Kutoka 14

Kutoka 14

Kuvuka Bahari Nyekundu

1BWANA akasema na Musa, akamwambia,

2Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari.[#Hes 33:7; Yer 44:1]

3Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, lile jangwa limewazuia wasitoke.[#Zab 35:21; 71:11]

4Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. Basi wakafanya hivyo.[#Yak 1:13-17; Kut 9:16; Rum 9:17-23]

5Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?

6Akaandaa gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye;

7tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maofisa wa kijeshi juu ya magari hayo yote.

8Na BWANA akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa jeuri.[#Kut 6:1; 13:9; Hes 33:3; #14:8 Katika tafsiri nyingine ni ‘ushupavu au ulinzi wa BWANA’.]

9Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi wote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata wakiwa wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni.[#Kut 15:9; Yos 24:6]

10Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli walipoangalia nyuma na kuona Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.[#Yos 24:7; Neh 9:9; Zab 34:17; 107:6]

11Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?[#Zab 106:7]

12Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.[#Kut 6:9]

13Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.[#2 Nya 20:15,17; Isa 41:10-14]

14BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.[#Kum 20:4; Yos 10:14; 23:3; 2 Nya 20:29; Neh 4:20; Isa 30:15; 31:4]

15BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.

16Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu.[#Kut 7:19]

17Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake.[#Mit 29:1]

18Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi wake.

19Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao;[#Mwa 48:16]

20ikawa katikati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha.[#Isa 8:14; 2 Kor 4:3]

21Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika.[#Yos 3:16; 4:23; Neh 9:11; Zab 74:13; 106:9]

22Wana wa Israeli wakaenda ndani wakipita kwenye nchi kavu ndani ya bahari; huku maji yakiwa ukuta kwao mkono wa kulia na mkono wa kushoto.[#1 Kor 10:1-2; Ebr 11:29; Kut 15:19; Hes 33:8; Zab 66:6; 78:13]

23Na wale Wamisri wakawafuata, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi wote wa Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake.

24Ikawa katika zamu ya alfajiri, BWANA akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri.

25Akayakwamisha magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa shida; na Wamisri wakasema, Na tuwakimbieni Waisraeli; kwa kuwa BWANA anawapigania.[#14:25 Katika Kiebrania ni ‘akayaondoa magurudumu’.]

Wamisri wazama

26BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi wao.

27Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji na BWANA akawaangamiza hao Wamisri katika bahari.[#Yos 4:18]

28Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.[#Kum 11:4; Zab 78:53; Neh 9:11; Hab 3:8]

29Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kulia, na upande wao wa kushoto.[#Zab 77:20; 78:52,53]

30Ndivyo BWANA alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni mwa bahari, wamekufa.[#Zab 106:8-10; 58:10; 59:10]

31Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya BWANA juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha BWANA, wakamwamini BWANA, na Musa mtumishi wake.[#Kut 19:9; Yn 2:11; 11:45]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya