Esta 8

Esta 8

Esta Awaokoa Wayahudi

1Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akaja mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu.[#Est 2:7]

2Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani.[#Mwa 41:42; Est 3:10; Dan 5:29; Lk 15:22]

3Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi.

4Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme.[#Est 4:11]

5Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, na iandikwe amri kuzitangua barua za Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika mikoa yote ya mfalme.

6Maana, ninawezaje kustahimili kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au kuyatazama maangamizi ya jamaa zangu?[#Neh 2:3; Zab 137:6]

7Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, akasema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi.[#Mit 13:22]

8Basi nanyi pia waandikieni Wayahudi vyovyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie mhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa mhuri kwa pete ya mfalme, hakuna awezaye kulitangua.[#Dan 6:8; 2 Tim 2:19]

9Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na wakuu wa tarafa na wakuu wa mikoa kuanzia Bara Hindi mpaka Kushi, mikoa mia moja na ishirini na saba, kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao.[#Est 3:12; 1:1,22]

10Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia mhuri kwa pete ya mfalme, barua zikapelekwa na matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme.[#1 Fal 21:8]

11Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji wakusanyike na kuyalinda maisha yao, kwa kuangamiza, kuua, na kulimaliza jeshi lote la watu au mkoa watakaowashambulia, pamoja na watoto na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara;[#Est 3:13; Isa 10:6]

12siku moja, katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.[#Kut 15:9,10]

13Nakala ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao.[#Est 3:14,15]

14Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Susa mjini.

15Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawati na nyeupe, mwenye taji kubwa la dhahabu, na joho la kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Susa wakapaza sauti, wakashangilia.[#Mit 28:12,18]

16Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi.[#Est 9:17; Ayu 11:17; Zab 18:28; Mit 4:18]

17Na katika kila mkoa, na kila mji, popote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, maana waliwaogopa Wayahudi.[#1 Sam 25:8; Neh 8:10; Zab 18:43; Mwa 35:5; Kut 15:16; Kum 2:25; Est 8:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya