The chat will start when you send the first message.
1Basi majina ya wana wa Israeli walioingia Misri ni haya; kila mtu pamoja na jamaa zake walikuja pamoja na Yakobo.[#Mwa 32:28; 46:8-27; Kut 6:14]
2Reubeni, na Simeoni na Lawi, na Yuda;
3na Isakari, na Zabuloni, na Benyamini;
4na Dani, na Naftali, na Gadi, na Asheri.
5Na wale watu wote waliotokana na uzao wa Yakobo walikuwa watu sabini; na huyo Yusufu alikuwa huko ndani ya Misri tangu hapo.[#Mwa 46:26; Kum 10:22]
6Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile.[#Mwa 50:26; Mdo 7:15; Mhu 1:4]
7Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao.[#Mdo 7:17; Mwa 46:3; Kum 26:5; Zab 105:24]
8Basi akatokea mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.[#Mdo 7:18]
9Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.[#Zab 105:24]
10Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.[#Mdo 7:19; Zab 10:2; 83:3; Ayu 5:13; Mit 28:16]
11Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.[#Mwa 15:1; Kut 2:11; 3:7; 5:4; Mit 27:3; Zab 81:6; Mwa 47:11]
12Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Ndipo Wamisri wakaogopa kwa sababu ya wana wa Israeli.
13Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali;
14wakafanya maisha yao kuwa machungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali.[#Kut 2:23; 22:21; Law 25:14,17; Hes 20:15; Ayu 20:19; Mit 14:31; 22:22; Mdo 7:19,34; Zab 10:17,18; 81:6]
15Kisha mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua;
16akasema, Wakati mnapowazalisha wanawake wa Kiebrania na kuona kuwa ni mtoto wa kiume basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto wa kike, na aishi.
17Lakini hao wakunga walikuwa wacha Mungu, hawakufanya kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale watoto wa kiume.[#Mit 16:6; Dan 3:16,18; 6:13; Mdo 5:29]
18Basi mfalme wa Misri akawaita wale wakunga na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili la kuwahifadhi watoto wa kiume wawe hai?
19Wakunga wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mkunga hajapata kuwafikia.[#Yos 2:4; 2 Sam 17:19,20]
20Basi Mungu akawatendea mema wale wakunga; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi.[#Mit 11:18; Mhu 8:12; Isa 3:10; Ebr 6:10]
21Ilikuwa kwa sababu wale wakunga walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba.[#1 Sam 2:25; 2 Sam 7:11,13,27,29; 1 Fal 2:24; 11:38; Zab 127:1]
22Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake wote, akisema, Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto wa kike mtamhifadhi hai.[#Mdo 7:19]