]

21Basi neno hili likawapendeza mfalme na wakuu wake; naye mfalme akafanya kama alivyopendekeza Memukani.

22Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake.[#Est 8:9; Efe 5:22-24]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya